Sifa kwa wema wa Mungu
(Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki)
1Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
2Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,
wanyonge wasikie na kufurahi.
3Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,
sote pamoja tulisifu jina lake.
4Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,
na kuniondoa katika hofu zangu zote.
5Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;
nanyi hamtaaibishwa kamwe.
6Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,
na kumwokoa katika taabu zake zote.
7Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,
na kuwaokoa katika hatari.
8 Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.
Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
9Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;
maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.
10Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;
lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
11Njoni enyi vijana mkanisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.
12 Je, watamani kufurahia maisha,
kuishi maisha marefu na kufurahia mema?
13Basi, acha kusema mabaya,
na kuepa kusema uongo.
14Jiepushe na uovu, utende mema;
utafute amani na kuizingatia.
15Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,
na kusikiliza malalamiko yao;
16lakini huwapinga watu watendao maovu,
awafutilie mbali kutoka duniani.
17Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,
na kuwaokoa katika taabu zao zote.
18Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
19Mateso ya mwadilifu ni mengi,
lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.
20 Huvilinda viungo vya mwili wake wote,
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
21Ubaya huwaletea waovu kifo;
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
22Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.