Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 17 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo42....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Imani na kweli,Yeye aliyetupa kibali cha kuiona leo hii,Mungu wetu yu mwema sana,Yeye aliyetuchagua kwa Mapenzi yake na si kwa wema na nguvu zetu..Kwa Neema/Rehema yeye ametupa pumzi na kuweza kusimama tena..Yeye ni Mwanzo na yeye ni mwisho..

Fadhili zake,Upendo watoka kwake,Furaha na Amani zapatikana kwawe..
Tukiamini na kufuata njia zake kamwe hatutapotea..Eee Mungu utuongoze katika njia zako..

Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.” Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ngoka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.
Utubariki na kutulinda katika Kazi zetu,Biashara,Masomo..Tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri,Hatua zetu ziwe nawe Mfalme wa Amani,Ukatutakase miili yetu na akaili zetu,Ukavitakase vyote tunavyoenda kugusa/kutumia na Damu ya mwana wako Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo..
Utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Baba nasi utupe neema ya kuweza kusameheana..
Ukawaguse na kuwaponya Wagonjwa,wanaopitia magumu/mapito,wenye Shida/Tabu na wote walio Magerezani pasipo na hatia...walifungwa kwa minyororo ya mwovu Baba ukawafungue na kuwaweka huru Kiroho na kimwili..
Roho Mtakafu akatuongoze kwenye kunena/kutenda, ukatufanye chombo chema na ukatutumie sawa sawa na mapenzi yako..


Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni,Tunashukuru na Kukusifu,Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina...!!
Mungu awabariki.


Ndugu za Yosefu wanakwenda Misri

1Yakobo alipopata habari kwamba kulikuwa na nafaka huko Misri, aliwaambia wanawe, “Mbona mnaketi mkitazamana tu? 2Nimesikia kwamba Misri kuna nafaka. Nendeni huko mkanunue nafaka tusije tukafa njaa.” 3Hivyo ndugu kumi wa Yosefu wakaenda Misri kununua nafaka. 4Lakini Yakobo hakumwacha Benyamini, nduguye Yosefu, aende pamoja nao maana aliogopa kwamba angeweza kupata madhara. 5Basi, wana wa Israeli wakafika Misri wakiwa miongoni mwa wanunuzi wengine, kwani hata katika nchi ya Kanaani kulikuwa na njaa.
6Wakati huo Yosefu alikuwa ndiye mkuu huko Misri. Yeye ndiye aliyehusika na kuwauzia wananchi nafaka. Basi, kaka zake wakaja na kumwinamia Yosefu kwa heshima. 7Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.” 8Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua. 9Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.” 10Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula. 11Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.” 12Lakini Yosefu akasisitiza, “Sivyo! Mmekuja hapa ili kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.” 13Wakamwambia, “Sisi, watumishi wako, tuko ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja, mwenyeji wa nchi ya Kanaani. Mdogo wetu amebaki na baba nyumbani, na ndugu yetu mwingine ni marehemu.” 14Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu. 15Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja. 16Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.” 17Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu.
18Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi: 19Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa. 20Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo. 21Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.” 22Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.” 23Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani. 24Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao.

Ndugu za Yosefu wanarudi nyumbani

25Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote. 26Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka. 27Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake. 28Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”
29Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia, 30“Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake. 31Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi. 32Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu. 33Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa. 34Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’”
35Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu. 36Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!”
37Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.” 38Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.”
Mwanzo42;1-38
Bible Society of Tanzania"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 16 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo41....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake..

Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu. Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku, kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze. Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda. Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno! Mawazo yako ni mazito mno!
Mtakatifu Matakatifu Baba wa Mbinguni, Tunashukuru na kukusifu daima..Asante kwa kibali ulichotupa Baba cha kuiona siku  hii..
Tunaomba ukatubariki katika Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri,tutembeapo Baba hatua zetu ziwe nawe..Ukabariki Vilaji/Vinywaji na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba wa Mbinguni ukavitakase na Damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo...
Roho Mtakati akatuongoze katika yote..
Tunakwenda kinyume na mwovu ,Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni Utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..
Tupate kiu ya kujua na kujifunza zaidi juu ya Fadhili na wema wako..


Uwaponye na kuwaokoa wote wanaoteseka kwa Magonjwa,Shida/Tabu na vifungo vya mwovu..
Baba Mungu utawale maisha yetu na utupe sawa sawa na mapenzi yako..
Tunayaweka haya mikononi mwako na tukiomba na kushukuru...
Tukiamini wewe ni Bwana wa Majeshi,Mlinzi mkuu,Bwana na Mwokozi wetu..
Amina...!!!!



Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina![Waroma 15:33]


Yosefu mbele ya Farao

1Baada ya miaka miwili mizima, Farao aliota ndoto: Alijikuta amesimama kando ya mto Nili, 2akaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. 3Halafu, baada ya hao, ng'ombe wengine saba waliokonda sana wakatoka katika mto Nili, wakaja na kusimama karibu na wale ng'ombe wazuri na wanono, kando ya mto. 4Hao ng'ombe waliokonda sana wakawala wale wengine saba wazuri na wanono. Hapo Farao akaamka usingizini. 5Alipolala tena, akaota mara ya pili. Aliona masuke saba makubwa na mazuri yanachipuka katika bua moja. 6Halafu, baada ya hayo, masuke mengine saba membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani yakatokeza. 7Hayo masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba makubwa yaliyojaa nafaka. Basi, Farao alipoamka akagundua kuwa ilikuwa ndoto. 8Kulipokuwa asubuhi, Farao akiwa na wasiwasi sana, aliwaita wachawi wote wa Misri, na wenye hekima, akawaambia ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumtafsiria ndoto hizo.
9Ndipo, yule mtunza vinywaji mkuu akamwambia Farao, “Leo nayakumbuka makosa yangu! 10Wakati ule ulipotukasirikia sisi watumishi wako, mimi na mwoka mikate mkuu, ulitufungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi. 11Usiku mmoja tuliota ndoto, kila mmoja ndoto yake tofauti. 12Basi, kijana mmoja Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi, alikuwa pamoja nasi kifungoni. Tulipomsimulia ndoto zetu, yeye aliweza kututafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake. 13Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.”
14Basi, Farao akaamuru Yosefu aitwe; naye akatolewa gerezani haraka. Baada ya kunyoa na kubadili nguo zake, Yosefu akaja mbele ya Farao. 15Farao akamwambia Yosefu, “Mimi nimeota ndoto, lakini hakuna mtu aliyeweza kunitafsiria. Nimesikia sifa zako kwamba wewe ukiambiwa ndoto unaweza kuitafsiri.” 16Yosefu akamjibu Farao, “Sina uwezo huo; lakini Mungu atakupa jibu lifaalo.” 17Hapo Farao akamwambia Yosefu, “Niliota kwamba nimesimama kando ya mto Nili, 18nikaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. 19Hao wakafuatwa na ng'ombe wengine saba dhaifu, wembamba na wamekonda sana. Mimi sijapata kamwe kuona ng'ombe wa hali hiyo katika nchi ya Misri. 20Basi, wale ng'ombe waliokonda sana wakawala wale ng'ombe saba wanono. 21Lakini hata baada ya kuwala wale wanono, mtu yeyote asingeweza kutambua kwamba wamewala wenzao, kwani bado walikuwa wamekondeana kama mwanzo. Hapo nikaamka usingizini. 22Kisha nikaota ndoto nyingine: Niliona masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka yakichipua katika bua moja. 23Halafu yakafuatwa na masuke mengine saba matupu, membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani. 24Yale masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba mazuri. Basi, mimi niliwaambia wachawi ndoto hizo lakini hakuna mtu aliyeweza kunifafanulia.”
25Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto zako zote mbili tafsiri yake ni moja. Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. 26Ngombe wale saba wazuri ni miaka saba, na yale masuke saba mazuri pia ni miaka saba; ndoto hiyo tafsiri yake ni moja. 27Wale ng'ombe saba waliokonda sana, ambao waliwafuata wale wanono, na yale masuke matupu saba, yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani, maana yake ni miaka saba ya njaa. 28Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni. 29Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri. 30Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii. 31Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. 32Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni.
33“Kwa hiyo yafaa sasa, ee Farao, umteue mtu mwenye ujuzi na hekima, umpe jukumu la kuiangalia nchi yote ya Misri. 34Tena, ee Farao, uwateue wasimamizi kadhaa hapa nchini, uwaagize wakusanye sehemu ya tano ya mavuno yote ya Misri katika kipindi hiki cha miaka saba ya shibe. 35Uwaagize wasimamizi hao wakusanye chakula chote katika miaka saba ijayo ya mavuno kwa wingi. Nafaka hiyo na iwekwe chini ya mamlaka yako, ee Farao, iwe akiba ya chakula kwa miji yote, nao waitunze nafaka hiyo. 36Chakula hicho kitakuwa akiba ya kinga kwa nchi ya Misri isije ikaangamia kutokana na njaa ya miaka saba itakayofuata.”

Yosefu apewa cheo

37Shauri alilotoa Yosefu lilionekana kuwa jema mbele ya Farao na watumishi wake wote. 38Kwa hiyo Farao akawauliza watumishi wake, “Huyu mtu ana roho ya Mungu! Je, tunaweza kumpata mtu mwingine kama huyu?” 39Kisha akamwambia Yosefu, “Kwa kuwa Mungu amekufunulia haya yote, hakuna mtu mwingine mwenye busara na hekima kama wewe. 40Wewe ndiwe utakayeisimamia nchi yangu, na watu wangu wote watakuwa chini ya amri yako. Mimi tu ndiye mkuu kuliko wewe kwa kuwa nakalia kiti cha kifalme. 41Basi, sasa nakuteua rasmi kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri!” 42Ndipo, Farao akaivua pete yake ya mhuri kidoleni mwake na kumvisha Yosefu, akamvalisha na mavazi ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni. 43Farao akampandisha katika gari lake la pili la farasi na walinzi wakatangulia mbele ya Yosefu wakipaza sauti na kusema, “Pigeni magoti!” Ndivyo Farao alivyompa Yosefu madaraka makubwa juu ya nchi yote ya Misri. 44Zaidi ya hayo, Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ndimi Farao! Nasema: Mtu yeyote katika nchi nzima ya Misri asiinue mkono wala mguu wake bila kibali chako.” 45Farao akampa Yosefu jina la Kimisri: Safenath-panea. Akamwoza Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Basi, Yosefu akaanza kuitembelea nchi nzima ya Misri.
46Yosefu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kumtumikia Farao, mfalme wa Misri. Alitoka nyumbani kwa Farao na kuitembelea nchi yote ya Misri. 47Ikawa, katika miaka ile saba ya shibe, mashamba ya Misri yakatoa mazao kwa wingi sana. 48Yosefu akakusanya chakula chote wakati huo wa miaka saba ya shibe na kukiweka akiba katika miji ya Misri. Katika kila mji akaweka akiba ya chakula kutoka mashamba yaliyo karibu na mji huo. 49Yosefu akaweka akiba ya nafaka kwa wingi mno ikawa nyingi kama mchanga wa bahari, hata isiweze kupimika.
50Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Yosefu alikuwa amekwisha pata wana wawili kwa mkewe, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. 51Yosefu alimwita mwanawe wa kwanza Manase, akisema, “Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote na jamaa ya baba yangu.” 52Mwanawe wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Mungu amenipa watoto katika nchi ya mateso yangu.”
53Miaka ile saba ya shibe nchini Misri ikapita. 54Ikaanza miaka saba ya njaa kama alivyokuwa amesema Yosefu hapo awali. Nchi nyingine zote zikawa na njaa, lakini nchi yote ya Misri ilikuwa na chakula. 55Wakati wananchi wa Misri walipoanza kuona njaa, walimlilia Farao awape chakula. Naye Farao akawaambia Wamisri wote, “Nendeni kwa Yosefu; atakalowaambia fanyeni.” 56Njaa ikazidi kuwa kali na kuenea katika nchi yote. Kwa hiyo Yosefu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri chakula. 57Zaidi ya hayo, watu toka kila mahali duniani walikuja Misri kwa Yosefu kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa kali duniani kote.
Mwanzo41;1-57

Bible Society of Tanzania
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday, 15 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo40....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu mkuu kwa Matendo yake makuu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi,Muweza wa yote,Hakuna wa kufanana naye,Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Hakuna lisilowezekana mbele zake Mungu..Yeye ndiye aliyetupa kibali cha kuiona leo hii..Yeye ndiye alituchagua tena..Tumsifu Mungu wetu na kumtukuza daima..Yeye anatujua zaidi tunavyojijua..shukrani na utukufu ni kwake Muumba wetu..
Tazama Jana imepita Mungu wetu,Leo ni siku mpya,Kesho ni siku nyingine Baba Mungu..Utubariki tuingiapo/tutokapo,hatua zetu ziwe na we Baba wa Mbinguni,Ubariki kazi zetu Baba..Biashara,Masomo,Vilaji/Vinywaji,Vyombo vya usafiri na tutembeapo...Ukavitakase vyote tunavyoenda kuvitumia/kugusa Mfalme wa Amani..Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/Kutenda,Ukatufanye chombo chema na ukatutumie sawasawa na mapenzi yako..Ukabariki Ridhiki zetu Baba wa mbinguni..kinachoingia na kutoka...
Utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mwokozi..
Utupe Neema ya kuweza kusameheana Baba wa mbinguni..

Baba Mungu ukaibariki Nchi hii tunayoishi,Ukabariki pia Tanzania,Afrika na Dunia yote Mfalme wa Amani ukatawale..Ukawaongoze wanaotuongoza na wakatuongoze katika haki na kweli..

Baba ukawaponye na kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu zozote..Ukawafungue waliokwenye vifungo vya mwovu.. wapate kupona kiroho na kimwili Baba..
Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa Mbingu Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu.. Amina..!!!!

Muwe na Wakati mwema.


Yosefu anatafsiri ndoto

1Wakati fulani baada ya mambo hayo, maofisa wawili wa mfalme wa Misri walimkosea mfalme. Maofisa hao walikuwa mtunza vinywaji mkuu na mwoka mikate mkuu wa mfalme. 2Farao aliwakasirikia hao maofisa wake wawili, 3akawafungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi, katika gereza, mahali alipofungwa Yosefu. 4Mkuu wa kikosi cha ulinzi akamteua Yosefu awatumikie. Nao wakawa kifungoni kwa muda fulani.
5Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti. 6Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi. 7Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?” 8Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.”
9Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu. 11Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.” 12Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu. 13Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali. 14Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani. 15Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.”
16Yule mwoka mikate mkuu alipoona kwamba tafsiri ile ni nzuri, akamwambia Yosefu, “Hata mimi niliota ndoto! Katika ndoto yangu nilikuwa nimechukua kichwani nyungo tatu za mikate. 17Katika ungo wa juu, kulikuwa na vyakula mbalimbali vilivyookwa kwa ajili ya Farao. Lakini, ndege walikuwa wakivila kutoka ungo huo kichwani pangu!” 18Yosefu akamwambia, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Zile nyungo tatu ni siku tatu. 19Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani, atakiinua kichwa chako akutundike mtini, nao ndege wataula mwili wako.”
20Mnamo siku ya tatu, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Farao aliwaandalia karamu watumishi wake wote. Akawatoa gerezani mtunza vinywaji wake mkuu na mwoka mikate mkuu, akawaweka mbele ya maofisa wake. 21Kisha akamrudishia cheo chake mtunza vinywaji, apate kumpatia Farao kikombe. 22Lakini yule mwoka mkate mkuu akamtundika mtini, kama Yosefu alivyokuwa amewatafsiria ndoto zao. 23Hata hivyo, yule mtunza vinywaji mkuu akamsahau Yosefu, badala ya kumkumbuka.
Mwanzo40;1-23

Bible Society of Tanzania
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 14 March 2017

Ujumbe Wa Leo;Kutoka Congo-Tafuteni Kwa Bidii na Muishi kwa Amani..




Muwe na Jioni Njema..

"Swahili Na Waswahili"Pamoja Daima.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo39....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu wetu Muumba wetu Muumba Mbingu na Nchi,Mungu wa Abrahamu Isaka na Yakobo,Baba yetu,Mwokozi wetu,Yeye asiyechoka,Yeye husamehe,Yeye asiye lala wala kunsinzia,Yeye si binadamu hata aseme uongo...


Siku hiyo mtasema: “Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, maana ingawa ulinikasirikia, hasira yako imetulia, nawe umenifariji. Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.” Mtachota maji kwa furaha kutoka visima vya wokovu. Siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu mwombeni kwa jina lake. Yajulisheni mataifa matendo yake, tangazeni kuwa jina lake limetukuka. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa kwa kuwa ametenda mambo makuu; haya na yajulikane duniani kote. Pazeni sauti na kuimba kwa furaha, enyi wakazi wa Siyoni, maana aliye mkuu miongoni mwenu ndiye Mungu, Mtakatifu wa Israeli.”

Asante Baba wa Mbinguni kwa kibali ulichotupa na kutuchagua tena kuiona siku hii,Si kwamba sisi ni wema sana ,Si kwamba wajuaji na wenye nguvu,Sikwamba sisi ni bora sana kuliko wengine,Ni kwa Neema/Rehema zako tuu Baba wa mbingu...
Tunaomba ukatulinde,ukatubariki katika kazi,Biashara,Masomo,Hatua zetu zikawe nawe Baba wa Mbinguni,Kuingiakwetu/Kutokakwetu,Vyombo vya Usafri,TutembeapoVilaji/Vinywaji..
Ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/Kutumia... na  ukatutakase Miili yetu/Akilizetu ..
Roho MtakatifuKu akatuongoze kwenye kunena/kutenda..
Ukatutumie na kutupa sawasawa na mapenzi yako...
 Mfalme wa Amani..
Ukawaponye/Kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo vya mwovu,Wagonjwa,Wafiwa wakawe mfariji wao,Wajane na Yatima Baba ukawabariki,Wenye shida/Tabu Baba ukawanyooshee mkono wako na kuwagusa

Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu![2Wakorintho 6:2]

Tunarudisha Sifa na Utukufu ni kwako Mungu wetu,Tunajiachilia mikononi mwako, Tukishukuru na Kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu...
Amina...!!!!



Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.[Waebrania 13:21]

Mke wa Potifa na Yosefu

1Basi, Yosefu alipochukuliwa mpaka Misri, Mmisri mmoja aitwaye Potifa ambaye alikuwa ofisa wa Farao na mkuu wa kikosi chake cha ulinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri. 2Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, akamfanikisha sana. Yosefu akawa anakaa katika nyumba ya bwana wake, Mmisri. 3Huyo bwana wake akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu, na kwamba ndiye aliyeyafanikisha mambo yote aliyofanya Yosefu. 4Basi, Yosefu akapendeka sana mbele ya Potifa, hata akawa ndiye mtumishi wake binafsi; alimfanya msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake yote. 5Tokea wakati Potifa alipomfanya Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba yake na mwangalizi wa mali yake, Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya huyo Mmisri kwa ajili ya Yosefu. Baraka za Mwenyezi-Mungu zikawa juu ya kila alichokuwa nacho, nyumbani na shambani. 6Kwa sababu hiyo Potifa alimpa Yosefu mamlaka juu ya mambo yake yote, naye Potifa akaacha kushughulika na chochote isipokuwa tu chakula chake mwenyewe.
Yosefu alikuwa kijana mzuri na wa kupendeza. 7Basi, baada ya muda fulani, mke wa Potifa akamtamani Yosefu na kumwambia, “Lala na mimi”. 8Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena. 9Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.” 10Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe.
11Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani. 12Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje. 13Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje, 14akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!”
16Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani. 17Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha. 18Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.” 19Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira, 20akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme. 21Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza. 22Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake. 23Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya.
Mwanzo39;1-23

Bible Society of Tanzania"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 13 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo38....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Kutupa Nafasi na Kibali cha kuiona siku/wiki hii..
Tumsifu na Kumtukuza yeye Daima..

Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake. Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu! Umsifu Mungu wako, ee Siyoni! Maana yeye huimarisha milango yako, huwabariki watu waliomo ndani yako. Huweka amani mipakani mwako; hukushibisha kwa ngano safi kabisa. Yeye hupeleka amri yake duniani, na neno lake hufikia lengo lake haraka. Hutandaza theluji kama pamba, hutawanya umande kama majivu. Huleta mvua ya mawe kama kokoto na kwa ubaridi wake maji huganda. Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka; huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka. Humjulisha Yakobo ujumbe wake, na Israeli masharti na maagizo yake. Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine; watu wengine hawayajui maagizo yake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Asante Baba kwa wema na Fadhili zako,Ukaibariki siku/wiki hii na ukatubariki katika kazi zetu,Biashara,Masomo,Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Hatuaze ziwe nawe ee Mungu Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,
Ukatutakase akili zetu Miili yetu,Utusamehe tulipo kwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni..Nasi tunaomba tuwezeshe kuwasamehe waliotukosea..
Utubariki na kutufanya  chombo chako tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki kipato chetu kiingiacho na kitokacho Baba ukakiguse na kupata kibali chako katika matumizi yetu..
Tunarudisha shukrani kwako ee Mungu wetu,Sifa na Utukufu ni kwako..
Tuanajiachilia mikononi mwako Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu
Amina...!!!!!!
Muwe na Wakati mwema..Tuanze na Mungu.


Yuda na Tamari

1Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira. 2Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa. 3Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri. 4Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani. 5Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu.
6Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari. 7Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua. 8Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.” 9Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto. 10Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia. 11Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake.
12Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake. 13Tamari aliposikia kwamba baba mkwe wake alikuwa njiani kwenda Timna kukata manyoya ya kondoo wake, 14alivua mavazi yake ya ujane na kujifunika shela kisha akaketi penye lango la kuingilia Enaimu, kijiji kilichokuwa njiani kwenda Timna. Alifanya hivyo kwa vile aliona kwamba Shela alikwisha kuwa mtu mzima, lakini yeye Tamari hakuozwa awe mkewe.
15Basi, Yuda alipomkuta Tamari hapo, alimdhania kuwa mwanamke malaya, kwani alikuwa amejifunika uso. 16Hapo, bila kujua kwamba huyo alikuwa mke wa mwanawe, akamwendea pale kando ya njia, akamwambia, “Napenda kulala nawe.” Tamari akamwuliza, “Utanipa nini nikikubali?” 17Yuda akamjibu, “Nitakupa mwanambuzi kutoka kundi langu.” Tamari akamwambia, “Weka rehani kuthibitisha utaniletea huyo mwanambuzi.” 18Yuda akamwuliza, “Unataka nikupe nini kama rehani?” Naye akamjibu, “Nipe hiyo pete na kamba yake pamoja na hiyo fimbo unayoshika.” Basi, Yuda akampa vitu hivyo vyote, akalala naye. Tamari akapata mimba yake. 19Basi, Tamari akarudi nyumbani akavua ile shela aliyojifunika, akavaa tena mavazi yake ya ujane.
20Wakati Yuda alipomtuma yule rafiki yake, Mwadulami, ampelekee yule mwanamke mwanambuzi ili arudishiwe rehani aliyomwachia, Hira hakumpata. 21Hira akawauliza wenyeji wa Enaimu, “Yuko wapi yule mwanamke kahaba aliyekuwa kando ya njia karibu na hapa?” Wakamjibu, “Hapa hapajawa na mwanamke kahaba.” 22Basi, huyo rafiki akarudi kwa Yuda, akamwambia, “Sikumpata! Tena wenyeji wa huko wameniambia kwamba hapajawa na mwanamke kahaba yeyote huko.” 23Yuda akasema, “Acha avichukue vitu hivyo, la sivyo atatufanya tuchekwe. Wewe mwenyewe umeona kwamba nilimpelekea mwanambuzi, lakini wewe hukumpata.”
24Baada ya miezi mitatu, Yuda akapata habari, “Tamari, mke wa mwanao amekuwa kahaba, tena amepata mimba kwa kufanya ukahaba.” Basi, Yuda akaamuru, “Mtoeni nje achomwe moto!” 25Walipokuwa wakimtoa nje, Tamari akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake, akisema, “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba. Kwa hiyo, nakuomba umtambue mwenye pete hii na kamba yake, na fimbo hii.” 26Yuda alivitambua vitu hivyo, akasema, “Tamari ni mwadilifu kuliko mimi. Ni kweli, maana sikumwoza kwa mwanangu Shela.” Tokea siku hiyo Yuda hakulala tena na Tamari.
27Wakati wa kujifungua kwake Tamari ulipofika, ikafahamika kuwa alikuwa na mimba ya mapacha. 28Basi, alipopata uchungu wa kuzaa pacha mmojawapo alitoa mkono nje, naye mkunga akaufunga kwa uzi mwekundu, akisema, “Huyu ndiye aliyezaliwa kwanza.” 29Lakini huyo mtoto alipourudisha mkono wake ndani, ndugu yake akazaliwa wa kwanza. Mkunga akasema, “Mbona wewe umepita kwa nguvu?” Kwa hiyo akaitwa Peresi. 30Baadaye ndugu yake akazaliwa akiwa na ule uzi mwekundu mkononi, naye akaitwa Zera.
Mwanzo38;1-30

Bible Society of Tanzania
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday, 12 March 2017

Natumaini Jumapili inaendelea Vyema;"Wanawake ni Nguvu ya Jamii",[Hongera Wanawake]Burudani kwa Mwanamke,Emmy Kosgei_Mama,TAAI (we are moving forward )

Wapendwa /Waungwana Ni matumaini yangu jumapili inaendelea vyema,pia Wanawake mlisheherekea/Manaendelea kusheherekea Vyema siku Yenu..Pia naamini Wanaume mlikuwa/mko sambamba kuungana na Wanawake kwenye siku yao..
Mwanamke ni nani kwako wewe Mwanaume?
Jee wewe Mwanamke unajitambua na kujivunia kuwa Mwanamke?
Nini kikubwa hutakisahau chema/kibaya ulichokifanya kama Mwanamke ulipaswa kukifanya/kutokifanya?
Mungu aendelee kuwabariki na kuwaongoza katika majukumu yenu kama Wanawake.
Neno La Leo;Esta 2;1-23

Esta anateuliwa kuwa malkia

1Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. 2Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? 3Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. 4Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo.
5Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. 6Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni.
7Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake.
8Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. 9Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie.
10Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. 11Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
12Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero. 13Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu. 14Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.
15Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye. 16Basi, Esta alipelekwa ikulu kwa mfalme katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Ahasuero, mwezi wa kumi uitwao Tebethi. 17Mfalme alipendezwa zaidi na Esta kuliko alivyopendezwa na wanawake wengine wote. Alipendwa sana kuliko wasichana wengine. Basi, mfalme akamvika taji ya kimalkia kichwani, akamfanya malkia badala ya Vashti. 18Kisha mfalme akaandaa karamu kubwa kwa heshima ya Esta, akawaalika viongozi na watumishi wote wa serikali yake. Pia, mfalme alitangaza msamaha wa kodi katika mikoa yote, akatoa zawadi nyingi kulingana na hadhi yake ya kifalme.










Mordekai aokoa maisha ya mfalme

19Wasichana walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi penye lango la mfalme. 20Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye.
21Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. 22Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. 23Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.