Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 8 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo15...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Natumaini mmeamka salama na mnaendelea vyema/Mmeanza vyema na Mungu,Andelee Kutubariki katika Kazi,Biashara,Masomo,kwenye Vyombo vya usafiri,njiani/Tutembeapo,Vilaji/Vinywaji,Tuingiapo/Tutokapo,
Mungu baba akatupe/Akatufanyie sawaswa na Mapenzi Yake.
Wagonjwa,Walio Magerezani pasipo na hatia,Wafiwa,wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu,Mungu Baba akawaguse na kuwaponya...
Baba Mungu ukaibariki na kuiponya Nchi yetu Tanzani,Ukabariki Afrika nzima Baba,Baba pia na Ubariki hapa tunapoishi, Na Dunia Nzima Mfalme wa Amani ukatawale na Kuongoza...Mfalme wa Amani ukawaguse wanaotuongoza ukawape kutenda sawasawa na mapenzi yako...
Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni katika yote...
Tunaomba na Kushukuru..Amina.!!!!
Mungu akawe nanyi.


Agano la Mungu na Abramu

1Baada ya mambo hayo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Abramu katika maono, “Abramu! Usiogope! Mimi ni ngao yako. Tuzo lako litakuwa kubwa!” 2Lakini Abramu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, utanipa nini hali naendelea kuishi bila mtoto, na mrithi wangu ni Eliezeri wa Damasko? 3Tazama! Hujanijalia mtoto; mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye atakayekuwa mrithi wangu!”
4Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Huyu hatakuwa mrithi wako! Mwanao halisi ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5Hapo Mwenyezi-Mungu akamleta Abramu nje na kumwambia, “Tazama mbinguni! Zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu! Hivyo ndivyo wazawa wako watakavyokuwa wengi!” 6Abramu akamwamini Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamkubali Abramu kuwa mwadilifu.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyekuleta toka Uri, mji wa Wakaldayo, ili nikupe nchi hii uimiliki.” 8Lakini Abramu akamwambia, “Ee Mwenyezi-Mungu, nitajuaje kwamba nitaimiliki nchi hii?” 9Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa.” 10Abramu akamletea hao wote, akamkata kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika safu mbili, vikielekeana; lakini ndege hakuwakata vipande viwili. 11Na tai walipoijia hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza.
12Jua lilipokuwa likitua, Abramu alishikwa na usingizi mzito; hofu na giza nene vikamfunika. 13Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ujue hakika ya kwamba wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watakuwa watumwa na watateswa kwa muda wa miaka 400. 14Hata hivyo, nitaliadhibu taifa watakalolitumikia, na hatimaye watatoka wakiwa na mali nyingi. 15Lakini wewe mwenyewe utaishi maisha marefu na kufariki kwa amani. 16Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne, kwa sababu uovu wa Waamori haujakamilika bado.”
17Jua lilipokwisha tua na giza kuingia, tanuri ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama. 18Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu akafanya agano na Abramu akisema, “Wazawa wako ninawapa nchi hii, toka mto wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrate, 19yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, 20Wahiti, Waperizi, Warefai, 21Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
Mwanzo15;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN): 
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 7 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo14...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu yu mwema sana na tuzidi Kumtukuza,Kumsifu,Kumshukuru ,Yeye aliyetupa kuiona Leo hii
kwa mapenzi yake na si kwa utashi,nguvu zetu au kwamba sisi ni wema sana..ni Kwa Neema/Rehema zake tuu kwakutuchagua sisi...
Asante sana Mungu wetu uliye mkuu,Uliyetukuka,Unayetupa ridhiki,Uliyetupa Afya,Uliyetupa kibali chako cha kuendelea  nasi katika maisha haya ya Dunia hii yenye mambo meengi...Ukatulinde na kutubariki katika Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri na tutembeapo,ukabariki Kuingia/Kutoka kwetu,Vilaji/Vinywaji..Na vyote tunavyoenda kugusa/Kutumia Baba ukavitakase na Kuvifunika/Kuviosha kwa Damu yako..
Tunakwenda kinyume na Roho chafu,Nguvu za giza,Kukata tamaa,Kukataliwa,Magonjwa Shida/Tabu
Baba ukatulinde na kutuokoa...Tunayakabidhi haya yote tuliyoyanena, tunayoyawaza/Yaliyo moyoni mwetu Baba yote unayajua..
Tunaomba na Kushukuru,Tukiamini wewe ni Baba Mungu wetu na Mwokozi wetu..Amina..!!
Muwe na wakati mwema.


Abramu anamwokoa Loti
1Wakati huo, mfalme Amrafeli wa Shinari, mfalme Arioko wa Elasari, mfalme Kedorlaomeri wa Elamu na mfalme Tidali wa Goiimu, 2walipigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, dhidi ya Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na dhidi ya mfalme wa Bela (yaani Soari). 3Wafalme hao watano waliyaunganisha majeshi yao katika bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). 4Kwa muda wa miaka kumi na miwili walikuwa wakimtii mfalme Kedorlaomeri, lakini mnamo mwaka wa kumi na tatu, walimwasi. 5Mnamo mwaka wa kumi na nne, mfalme Kedorlaomeri na wale wafalme wenzake walikuja na kuwashinda watu wa Refaimu huko Ashtaroth-karnaimu, na Wazuzi huko Hamu, na Waemi huko Shawe-kiriathaimu, 6na Wahori huko mlimani kwao Seiri, wakawafukuza hadi Elparani, mpakani mwa jangwa. 7Kisha wakarudi nyuma mpaka Enmishpati (yaani Kadeshi), wakaivamia nchi yote ya Waamaleki, na kuwashinda Waamori waliokaa Hasason-tamari.
8Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela 9(yaani Soari), wakaingia vitani katika bonde la Sidimu kupigana na Kedorlaomeri mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari na Arioko mfalme wa Elasari; wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. 10Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami; kwa hiyo wafalme wa Sodoma na Gomora walipokuwa wakiikimbia vita, wakatumbukia humo, lakini wengine wakatorokea mlimani. 11Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. 12Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao.
13Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. 14Abramu alipopata habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka, akatoka na watu wake stadi 318 waliozaliwa katika nyumba yake, akawafuatia adui mpaka Dani. 15Huko, akaligawa jeshi lake katika makundi. Usiku, akawashambulia adui zake, akawashinda na kuwafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Damasko. 16Basi, Abramu akaikomboa mali yote iliyotekwa na adui, na kumkomboa Loti mpwa wake, mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.
Melkisedeki anambariki Abramu
17Abramu aliporudi baada ya kumshinda mfalme Kedorlaomeri na wenzake, mfalme wa Sodoma alitoka kwenda kumlaki katika bonde la Shawe, (yaani Bonde la Mfalme). 18Naye Melkisedeki, mfalme wa mji wa Salemu, ambaye alikuwa kuhani wa Mungu Mkuu, akaleta mkate na divai, 19akambariki Abramu akisema,
“Abramu na abarikiwe na Mungu Mkuu,
Muumba mbingu na dunia!
20Na atukuzwe Mungu Mkuu,
aliyewatia adui zako mikononi mwako!”
Naye Abramu akampa Melkisedeki mchango wake sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo.
21Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, lakini jichukulie mali yote wewe mwenyewe.” 22Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, aliyeumba mbingu na dunia, 23kwamba sitachukua uzi au kamba ya kiatu, wala chochote kilicho chako, usije ukajivuna na kusema kwamba umenitajirisha. 24Basi, sitachukua chochote isipokuwa tu vile vitu vijana wangu walivyokula na sehemu ya wale waliokuwa pamoja nami, Aneri, Eshkoli na Mamre ambao wana haki nayo.”
Mwanzo14;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 6 February 2017

Kikombe Cha Asubuhu;Mwanzo 13...

Shalom,Habari za Asubuhi,Mmeamkaje,Wapendwa/Waungwana?
Siku/wiki Nyingine tena kwa Neema/Rehema za Mungu tumebarikiwa kuiona leo hii..
Tunamshukuru sana Mungu kwa Neema hii,Tuanze wiki hii vyema kwa kumrudishia Mungu Utukufu na Sifa yeye
Astahiliye yote,Mungu wetu aliyeumba Mbingu na Nchi, Yeye ni kimbilio la wote,Yeye akatubariki kuingia/Kutoka kwetu
kwenye Vyombo vya usafiri,Akabariki Kazi zetu,Biashara,Akawaguse na kuwaongoza wanafunzi katika masomo yao, Wapate kukumbuka na kuelewa wanayofundishwa.
Akawaponye Wagonjwa walio Mahospitalini/Majumbani,Wenye Shida/Tabu,Wanaopitia Magumu/Majaribu wamgeukie Mungu na kuomba pasipo kikomo yeye anatosha..
Akawafariji wafiwa,Akawaguse Yatima na Wajane...Wafungwa walio Magerezani pasipo na hatia baba akawaguse, Waliofungwa kwa shida mbalimbali za kidunia,Shetani na minyororo yoyote ya nguvu za Giza Baba ukawafungue na Wakapate Uponyaji..
Tumshukuru Mungu na Kumtukuza,Kuomba na Kuamini yeye ni mwingi wa Huruma na Uponyaji..
Anza na Mungu naye hatokuacha....!!!!
Mungu awabariki Sana.



Abramu na Loti wanatengana

1Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. 2Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu. 3Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai, 4ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. 5Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema. 6Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja. 7Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
8Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja. 9Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora). 11Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani, akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana. 12Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma. 13Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu.

Abramu anaoneshwa nchi

14Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. 15Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele. 16Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika! 17Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.” 18Kwa hiyo, Abramu akangoa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre kule Hebroni; huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu.
Mwanzo 13;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili Mbarikiwe.

Friday, 3 February 2017

Wanawake na Maisha;Mwanamke/Mama huyu Mjane amenigusa..;Wanawake wengi wanapitia haya...







Shukrani;BongoStars

Haya mambo yanawakuta wanawake wengi wanapofiwa na waume/wenza wao,Inafikia baba wadogo/Ndugu wa mume wanawagombanisha mama na watoto...
Wewe imeshakukuta/kupitia haya matatizo, Au mtu wako wa karibu?
Mungu awabariki wamama wote na wote wanaopitia/waliopitia haya.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo12..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu muumba wa Mbingu na Nchi,
Muweza wa yote,Bwana wa Mabwana,
Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Tumsifu,Tumuabudu,Tumuombe,Tumkabidhi mizigo yetu...
Asante Mungu wetu kwa Neema/Rehema hii Baba ya kuiona siku nyingine tena
wengi walitamani kuiona Baba lakini imeshindikana,
 si kwamba si wema au wakosefu sana bali ni kwa Mapenzi yako..
Ukabariki  Kuingia/Kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri,kazi zetu Baba wa mbinguni,Biashara,Masomo na ukatupe sawasawa na mapenzi yako.
Utulinde na kutuokoa katika Shida/Tabu,Ukawafariji wafiwa,Utusamehe Baba wa Mbinguni nasi tupate kuwasamehe waliotukosea,Tunakwenda kinyume na Shetani na Tunakutanguliza/Kuja kwako Mfalme wa Amani..Ukatuongoze katika Maisha yetu.
Ameeeen..!!!!
Mungu yu Macho na  Anasamehe,Anasikia, Omba pasipo  kuchoka.
Mbarikiwe sana.


Mungu anamwita Abramu aiache nchi yake

1Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. 2Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka.
3Anayekubariki, nitambariki;
anayekulaani, nitamlaani.
Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.”
4Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru; na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani. 5Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani, 6Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu, mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo. 7Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea. 8Baadaye Abramu akaondoka, akaelekea mlimani mashariki ya Betheli akapiga hema kati ya mji wa Betheli, upande wa magharibi, na mji wa Ai upande wa mashariki. Hapo pia akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu na kumwomba kwa jina lake. 9Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu.

Abramu nchini Misri

10Wakati huo, njaa ilitokea nchini. Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri kukaa huko kwa muda. 11Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia. 12Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai. 13Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.” 14Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana. 15Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao. 16Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ng'ombe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia.
17Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu. 18Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo? 19Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!” 20Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote.
Mwanzo 12;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 2 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo 11....

Shalom,habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeamka salama na mnaendelea/mmeanza na Mungu.
Mungu aendelee kutulinda,Kutubariki,Kututendea...
Katika Kazi,Biashara,Masomo,
Kwenye vyombo vya usafiri, Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Familia na katika yote
tumtangulize yeye Atoshaye,Ikawe siku njema yenye Amani,Furaha,Upendo,Faraja na shukrani...
Akawaguse wote Wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu Mungu hajawaacha Muite naye Ataitika
Mungu wetu yu mwema sana...!!!!!
Muwe na wakati mwema.


Mnara wa Babeli

1Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale. 2Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa. 3Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. 4Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.”
5Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu. 6Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa. 7Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” 8Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji. 9Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani.

Wazawa wa Shemu

10Wafuatao ni wazawa wa Shemu. Miaka miwili baada ya ile gharika, Shemu akiwa na umri wa miaka 100, alimzaa Arfaksadi. 11Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
12Arfaksadi alipokuwa na umri wa miaka 35, alimzaa Shela. 13Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
14Shela alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Eberi. 15Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
16Eberi alipokuwa na umri wa miaka 34, alimzaa Pelegi. 17Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka 430 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
18Pelegi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Reu. 19Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka 209 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
20Reu alipokuwa na umri wa miaka 32, alimzaa Serugi. 21Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka 207 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
22Serugi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Nahori. 23Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka 200 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
24Nahori alipokuwa na umri wa miaka 29, alimzaa Tera. 25Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka 119, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
26Tera alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Abramu na Nahori na Harani.

Wazawa wa Tera

27Wafuatao ni wazawa wa Tera, baba yao Abramu, Nahori na Harani. Harani alikuwa baba yake Loti. 28Huyo Harani alifariki wakati Tera baba yake alikuwa anaishi huko Uri alikokuwa amezaliwa. 29Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai. Mke wa Nahori aliitwa Milka, binti Harani ambaye pia alikuwa baba yake Iska. 30Sarai hakuwa na mtoto kwa sababu alikuwa tasa.
31Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mjukuu wake aliyekuwa mwanawe Harani, na Sarai mkewe Abramu, wakaondoka wote pamoja toka Uri, mji wa Wakaldayo, wakaenda katika nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakakaa. 32Tera alifariki huko Harani akiwa na umri wa miaka 205.
Mwanzo11;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili" Mbarikiwe sana.

Wednesday, 1 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo 10....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Ni mwezi/Siku mpya tena kwa mapenzi ya Muumba wa vyote ametupa Neema/Rehema ya kuiona tena..
Shukrani na Utukufu daima ni kwake Mungu,
Yeye awezaye yote,Yeye aponyae,
Yeye hutengeneza njia pasipo na njia,Yeye Abarikiae, Yeyeagawae ridhiki,Yeye ni mkuu wa vyote,
Yeye ni mwanzo na Yeye ni mwisho..
Jina lake na Litukuzwe milele na Milele.
Akawabariki wenye Shida/Tabu,Yatima/Wajane,Wagonjwa walio mahospitalini/Majumbani,Wafungwa wasio na Hatia
Waliopatwa na misiba akawe mfariji wao...
Wenye kutafuta watoto baba akawaguse...Wenye kukata tamaa wamgeukie Mungu yeye anaweza,
Tua mizigo uliyonayo Mungu anaponya....
Abariki Kazi zetu,Biashara Watoto wetu/Familia,Wanafunzi Mungu akawaongoze wapate kuelewa na kukumbuka wanayo fundishwa..Muombe kwa Kumaani sha,Kumtukuza na Kumsifu yeye Anatosha.!!!!
Mungu atuongoze vyema..


Wazawa wa Noa

1Baada ya gharika, watoto wa Noa, Shemu, Hamu na Yafethi, walipata watoto wa kiume na wa kike. Hii ndiyo orodha ya wazawa wao:
2Watoto wa kiume wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi. 3Watoto wa kiume wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Rifathi na Togama. 4Watoto wa kiume wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Dodanimu. 5Hawa ndio asili ya watu walioenea sehemu za pwani, kila watu kwa lugha yao, kwa jamaa zao na kufuata mataifa yao.
6Watoto wa kiume wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani. 7Watoto wa kiume wa Kushi walikuwa Seba, Hawila, Sabta, Raama na Sabteka. Watoto wa kiume wa Raama walikuwa Sheba na Dedani. 8Kushi alikuwa baba yake Nimrodi ambaye alikuwa shujaa wa kwanza duniani. 9Alikuwa mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ndiyo maana kuna msemo usemao, “Kama Nimrodi mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.” 10Miji ya kwanza ya utawala wake ilikuwa Babuloni, Ereki na Akadi, katika nchi ya Shinari. 11Kutoka huko, Nimrodi alikwenda Ashuru, akajenga miji ya Ninewi, Rehoboth-iri, Kala na 12Reseni ulioko kati ya Ninewi na mji mkubwa wa Kala.
13Misri alikuwa babu wa Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi, 14Wapathrusi, Wakasluhi (ambao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori.
15Kanaani alikuwa babu yake Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi, 16na pia babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi, 17Wahivi, Waarki, Wasini, 18Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. Baadaye watu wa jamii mbalimbali za Kanaani walitawanyika, 19hata eneo la nchi yao likawa toka Sidoni kuelekea kusini, hadi Gerari mpaka Gaza, na kuelekea mashariki hadi Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu hadi Lasha. 20Hao ndio wazawa wa Hamu kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
21Shemu, mkubwa wa Yafethi, alikuwa baba yao Waebrania wote. 22Watoto wa kiume wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu. 23Watoto wa kiume wa Aramu walikuwa Usi, Huli, Getheri na Mashi. 24Arfaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi. 25Eberi alikuwa na watoto wa kiume wawili; wa kwanza akamwita Pelegi kwa sababu wakati huo watu duniani waligawanyika, na wa pili akamwita Yoktani. 26Yoktani alikuwa baba wa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera, 27Hadoramu, Uzali, Dikla, 28Obali, Abimaeli, Sheba, 29Ofiri, Hawila na Yobabu. Hao wote walikuwa watoto wa Yoktani. 30Nchi walimokaa ilienea toka Mesha mpaka Sefari katika nyanda za juu za mashariki. 31Hao ndio wazawa wa Shemu, kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
32Hao ndio jamaa za watoto wa Noa, kadiri ya vizazi vyao na mataifa yao. Kutokana nao mataifa yote yalienea duniani baada ya gharika.
Mwanzo10;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.