Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 14 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo39....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu wetu Muumba wetu Muumba Mbingu na Nchi,Mungu wa Abrahamu Isaka na Yakobo,Baba yetu,Mwokozi wetu,Yeye asiyechoka,Yeye husamehe,Yeye asiye lala wala kunsinzia,Yeye si binadamu hata aseme uongo...


Siku hiyo mtasema: “Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, maana ingawa ulinikasirikia, hasira yako imetulia, nawe umenifariji. Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.” Mtachota maji kwa furaha kutoka visima vya wokovu. Siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu mwombeni kwa jina lake. Yajulisheni mataifa matendo yake, tangazeni kuwa jina lake limetukuka. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa kwa kuwa ametenda mambo makuu; haya na yajulikane duniani kote. Pazeni sauti na kuimba kwa furaha, enyi wakazi wa Siyoni, maana aliye mkuu miongoni mwenu ndiye Mungu, Mtakatifu wa Israeli.”

Asante Baba wa Mbinguni kwa kibali ulichotupa na kutuchagua tena kuiona siku hii,Si kwamba sisi ni wema sana ,Si kwamba wajuaji na wenye nguvu,Sikwamba sisi ni bora sana kuliko wengine,Ni kwa Neema/Rehema zako tuu Baba wa mbingu...
Tunaomba ukatulinde,ukatubariki katika kazi,Biashara,Masomo,Hatua zetu zikawe nawe Baba wa Mbinguni,Kuingiakwetu/Kutokakwetu,Vyombo vya Usafri,TutembeapoVilaji/Vinywaji..
Ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/Kutumia... na  ukatutakase Miili yetu/Akilizetu ..
Roho MtakatifuKu akatuongoze kwenye kunena/kutenda..
Ukatutumie na kutupa sawasawa na mapenzi yako...
 Mfalme wa Amani..
Ukawaponye/Kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo vya mwovu,Wagonjwa,Wafiwa wakawe mfariji wao,Wajane na Yatima Baba ukawabariki,Wenye shida/Tabu Baba ukawanyooshee mkono wako na kuwagusa

Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu![2Wakorintho 6:2]

Tunarudisha Sifa na Utukufu ni kwako Mungu wetu,Tunajiachilia mikononi mwako, Tukishukuru na Kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu...
Amina...!!!!



Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.[Waebrania 13:21]

Mke wa Potifa na Yosefu

1Basi, Yosefu alipochukuliwa mpaka Misri, Mmisri mmoja aitwaye Potifa ambaye alikuwa ofisa wa Farao na mkuu wa kikosi chake cha ulinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri. 2Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri. 3Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu. 4Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote. 5Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani. 6Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe.
Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza. 7Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”. 8Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena. 9Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.” 10Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe.
11Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani. 12Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje. 13Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje, 14akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!”
16Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani. 17Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha. 18Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.” 19Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira, 20akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme. 21Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza. 22Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake. 23Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya.
Mwanzo39;1-23

Bible Society of Tanzania"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 13 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo38....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Kutupa Nafasi na Kibali cha kuiona siku/wiki hii..
Tumsifu na Kumtukuza yeye Daima..

Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake. Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu! Umsifu Mungu wako, ee Siyoni! Maana yeye huimarisha milango yako, huwabariki watu waliomo ndani yako. Huweka amani mipakani mwako; hukushibisha kwa ngano safi kabisa. Yeye hupeleka amri yake duniani, na neno lake hufikia lengo lake haraka. Hutandaza theluji kama pamba, hutawanya umande kama majivu. Huleta mvua ya mawe kama kokoto na kwa ubaridi wake maji huganda. Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka; huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka. Humjulisha Yakobo ujumbe wake, na Israeli masharti na maagizo yake. Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine; watu wengine hawayajui maagizo yake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Asante Baba kwa wema na Fadhili zako,Ukaibariki siku/wiki hii na ukatubariki katika kazi zetu,Biashara,Masomo,Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Hatuaze ziwe nawe ee Mungu Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,
Ukatutakase akili zetu Miili yetu,Utusamehe tulipo kwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni..Nasi tunaomba tuwezeshe kuwasamehe waliotukosea..
Utubariki na kutufanya  chombo chako tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki kipato chetu kiingiacho na kitokacho Baba ukakiguse na kupata kibali chako katika matumizi yetu..
Tunarudisha shukrani kwako ee Mungu wetu,Sifa na Utukufu ni kwako..
Tuanajiachilia mikononi mwako Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu
Amina...!!!!!!
Muwe na Wakati mwema..Tuanze na Mungu.


Yuda na Tamari

1Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira. 2Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa. 3Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri. 4Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani. 5Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu.
6Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari. 7Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua. 8Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.” 9Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto. 10Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia. 11Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake.
12Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake. 13Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake, 14alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe.
15Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso. 16Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?” 17Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.” 18Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake. 19Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane.
20Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata. 21Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.” 22Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.” 23Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.”
24Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!” 25Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.” 26Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari.
27Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha. 28Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.” 29Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi. 30Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera.
Mwanzo38;1-30

Bible Society of Tanzania
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday, 12 March 2017

Natumaini Jumapili inaendelea Vyema;"Wanawake ni Nguvu ya Jamii",[Hongera Wanawake]Burudani kwa Mwanamke,Emmy Kosgei_Mama,TAAI (we are moving forward )

Wapendwa /Waungwana Ni matumaini yangu jumapili inaendelea vyema,pia Wanawake mlisheherekea/Manaendelea kusheherekea Vyema siku Yenu..Pia naamini Wanaume mlikuwa/mko sambamba kuungana na Wanawake kwenye siku yao..
Mwanamke ni nani kwako wewe Mwanaume?
Jee wewe Mwanamke unajitambua na kujivunia kuwa Mwanamke?
Nini kikubwa hutakisahau chema/kibaya ulichokifanya kama Mwanamke ulipaswa kukifanya/kutokifanya?
Mungu aendelee kuwabariki na kuwaongoza katika majukumu yenu kama Wanawake.
Neno La Leo;Esta 2;1-23

Esta anateuliwa kuwa malkia

1Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. 2Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? 3Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. 4Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo.
5Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. 6Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni.
7Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake.
8Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. 9Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie.
10Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. 11Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
12Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero. 13Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu. 14Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.
15Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye. 16Basi, Esta alipelekwa ikulu kwa mfalme katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Ahasuero, mwezi wa kumi uitwao Tebethi. 17Mfalme alipendezwa zaidi na Esta kuliko alivyopendezwa na wanawake wengine wote. Alipendwa sana kuliko wasichana wengine. Basi, mfalme akamvika taji ya kimalkia kichwani, akamfanya malkia badala ya Vashti. 18Kisha mfalme akaandaa karamu kubwa kwa heshima ya Esta, akawaalika viongozi na watumishi wote wa serikali yake. Pia, mfalme alitangaza msamaha wa kodi katika mikoa yote, akatoa zawadi nyingi kulingana na hadhi yake ya kifalme.










Mordekai aokoa maisha ya mfalme

19Wasichana walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi penye lango la mfalme. 20Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye.
21Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. 22Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. 23Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Friday, 10 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo37....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu Kwa siku hii..

Mungu Mtawala Mkuu
Mwenyezi-Mungu anatawala, mataifa yanatetemeka! Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa, nayo dunia inatikisika! Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni; ametukuka juu ya mataifa yote. Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha. Mtakatifu ndiye yeye! Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu! Umethibitisha haki katika Israeli; umeleta uadilifu na haki. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; angukeni kifudifudi mbele zake. Mtakatifu ndiye yeye! Mose na Aroni walikuwa makuhani wake; Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia. Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza. Alisema nao katika mnara wa wingu; waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza; kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao. Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; abuduni katika mlima wake mtakatifu! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.[Zaburi 99:1-9]

Asante Baba wa Mbingu kwa kutuamsha salama na kutupa kibali chako cha kuendelea kuiona leo hii,Sifa na Utukufu ni kwako Baba yetu,Mungu wetu, Mungu wa Ibrahimu,Isaka na Yakobo..Muweza wa yote,Tunaomba Baba ukaibariki siku hii ikawe Njema, Yenye Furaha,Amani,Mafanikio na Kukupendeza wewe..Ukatulinde na kutuongoza kwenye Kazi,Biashara,Masomo,Hatua zetu ziwe nawe,Tuingiapo/Tutokapo,Vyombo vya usafiri na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase...
RohoMtakatifu ukatuongoze kwenye Kunena/Kutenda,Kuamua,kutambua/kujitambua...

Baba ukawaguse/kuwaokoa wote wanaopitia magumu/majaribu,shida/tabu,vifungo vya mwovu..wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao...
 11Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye. 12Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13Mtanitafuta na kunipata. Mtakaponitafuta kwa moyo wote 14mtanipata. Nami nitawarudishieni fanaka zenu na kuwakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipowafukuzia. Nitawarudisheni mahali ambapo niliwatoa, nikawapeleka uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.[Yeremia29;11-14]


Tunasifu na Kushukuru, Tukiamani wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina...!!
Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.Shukrani kwa Mungu.[2Wakorintho 1:2]





Yosefu na ndugu zake

1Yakobo aliendelea kukaa katika nchi ya Kanaani, alimoishi baba yake kama mgeni. 2Hizi ndizo habari za ukoo wa Yakobo.
Yosefu, akiwa kijana wa umri wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, wana wa Bilha na Zilpa, wake za baba yake. Yosefu akawa anamjulisha baba yake juu ya tabia mbaya za ndugu zake.
3Israeli alimpenda Yosefu kuliko watoto wake wote kwa sababu alikuwa amezaliwa wakati wa uzee wake. Alimshonea Yosefu kanzu ndefu. 4Lakini ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda Yosefu kuliko wao, wakamchukia hata hawakuzungumza naye kwa amani.

Ndoto za Yosefu

5Usiku mmoja, Yosefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia. 6Aliwaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7Niliota kuwa sote tulikuwa shambani tukifunga miganda na ghafla mganda wangu ukainuka na kusimama wima. Miganda yenu ikakusanyika kuuzunguka na kuuinamia mganda wangu.” 8Ndugu zake wakamwuliza, “Je, unataka kutuambia kwamba utatutawala? Au utakuwa na mamlaka juu yetu?” Basi, wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto na maneno yake.
9Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.” 10Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?” 11Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo.

Yosefu anauzwa

12Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu. 13Basi, Israeli akamwambia Yosefu, “Unajua ndugu zako wanachunga wanyama kule Shekemu. Kwa hiyo nataka nikutume kwao.” Yosefu akajibu, “Niko tayari.” 14Baba yake akamwambia, “Nenda ukawaangalie ndugu zako na wanyama kama wako salama, kisha uniletee habari.” Basi, Yakobo akamtuma Yosefu kutoka bonde la Hebroni. Yosefu alipokaribia Shekemu 15mtu mmoja akamkuta akitangatanga mbugani, akamwuliza, “Unatafuta nini?” 16Yosefu akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali, niambie mahali wanakochunga wanyama.” 17Yule mtu akamwambia, “Bila shaka wamekwisha ondoka, kwa sababu niliwasikia wakisema kwamba wanakwenda Dothani.” Basi, Yosefu akawafuata ndugu zake, akawakuta huko Dothani. 18Ndugu zake walipomwona akiwa mbali na kabla hajafika karibu, wakafanya mpango wa kumuua. 19Waliambiana, “Tazameni! Yule mwota ndoto anakuja. 20Haya, tumuue na kumtupa ndani ya shimo mojawapo. Baadaye tutasema kwamba ameuawa na mnyama wa porini. Halafu tutaona hizo ndoto zake zitakuwaje.” 21Lakini Reubeni aliposikia maneno hayo, akataka kumwokoa mikononi mwao; basi akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, tusimuue. 22Msimwage damu. Ila mtumbukizeni katika shimo hili hapa mbugani, lakini msimdhuru.” Alisema hivyo kusudi aweze kumwokoa Yosefu mikononi mwao, na baadaye amrudishe kwa baba yake. 23Yosefu alipowafikia ndugu zake, wao wakamvua kanzu yake. 24Kisha wakamshika na kumtupa shimoni. Lakini shimo hilo halikuwa na maji.
25Walipoketi kula, wakaona msafara wa Waishmaeli wakisafiri kutoka Gileadi kwenda Misri. Ngamia wao walikuwa wamebeba ubani, zeri na manemane. 26Hapo Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutapata faida gani tukimuua ndugu yetu na kuficha mauaji yake? 27Afadhali tumwuze kwa hawa Waishmaeli, lakini tusiguse maisha yake, kwani yeye ni ndugu yetu; yeye ni damu moja nasi.” Ndugu zake wakakubaliana naye. 28Wafanyabiashara Wamidiani walipofika mahali hapo, hao ndugu wakamtoa Yosefu katika shimo, wakamwuza kwa Waishmaeli kwa bei ya vipande ishirini vya fedha; nao wakamchukua Yosefu hadi Misri.
29Basi, Reubeni aliporudi kwenye lile shimo, na asimwone Yosefu tena, akazirarua nguo zake kwa huzuni, 30akawaendea ndugu zake, akawaambia, “Kijana hayupo nami niende wapi?” 31Basi, wakachinja mbuzi, wakaichukua kanzu ya Yosefu na kuichovya katika damu ya huyo mbuzi. 32Kisha wakampelekea baba yao ile kanzu, wakamwambia, “Tumeiokota kanzu hii. Hebu iangalie kama ni ya mwanao, au siyo.” 33Baba yao akaitambua hiyo kanzu, akasema, “Ndiyo hasa! Bila shaka mnyama wa porini amemshambulia na kumla. Hakika Yosefu ameraruliwa vipandevipande.” 34Hapo Yakobo akayararua mavazi yake kwa huzuni, akavaa vazi la gunia kiunoni. Akamlilia mwanawe kwa muda wa siku nyingi. 35Watoto wake wa kiume na wa kike wakamjia ili kumfariji, lakini akakataa kufarijiwa, akisema, “Niacheni; nitaendelea kuomboleza kwa ajili ya mwanangu, mpaka nitakaposhuka kuzimu alipo.” Ndivyo baba yake alivyomlilia.
36Wakati huo, kule Misri, wale Wamidiani walimwuza Yosefu kwa mtu aitwaye Potifa, mmoja wa maofisa wa Farao, ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi.
Mwanzo37:1-36

Bible Society of Tanzania

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 9 March 2017

Maandalizi Ya TANZANIA DAY 2017 Dallas Texas






Aprili 29, 2016, Mstahiki Meya wa jiji la Dallas, jimbo la Texas aliitangaza rasmi siku hiyo kuwa SIKU YA TANZANIA

Na mwaka huu, Jumuiya ya waTanzania waishio jimboni humo kwa kushirikiana na Baraza la waTanzania waishio nchini Marekani (Diaspora Council of Tanzanians in America) wanaandaa maadhimisho makubwa ya siku hiyo yatakayofanyika katika jiji la Dallas.

Viongozi Ben Kazora wa Jumuiya ya Dallas na Charles Bishota wa DICOTA wamezungumza na Mubelwa Bandio kuhusu maandalizi ya siku hiyo

KARIBU USIKILIZE


Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo36....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunasema Asante Mungu wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi,Mungu wa Isaka na Yakobo,Baba waYatima,Mume wa Wajane,Mfalme wa Amani,Umetulinda usiku na Umetuchagua tena ,Umetupa kibali cha Kuiona Leo hii Baba tukiwa wenye Afya...Si kwa uwezo wetu Baba wa Mbinguni wala nguvuzetu..Ni kwa Neema/Rehema zako Muumba wetu..
Tunaomba utusamehe pale tulipo kwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni,

Ombeni toba kwake, mrudieni na kumwambia: “Utusamehe uovu wote, upokee zawadi zetu, nasi tutakusifu kwa moyo.[Hosea 12:2]
Tunajikabidhi mikononi mwako Baba wa Mbinguni na ukatuongoze katika
Siku hii Baba ,Jana imepita Baba Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine,Usituache ee Mwokozi wetu..Roho Mtakatifu utuongoze kwenye kutenda/kunena, na tukawe barua njema,Baba Ukatubariki katika kazi zetu,Biashara,Masomo,Tuingiapo/Tutokapo,Vyombo vya usafiri na hatua zetu ziwe nawe,Vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba wa Mbinguni ukavitakase....

Mfalme wa Amani utawale katika maisha yetu na uibariki Nchi hii na mji huu tunaoishi,Bariki Tanzania,Afrika na Dunia yote ukatawale ee Mwokozi,Ukawaongoze na kuwagusa wanaotuongoza nao wakatuongoze katika haki na kweli..
Baba ukawaguse na kuwaponya wote wanaopitia magumu/majaribu,walio na vifungo mbali mbali vya  mwovu,Wagonjwa,Wafiwa ukawe mfariji wao..wenye shida/tabu baba ukaonekane...

Utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utukusanye pamoja kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, na kuona fahari juu ya sifa zako.[Zaburi 106:47]
Tunarudisha Sifa na Shukrani kwako Muumba wetu
Asante kwa yote,Tunajiachilia mikononi mwako Baba tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote tangu sasa na hata milele.[Zaburi 121:8]
Amina...!!!!



Wazawa wa Esau

(1Nya 1:34-37)

1Wafuatao ni wazawa wa Esau (yaani Edomu). 2Esau alioa wake Wakanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi, 3na Basemathi, binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi. 4Ada alimzalia Esau Elifazi, naye Basemathi akamzalia Reueli. 5Oholibama alimzalia Yeushi, Yalamu na Kora. Hao ndio watoto wa kiume wa Esau ambao wake zake walimzalia alipokaa katika nchi ya Kanaani.
6Kisha, Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, watu wote wa nyumbani mwake, ng'ombe wake, wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata katika nchi ya Kanaani, akahamia mahali pengine, mbali na nduguye Yakobo. 7Alifanya hivyo kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi hata wasiweze kuishi pamoja. Nchi waliyokaa kama wageni haikuweza kuwatosha kwa sababu ya wingi wa mifugo yao. 8Kwa hiyo, Esau akaenda kukaa katika nchi ya milima ya Seiri. Jina lingine la Esau ni Edomu.
9Wafuatao ni wazawa wa Esau, baba ya Waedomu katika nchi ya milima ya Seiri. 10Watoto wa kiume wa Esau walikuwa Elifazi aliyezaliwa na Ada mkewe, na Reueli aliyezaliwa na Basemathi mke wake mwingine. 11Watoto wa kiume wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi. 12Elifazi alikuwa na suria jina lake Timna. Huyu alimzalia mwana, jina lake Amaleki. 13Basemathi, mkewe Esau, alimzaa Reueli. Watoto wa kiume wa Reueli walikuwa Nahathi, Zera, Shama na Miza. 14Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, alimzalia Esau mumewe watoto wa kiume watatu: Yeushi, Yalamu na Kora.
15Wafuatao ni wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau. Elifazi, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Esau aliwazaa Temani, Omari, Sefo, Kenazi, 16Kora, Gatamu na Amaleki, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Elifazi katika nchi ya Edomu, waliotokana na Ada, mkewe Esau. 17Reueli, mwanawe Esau, aliwazaa Nahathi, Zera, Shama na Miza, kila mmoja wao akawa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Reueli katika nchi ya Edomu, waliotokana na Basemathi, mkewe Esau. 18Watoto wa kiume wa Oholibama, mkewe Esau, walikuwa Yeushi, Yalamu na Kora, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake. Hao wote ni watoto wa kiume wa Oholibama, binti Ana, mkewe Esau. 19Basi, hao ndio wazawa wa Esau yaani Edomu, kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake.

Wazawa wa Seiri

(1Nya 1:38-42)

20Wafuatao ni wazawa wa Seiri, Mhori, na ndio wenyeji wa nchi hiyo: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, 21Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake miongoni mwa Wahori wa uzawa wa Seiri, katika nchi ya Edomu.
22Watoto wa kiume wa Lotani walikuwa Hori na Hemani; na dada yake Lotani aliitwa Timna. 23Watoto wa kiume wa Shobali walikuwa Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu. 24Watoto wa kiume wa Sibeoni walikuwa Aya na Ana. Ana ndiye aliyeziona chemchemi za maji ya moto jangwani, alipokuwa anawachunga punda wa baba yake Sibeoni. 25Watoto wa Ana walikuwa Dishoni na dada yake mmoja aitwaye Oholibama. 26Watoto wa kiume wa Dishoni walikuwa Hemdani,Eshbani, Ithrani na Kerani. 27Watoto wa kiume wa Eseri walikuwa Bilhani Zaawani na Akani. 28Watoto wa kiume wa Dishani walikuwa Usi na Arani.
29Basi, hao ndio wakuu wa Wahori: Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, 30Dishoni, Eseri na Dishani; kila mmoja wao akiwa mkuu wa kabila lake katika nchi ya Seiri.

Wafalme wa nchi ya Edomu

(1Nya 1:43-45)

31Wafuatao ni wafalme waliotawala nchi ya Edomu, kabla mfalme yeyote hajawatawala Waisraeli: 32Bela mwana wa Beori alitawala nchi ya Edomu akiwa na makao yake makuu katika mji wa Dinhaba. 33Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra alitawala badala yake. 34Yobabu alipofariki, Hushamu wa nchi ya Watemani, alitawala badala yake. 35Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi alitawala badala yake, makao yake makuu yakiwa katika mji wa Avithi. Huyu ndiye aliyewapiga na kuwashinda Wamidiani katika nchi ya Moabu. 36Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka, alitawala badala yake. 37Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi, ulio karibu na mto Eufrate, alitawala badala yake. 38Shauli alipofariki, Baal-hanani, mwana wa Akbori, alitawala badala yake. 39Baal-hanani, mwana wa Akbori alipofariki, Hadadi alitawala badala yake, na jina la mji wake likiwa Pau. Mkewe Akbori alikuwa Mehetabeli, binti Matredi na mjukuu wa Mezahabu.
40Wakuu wa makabila yaliyotokana na Esau, kadiri ya makabila yao na makazi yao walikuwa: Timna, Alva, Yethethi, 41Oholibama, Ela, Pinoni, 42Kenazi, Temani, Mibsari, 43Magdieli na Iramu. Hao ndio wakuu wa makabila yaliyotokana na Edomu, yaani Esau, baba yake Edomu; wametajwa kulingana na makazi yao katika sehemu za nchi walizomiliki.
Mwanzo 34;1-43
Bible Society of Tanzania

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday, 8 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo35....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mtakatifu Mtakatifu Baba wa Mbinguni, Muumba Mbingu na Nchi, Muumba wetu, Muweza wa yote,Mungu wetu na Baba Yetu,Mwokozi na Mponyaji wetu..Tunasema asante Baba kwa kibali chako ulichotupa cha kuendelea kuiona siku hii..Shukrani na utufu ni kwako Baba, Mfalme wa Amani ukatawale siku hii na maisha yetu yawe juu yako,Ukatuongoze tuingiapo/Tutokapo,Hatua zetu ziwe nawe,Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba ukavitakase na damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu..
Ukatusamehe pale tulipoenda kinyume nawe Baba..
Nasi ukatupe kuweza kuwasamehe waliotukosea...
Ukatupe sawasawa na mapenzi yako...
Tukatumike kama chombo chako na kutuongoza katika Kunena/kutenda..

Wema wako ,Fadhili zako, Upendo na Neema/Rehema zisipungue..
Kwakuwa Ufalme ni Wako,Nguvu na Utukufu ni wako Baba..

Wema wa Mungu
5Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni;
uaminifu wako wafika mawinguni.
6Uadilifu wako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama
7Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako!
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
8Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;
wawanywesha kutoka mto wa wema wako.
9Wewe ndiwe asili ya uhai;
kwa mwanga wako twaona mwanga.
10Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua;
uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.
11Usikubali wenye majivuno wanivamie,
wala watu waovu wanikimbize.
12Kumbe watendao maovu wameanguka;
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.
                   [Zaburi 36:5-12]
Tunashukuru na kukusifu..Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa mbinguni, Tukishukuru na kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina....!!!!

Yakobo anahamia Betheli

1Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.” 2Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu. 3Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.” 4Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
5Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia. 6Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao. 7Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake. 8Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi.
9Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. 10Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli. 11Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme. 12Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.” 13Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu. 14Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta. 15Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli.

Kuzaliwa kwa Benyamini na kifo cha Raheli

16Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa. 17Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.” 18Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini. 19Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu). 20Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo. 21Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi.
22Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo.

Wana wa Yakobo

(1Nya 2:1-2)

Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili. 23Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni. 24Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini. 25Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali. 26Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu.

Kifo cha Isaka

27Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni. 28Isaka alikuwa na miaka 180 29akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika.
Mwanzo35;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.