Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 13 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 16 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..
Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
si kwamba sisi tumetenda mema sana,si kwa nguvu/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa Neema/rehema zako Mungu wetu..
Tunakushukuru Mungu wetu,Tunakuabudu Jehovah..
Uhimidiwe Yahweh,Unastahili sifa Jehovah..
unatosha Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Huruma..
Muweza wa yote,Mponyaji,Mfaji,Alfa na Omega..
Hakuna kama wewe...

Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu  wetu..!



Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala! Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu). Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.” Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.”

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mfalme wa Amani tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..





“Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: “Mimi niitwaye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu nasema hivi. Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: Baridi au moto. Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! Wewe unajisema, ‘Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote;’ kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi! Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona. Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo uwe na bidii na kutubu. Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami. “Mshindi nitamjalia kuketi pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!”

Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Mungu wetu tunaomba ukatubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo ...
Jehova nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..

Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
 Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mungu wetu tunaomba ukabariki Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi/wazee wetu,Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni ukatulinde na ukatupe Amani,kupendana,kusaidiana,kuhurumiana,kuchukuliana na kuonyana kwa  hekima na busara..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..




Kisha, nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: Watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Wakapaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!” Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na wale viumbe hai wanne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu, wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!” Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?” Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa. Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena, kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”

Mungu wetu ukatufanye Barua njema na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mfalme wa Amani tunaomba ukawaponye na kuwagusa wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa,wenye shida/tabu na wote wanaoteseka na yule mwovu..
ukawape uponyaji wa mwili na roho pia,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako ili wawe huru..

Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa pamoja..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yampendezezayo..
Nawapenda.

Pasaka

(Kut 12:1-20)

1“Adhimisheni mwezi wa Abibu na kufanya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana katika mwezi huo wa Abibu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwatoa Misri wakati wa usiku. 2Mtatoa sadaka ya Pasaka kutoka mifugo yenu ya kondoo au ng'ombe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atachagua likae jina lake. 3Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso – kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri. 4Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi. 5Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, 6bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri. 7Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu. 8Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo.

Sikukuu ya mavuno

(Kut 34:22; Lawi 23:15-21)

9“Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka. 10Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 11Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake. 12Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya.

Sikukuu ya vibanda

(Lawi 23:33-43; Hes 29:12-39)

13“Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. 14Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu. 15Kwa siku saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sherehe mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atapachagua; kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki kwa mazao yenu yote na katika shughuli zenu zote nanyi hakika mtafurahi.
16“Wanaume wote wa taifa lenu watakuja mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mara tatu kila mwaka, mahali atakapopachagua: Wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya kuvuna majuma na wakati wa sikukuu ya vibanda. Wasiende mbele ya Mwenyezi-Mungu mikono mitupu. 17Wote watatoa kadiri wanavyoweza kulingana na baraka Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowajalia.

Mwongozo juu ya haki za watu

18“Mtateua waamuzi na maofisa kutoka makabila yenu katika miji yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, nao watatoa hukumu za haki kwa watu. 19Msipotoshe haki; msiwe na upendeleo, wala msikubali kupokea rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya watu wenye hekima na kupotosha kesi ya mtu mwadilifu. 20Mtazingatia haki tu, ili mpate kuishi na kuimiliki nchi mnayopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
21“Msipande mti wowote uwe nguzo ya mungu wa uongo karibu na meza ya madhabahu sadaka mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 22Wala msisimamishe nguzo ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wako anaichukia.




Kumbukumbu la Sheria 16:1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 12 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 15 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..! ni siku nyingine tena Mungu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwa Neema hii ya pumzi na uzima..

Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada.


Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unatosha Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote,wewe ni mwanzo na mwisho,Alfa na Omega..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Hakuna kama wewe....

Jehovah tunakuja mbele zako tukinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa rehema tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Mfalme wa Amani tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


“Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.



Baba wa Mbninguni tunaomba ukabariki,ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende kama ikupasavyo..

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi/wazee wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mungu wetu ukaonekane na kutubariki..
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..

“Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao! Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”

Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...




Petro akamwambia, “Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?” Bwana akajibu, “Ni nani, basi, aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao? Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote. Lakini, kama mtumishi huyo akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia sana kurudi;’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa, bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamwadhibu mtumishi huyo vibaya na kumweka fungu moja na wasioamini. Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atadaiwa vingi; aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi.


Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,waliokata tamaa,waliokataliwa..
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..
Ukawape uponyaji wa mwili na roho pia..
Ukawape neema ya kutambua/kujitambua na kusimamia Neno lako..
Na waweze kukuomba Mungu na ukuwaokoe katika mitego yote ..
Mungu wetu usikie kuomba kwao na ukawatendee kama inavyokupendeza wewe..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami..
Mungu mwenye upendo aendelee kudumisha pendo lenu kwa watu wote..
Akawabariki na mkawabariki wengine..
Amani iwe nayi wakati wote..
Nawapenda.




Mwaka wa Sabato

(Lawi 25:1-7)

1“Kila mwisho wa mwaka wa saba mtawasamehe wadeni wenu wote. 2Hivi ndivyo mtakavyofanya: Kila mmoja aliyemkopesha jirani yake, alifute hilo deni, wala asijaribu kumdai kwa sababu Mwenyezi-Mungu mwenyewe ameamua deni hilo lifutwe. 3Mnaweza kuwadai wageni, lakini madeni yote ya ndugu zenu wenyewe mtayafuta.
4“Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika nchi anayowapa iwe mali yenu. Hakuna hata mmoja atakayekuwa maskini kati yenu, 5mradi tu mumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kufuata kwa uangalifu amri ninazowapeni hivi leo. 6Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama vile alivyowaahidi. Nanyi mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Kadhalika mtatawala mataifa mengi, lakini mataifa hayo hayatawatawala nyinyi.
7“Kukiwa na maskini wa jamaa yenu katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu atawapa, msiwe wachoyo na wagumu kwake. 8Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake. 9Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu. 10Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo. 11Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu.

Jinsi ya kuwatendea watumwa

(Kut 2:1-11)
12“Kama nduguyo Mwebrania, mwanamume au mwanamke, akiuzwa kwako, atakutumikia kwa miaka sita, lakini katika mwaka wa saba, utamwacha huru. 13Nawe utakapomwacha huru, usimwache aende mikono mitupu. 14Mpe kwa ukarimu kile ambacho Mwenyezi-Mungu amekubariki: Kondoo, nafaka na divai. 15Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa huko Misri na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa; ndiyo maana leo nawaamuru hivyo. 16Lakini akikuambia, ‘Sitaondoka kwako,’ kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako na anaridhika kuishi nawe, 17basi, utachukua shazia na kutoboa sikio lake mpaka hiyo shazia iingie mlangoni naye atakuwa mtumwa wako milele. Kadhalika mtendee vivyo hivyo mtumwa wako wa kike. 18Wala usione ugumu utakapomwacha huru mtumwa wako, maana, amekutumikia kwa muda wa miaka sita kwa nusu ya ujira wa mtumishi wa kuajiri. Fanya hivyo, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakubariki kwa kila utakalofanya.

Wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo

19“Mtolee Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa kundi lako la ng'ombe na kondoo. Usiwafanyize kazi ng'ombe hao na kondoo hao usiwakate manyoya. 20Kila mwaka, wewe na jamaa yako mtakula wanyama hao mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua. 21Lakini mnyama huyo akiwa na dosari yoyote, yaani akiwa kilema au kipofu, au ana kasoro yoyote kubwa, usimtoe kuwa sadaka kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. 22Utamla mnyama wa namna hiyo ukiwa katika mji wako; pia wote walio safi na wasio safi wanaweza kumla kama unavyokula paa au kulungu. 23Lakini usile damu yake; bali hiyo utaimwaga chini kama maji.



Kumbukumbu la Sheria 15:1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 11 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 14 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na 
ametupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,
si kwa nguvu zetu au akili zetu..
Hapana ni kwa neema na rehema zake Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo...


Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe. Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.

Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Unastahili sifa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuabudiwa Jehovah..
Unastahili kutukuzwa Yahweh,Unastahili kuheshimiwa Mungu wetu..
Matendo yako ni ya Ajabu,Wema na fadhili zako  zatutosha..

Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’” Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.


Sifa na Utukufu ni kwako Mungu wetu..
Tunakuja Mbele zako Mungu wetu,Tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Upendo nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..

Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.” Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”

Yahweh utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. “Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu,” yasema Maandiko. Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: Wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, sitakuwa na huruma. Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu. Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu. Jichunguzeni nyinyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni nyinyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi nyinyi mmeshindwa. Lakini natumaini kwamba nyinyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa. Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa. Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli. Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini nyinyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu. Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa. Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni. Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.

Mungu Baba tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba  ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Ukatuongoze katika yote tunayoenda kufanya/kutenda
 na tukatende kamainavyokupendeza wewe..
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako,Amri na Sheria zako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Asante Mungu wetu na yote tunayaweka mikononi mwako..
Tuliyoyanena na tusiyo yanena Mungu wetu unayajua na kutujua sisi zaidi ya tunavyojijua..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami..
Mungu aendelee kuwalinda na kuwatendea kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.



Desturi za maombolezo zilizokatazwa

1“Nyinyi ni watoto wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; msijichanje wala kunyoa upara kwa ajili ya mtu aliyefariki. 2Nyinyi ni watu watakatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; Mwenyezi-Mungu amewachagua muwe watu wake hasa, kati ya watu wote waishio duniani.

Wanyama safi na najisi

(Lawi 11:1-47)
3“Msile kitu kilicho chukizo kwa Mungu. 4Mnaweza kula wanyama wafuatao: Ng'ombe, kondoo, mbuzi, 5kulungu, paa, kongoni, mbuzimwitu, paa mweupe, pofu na mbuzi wa mlimani; 6na kila mnyama mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na mwenye kucheua, huyo mnaweza kula. 7Lakini msile mnyama yeyote ambaye kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili na hacheui; msile ngamia, sungura na pelele, ingawa hucheua lakini kwato zao hazikugawanyika sehemu mbili; hao ni najisi kwenu. 8Pia msile nguruwe, maana ijapokuwa kwato zake zimegawanyika sehemu mbili, yeye hacheui; hao ni najisi kwenu, msile nyama zao wala msiguse mizoga yao.
9“Mnaweza kula kila aina ya samaki wenye mapezi na magamba. 10Lakini kiumbe chochote kinachoishi majini kisicho na mapezi wala magamba msile; hivyo ni najisi kwenu.
11“Mnaweza kula ndege wote walio safi. 12Lakini msile ndege wafuatao: Furukombe, kipungu, 13kengewa, kozi, mwewe kwa aina zake, 14kunguru kwa aina zake, 15mbuni, kirukanjia, dudumizi, kipanga kwa aina zake, 16bundi, mumbi, bundi mkubwa, 17mwari, nderi, mnandi, 18membe, koikoi kwa aina zake, hudihudi na popo. 19Na wadudu wote wenye mabawa ni najisi kwenu; msiwale. 20Mnaweza kula viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi. 21Msile nyamafu yoyote; mnaweza kumpa mgeni anayeishi katika miji yenu, ale, au mnaweza kumwuzia mtu wa taifa lingine, kwa sababu nyinyi ni watakatifu na Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Msimchemshe mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.

Sheria kuhusu zaka

22“Toeni sehemu moja ya kumi ya mazao yenu yote ya shambani kila mwaka. 23Halafu nendeni mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amepachagua kuweka jina lake, na mkiwa mbele yake mtaila zaka ya nafaka yenu, ya divai yenu na ya mafuta, na ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu; fanyeni hivi ili mjifunze kumcha Mwenyezi-Mungu Mungu wenu daima. 24Ikiwa safari ni ndefu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amechagua mahali pa kuweka jina lake ambapo ni mbali mno na nyumbani, nanyi hamwezi kubeba zaka za mazao yenu ambayo Mwenyezi-Mungu amewajalia kupata, basi, fanyeni hivi:
25“Uzeni mazao yenu na kuchukua fedha hiyo mpaka mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alipopachagua, 26mzitumie hizo fedha kwa chochote kile mtakachopenda – nyama ya ng'ombe, nyama ya kondoo, divai au kinywaji kikali; mtavila na kufurahi hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, pamoja na jamaa zenu. 27Msiwasahau Walawi wanaoishi miongoni mwenu; wao hawana fungu wala urithi wao kati yenu. 28Na kila mwisho wa mwaka wa tatu toeni zaka ya mazao yenu yote na kuyaweka akiba katika miji yenu. 29Hiyo itakuwa kwa ajili ya Walawi, kwa kuwa hawana fungu wala urithi wao kati yenu, nao wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu, watakuja kula na kushiba. Fanyeni hivi naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, awabariki katika kazi zenu zote mfanyazo kwa mikono yenu.



Kumbukumbu la Sheria 14:1-29

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday, 8 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 13 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..!
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mwokozi wetu,Mlinzi wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mume wa Wajane,Baba wa Yatima,Mungu mwenye upendo..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe,Uabudiwe,Uhidiwe Yahwe..
Unatosha Mungu wetu,Matendo yako ni ya Ajabu..!

Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe.
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Utuepushe katika majaribu Jehovah utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..



Endeleeni kupendana kindugu. Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao. Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?” Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..
Tunaomba ulinzi wako na Baraka zako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi/wazee wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Mungu Baba tunaomba uwafunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako Yahweh..
Ukatufanye chombo chema na tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina. Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni. Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu. Wasalimuni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni. Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.
Baba wa Mbinguni tunaomba Amani yako ikatawale katika mji huu na Nchi hii tunayoishi..
Baba wa Mbinguni usiiache Tanzania tunaomba unyooshe mkono wako wenye nguvu na uponyaji kwa wote wanaopitia magumu/majaribu..
Baba wa Mbinguni ukatawale na kuwaongoza katika yote..
Amani yako iwe nao daima..wawe na hofu ya Mungu na kufuata Amri,Sheria na Neno lako..
Ukawape Hekima,Busara na Upendo katika yote..
Ukaifunike Tanzania kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Baba Mungu  hakuna lisilowezekana mbele zako..


Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.”
Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure.

Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tukiamini na kukuabudu Milele..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami.
Mungu aendelee kuwabariki..
Nawapenda. 



1“Akitokea nabii au mtabiri wa ndoto miongoni mwenu, akawaahidi na kuwapa ishara au maajabu fulani, 2halafu ishara au maajabu hayo yatokee, kisha aseme: ‘Tufuate miungu mingine na kuitumikia, (miungu ambayo hamjapata kuijua)’, 3msisikilize maneno yake nabii huyo au mtabiri wa ndoto, kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawatumia wao kuwajaribu, ili ajue kama mnampenda yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4Mfuateni na kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika amri zake na kuitii sauti yake; mtumikieni na kuambatana naye. 5Lakini nabii huyo au mtabiri wa ndoto atauawa, kwa sababu atakuwa amewafundisha uasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka utumwani, ili muiache njia ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwaamuru muifuatea. Hivyo ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
6“Ikiwa ndugu yako wa tumbo moja, au mtoto wako wa kiume au wa kike, au mke wako umpendaye sana, au rafiki yako mwandani, atakushawishi kwa siri akisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine’, miungu ambayo wewe wala babu zenu hamuijui, 7au baadhi ya miungu ya watu wanaoishi karibu nanyi, au miungu ya watu waishio mbali toka ncha moja ya dunia hadi nyingine, 8usikubali kushawishiwa, wala usimsikilize au kumhurumia, wala usimwachilie wala kumficha; 9bali utamuua. Wewe utakuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumuua, kisha watu wengine wote watafuata. 10Mpigeni mawe mpaka afe! Kwa sababu amejaribu kukuvutia mbali na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, aliyekutoa utumwani nchini Misri. 11Hivyo, Waisraeli wote watasikia na kuogopa, na kamwe hawatafanya uovu kama huo.
12“Mtakapoishi katika miji ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapa, huenda mkasikia 13kuwa watu fulani mabaradhuli miongoni mwenu, wamewashawishi watu wa mji wakisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine,’ miungu ambayo bado hamjawahi kuijua, 14basi mtapeleleza na kufanya uchunguzi na kuuliza kwa makini; na kama ni kweli kuwa jambo la kuchukiza limetendeka kati yenu, 15hamna budi kuwaua kwa upanga watu wa mji huo; mtauangamiza kabisa mji huo na kuwaua ng'ombe wote kwa upanga. 16Mtakusanya nyara zake zote katika uwanja wa hadhara wa mji na kuzichoma kwa moto kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wenu; mji huo utakuwa rundo la magofu milele, nao hautajengwa tena. 17Msichukue kitu chochote kilichotolewa kiteketezwe, ili Mwenyezi-Mungu aache ile hasira yake kali, awaoneshe rehema na huruma, na kuwafanya muwe wengi sana kama alivyowaahidi babu zenu, 18kama tu mtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkishika amri zake zote ninazowapa hivi leo, na kufanya yaliyo sawa mbele yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.



Kumbukumbu la Sheria 13:1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.