Anayeonywa mara nyingi akawa mkaidi, ataangamia ghafla asipone tena. Waadilifu wakitawala watu hufurahi, lakini waovu wakitawala watu hulalamika. Apendaye hekima humfurahisha baba yake; lakini aandamanaye na malaya hufuja mali yake. Mfalme akitumia haki huipatia nchi uthabiti, lakini akipenda hongo taifa huangamia. Mwenye kumbembeleza jirani yake, anatega mtego wa kujinasa mwenyewe. Mtu mbaya hunaswa kwa kosa lake, lakini mtu mwadilifu huimba na kufurahi. Mwadilifu anajua haki za maskini, lakini mtu mwovu hajui mambo hayo. Wenye dharau huutia vurugu mji mzima, lakini wenye hekima hutuliza ghadhabu. Mwenye hekima akibishana na mpumbavu, mpumbavu huwaka hasira na kucheka bila kutulia. Wapendao kumwaga damu humchukia mtu asiye na hatia, lakini watu wema huyalinda maisha yake. Mpumbavu huonesha hasira yake wazi, lakini mwenye hekima huizuia na kuituliza. Mtawala akisikiliza mambo ya uongo, maofisa wake wote watakuwa waovu. Maskini na mkandamizaji wanafanana kwa kitu kimoja: Wote wawili wamepewa macho na Mwenyezi-Mungu. Mfalme anayewaamua maskini kwa haki, atauona utawala wake umeimarika milele. Adhabu na maonyo huleta hekima, lakini mtoto aliyeachwa afanye apendavyo humwaibisha mama yake. Waovu wakitawala maovu huongezeka, lakini waadilifu watashuhudia kuanguka kwao. Mpe nidhamu mwanao naye hatakupa wasiwasi; yeye ataufurahisha moyo wako. Pasipo maono ya kinabii watu hukosa nidhamu; heri mtu yule anayeshika sheria. Mtumwa haonyeki kwa maneno matupu, maana ingawa anayaelewa yeye hatayatii. Wamwona mtu apayukaye bila kufikiri? Mtu mpumbavu ni afadhali kuliko yeye. Ambembelezaye mtumwa wake tangu utoto, mwishowe mtumwa huyo atamrithi. Mwenye ghadhabu huchochea ugomvi, mtu wa hasira husababisha makosa mengi. Kiburi cha mtu humporomosha mwenyewe, lakini mnyenyekevu wa roho atapata heshima. Anayeshirikiana na mwizi anajidhuru mwenyewe; husikia laana ya aliyeonewa bila kusema neno. Kuwaogopa watu ni kujitega mwenyewe, lakini anayemtumaini Mwenyezi-Mungu yu salama. Wengi hupenda kujipendekeza kwa mtawala, hali mtu hupata haki yake kwa Mwenyezi-Mungu. Mdhalimu ni chukizo kwa mnyofu, naye mnyofu ni chukizo kwa mwovu.
Methali 29:1-27
"Swahili Na Waswahili"Pamoja Daima.