1Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. 2Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. 3Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. 4Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” 5Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Esau anaoa mke wa tatu
6Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani. 7Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu. 8Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani. 9Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.
Ndoto ya Yakobo kule Betheli
10Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani. 11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala. 12Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo. 13Mwenyezi-Mungu alisimama juu ya ngazi hiyo,akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi unayoilalia nitakupa wewe na wazawa wako. 14Wazawa wako watakuwa wengi kama mavumbi ya dunia, na milki yao itaenea kila mahali: Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Kusini. Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa. 15Mimi nipo pamoja nawe; nitakulinda popote uendapo na kukurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapotimiza ahadi niliyokupa.”
16Ndipo Yakobo akaamka usingizini, akasema, “Hakika, Mwenyezi-Mungu yupo mahali hapa, nami sikujua!” 17Yakobo akaogopa na kusema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu na lango la mbinguni.”
18Yakobo akaamka asubuhi na mapema, akachukua lile jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kama nguzo na kuliweka wakfu kwa kulimiminia mafuta. 19Akapaita mahali hapo Betheli; lakini jina la awali la mji huo lilikuwa Luzu. 20Kisha Yakobo akaweka nadhiri akisema, “Iwapo, ee Mungu, utakuwa pamoja nami na kunilinda katika safari yangu, ukinipa chakula na mavazi 21ili nirudi nyumbani kwa baba yangu salama, basi, wewe Mwenyezi-Mungu utakuwa ndiwe Mungu wangu. 22Nalo jiwe hili nililosimika hapa kama nguzo, litakuwa nyumba yako Mungu, nami nitakupa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote utakavyonipa.”
Mwanzo28;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.