"Swahili Na Waswahili"Pamoja Daima.
Thursday, 12 October 2017
Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 3..
Waisraeli wanavuka mto Yordani
1Asubuhi na mapema Yoshua pamoja na watu wote wa Israeli walianza safari kutoka Shitimu. Walipoufikia mto Yordani, walipiga kambi hapo kwa muda kabla ya kuvuka. 2Baada ya siku tatu, viongozi walipita katikati ya kambi hiyo, 3wakawaambia watu, “Mtakapoliona sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, limebebwa na makuhani Walawi, mtaondoka na kulifuata; 4ndivyo mtakavyojua njia ya kupita maana hamjapita huku kamwe. Lakini msilikaribie mno sanduku la agano; muwe umbali wa kilomita moja hivi.”
5Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni kwa kuwa kesho Mwenyezi-Mungu atatenda maajabu kati yenu.” 6Kisha akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, mtangulie nalo mbele ya watu.” Nao wakalichukua na kutangulia mbele ya watu.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua: “Leo hii, nitaanza kukutukuza mbele ya watu wote wa Israeli ili wajue kwamba, kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo pia nitakavyokuwa pamoja nawe. 8Utawaamuru hao makuhani wanaobeba sanduku la agano wasimame karibu na ukingo wa mto Yordani wakati watakapofika huko.”
9Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli: “Njoni karibu mpate kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” 10Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa. 11Tazameni, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote, liko karibu kupita mbele yenu kuelekea mtoni Yordani. 12Sasa, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, kila kabila mtu mmoja. 13Wakati nyayo za makuhani wanaobeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Bwana wa dunia yote, zitakapoingia katika maji ya mto Yordani, maji ya mto huo yataacha kutiririka. Na yale yatakayokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yatajikusanya pamoja kama rundo.”
14Basi, watu waliondoka katika kambi zao ili kwenda kuvuka mto Yordani, nao makuhani wakiwa wamebeba sanduku la agano wanawatangulia watu. 15Na mara tu hao waliobeba sanduku la agano walipofika Yordani na nyayo zao zilipokanyaga ukingoni mwa mto huo (mto Yordani hufurika wakati wa mavuno), 16maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yalisimama na kurundikana mpaka huko Adamu kijiji kilicho karibu na mji wa Sarethani. Maji yaliyokuwa yanateremka kwenda bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yalitoweka kabisa, watu wakavuka mbele ya Yeriko. 17Wakati Waisraeli walipokuwa wanavuka makuhani waliokuwa wanalibeba sanduku la agano walisimama mahali pakavu katikati ya mto Yordani mpaka taifa lote likavuka.
Yoshua 3;1-17
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Wednesday, 11 October 2017
Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 2..
Yoshua anawatuma wapelelezi Yeriko
1 Taz Ebr 11:31; Yak 2:25 Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kwa siri kutoka Shitimu waende kufanya upelelezi, katika nchi ile na hasa mji wa Yeriko. Wakaenda, wakafika kwenye nyumba ya malaya mmoja aliyeitwa Rahabu wakalala humo.
2Mfalme wa mji wa Yeriko akaambiwa, “Tazama, wanaume wawili Waisraeli wameingia mjini leo usiku ili kuipeleleza nchi.” 3Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje watu waliokuja nyumbani kwako kwani wamekuja kuipeleleza nchi yote.” 4Lakini, yule mwanamke alikuwa amekwisha waficha watu hao wawili. Basi, akawaambia wajumbe hao, “Ni kweli kwamba hao watu walikuja kwangu, lakini mimi sikujua wametoka wapi. 5Wakati wa kufunga lango la mji, giza lilipoingia, hao watu waliondoka. Kule walikokwenda mimi sijui; wafuateni upesi nanyi mtawapata.” 6Lakini Rahabu alikuwa amewapandisha hao wapelelezi kwenye paa na kuwaficha kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandaza huko paani. 7Basi, wale watu waliotumwa na mfalme wakawafuatia kwa kupitia njia iliyokuwa imeelekea kwenye vivuko vya Yordani. Na mara tu walipoondoka mjini, lango la mji likafungwa. 8Rahabu akawaendea hao wapelelezi juu darini kabla hawajalala, 9akawaambia, “Mimi ninajua kwamba Mwenyezi-Mungu amewapa nchi hii; tumekumbwa na hofu juu yenu na wakazi wote wa nchi hii wamekufa moyo kwa sababu yenu. 10Taz Kut 14:21; Hes 21:21-35 Maana tumesikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri, na jinsi mlivyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, yaani Sihoni na Ogu, ambao mliwaangamiza kabisa. 11Mara tu tuliposikia mambo hayo, tulikufa moyo kabisa kwa sababu yenu, tukaishiwa nguvu kabisa. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani! 12Kwa hiyo basi, tafadhali mniapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba mtanitendea kwa wema mimi na jamaa yangu kama vile mimi nilivyowatendeeni kwa wema, na mnipe uthibitisho kamili. 13Ahidini kwamba mtamsalimisha baba yangu na mama yangu, kaka zangu na dada zangu, na jamaa yao yote; hamtakubali tuuawe!”
14Wale watu wakamjibu, “Uhai wenu ni uhai wetu! Kama hamtaifichua siri yetu, Mwenyezi-Mungu atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa wema na uaminifu.”
15Basi, Rahabu akawashusha hao watu kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa ikiambatana na ukuta wa mji wa Yeriko. 16Akawaambia: “Nendeni mlimani mkajifiche huko ili wanaowafuatia wasiwakute. Kaeni huko kwa muda wa siku tatu, mpaka wanaowafuatia watakapokuwa wamerudi mjini, kisha mwende zenu.” 17Hao watu wakamwambia, “Sisi tutalitimiza kabisa jambo ulilotufanya tuahidi kwa kiapo. 18Tutakapokuja katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu kwenye dirisha ambalo umetuteremshia. Uwakusanye hapa kwako baba yako, mama yako na kaka zako na jamaa yote ya baba yako. 19Lakini mtu yeyote akitoka nje ya nyumba yako na kwenda mitaani hatutakuwa na lawama juu ya kifo chake. Lakini kama mtu yeyote atakayekuwamo ndani ya nyumba yako akiguswa tu, basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yetu. 20Lakini kama ukimwambia mtu yeyote juu ya shughuli hii yetu, basi, sisi hatutabanwa na kiapo ulichotufanya tukuapie.” 21Naye akawaambia “Na iwe jinsi mlivyosema.” Kisha akawaruhusu waende zao, nao wakaondoka. Naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
22Wapelelezi hao waliondoka wakaenda milimani. Walikaa huko kwa muda wa siku tatu mpaka wale waliokuwa wanawafuatia waliporudi mjini Yeriko, baada ya kuwatafuta na kukosa kuwaona. 23Basi, hao wapelelezi wawili wakashuka kutoka milimani, wakavuka mto na kumwendea Yoshua, mwana wa Nuni; wakamwambia yote yaliyowapata. 24Wakamwambia “Hakika Mwenyezi-Mungu ameitia nchi yote mikononi mwetu. Tena wakazi wa nchi hiyo wamekufa moyo kwa sababu yetu.”
Yoshua 2;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Tuesday, 10 October 2017
Kikombe Cha Asubuhi ;Leo tunaanza Kitabu cha Yoshua 1..
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje? Haleluyah..!Tunamshukuru Mungu kwa kumemaliza kitabu cha Kumbukumbu la Sheria (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)katika kitabu kilichopita na vinginevyo huko nyuma.. Mungu wetu yu mwema sana,Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu ni kwa Neema yake Mungu katuwezesha kuwa na utaratibu huu. Basi kufikia mwisho na isiwe mwisho wa kusoma tena.. Hapana tujiwekee muda wa kusoma na kurudia pia huko tulikopita ili tuweze kuhifadhi ,kujikumbusha na kujifunza zaidi.. Tuzidi kumuomba Mungu wetu akatupe Neema,Kiu,Shauku zaidi ya kusoma Neno lake na kusimamia Amri na Sheria zake.. Neno la uhai
Habari hii yahusu Neno la uhai lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni nyinyi pia, ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. Tunawaandikia nyinyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.
Baba wa Mbinguni akatupe maalifa,uelewa tunapoenda kuanza kusomakitabu cha "YOSHUA",Mungu wetu akawe nasi katika kitabu hiki na vingine vijavyo.. Mungu ni mwanga
Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu.. Tumshukuru Mungu kwa ulinzi wake kwetu wakati wote.. Asante Baba wa Mbinguni kwa mema meengi uliyotutendea na unayoendelea kututendea... Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah.. Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unasthahili Mungu wetu.. Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni,Baba wa Baraka,Baba wa Upendo Baba wa Faraja,Mfariji wetu,Mungu mwenye huruma.. Unatosha Yahweh,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya Ajabu.. Sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu.. Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni.. Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa. Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote. Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua. Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye: Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetuBiashara,masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe.. Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu ukatupe nasi neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako.. Mfalme wa Amani tunaomba Amani yako ikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mungu wetu pendo lako likadumu,furaha ikatawale hekima na busara ziwe nasi,utuwema na fadhili visipungue msamaha na kusamehe tunapokosa kuelewana tukaelimishane kwa upendo na Amani,tuchukuliane na kuhurumiana.. Mungu wetu ukatupe Neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu.. Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia. Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza. Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani. Yeyote ampendaye ndugu yake yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine. Lakini anayemchukia ndugu yake yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha. Ninawaandikieni nyinyi watoto kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu. Nawaandikieni nyinyi watoto kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mumemshinda yule Mwovu. Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake. Vitu vyote vya ulimwengu – tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali – vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia vikwazo,majaribu,shida/tabu wagonjwa,wenye njaa,waliokatika vifungo mbalimbali Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho pia wakapate tumaini jipya,amani na wakasimame tena ukawape neema ya kuweza kujiombea,kutambua/kujitambua na kufuata nja zako nazo ziwaweke huru..
Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba mpinzani wa Kristo anakuja, na sasa wapinzani wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu. Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu. Nyinyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli. Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamwujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli. Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Kristo. Mtu wa namna hiyo ni mpinzani wa Kristo – anamkana Baba na Mwana. Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia. Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba. Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: Uhai wa milele. Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha nyinyi. Lakini, kwa upande wenu nyinyi, Kristo aliwatia mafuta kwa Roho wake. Na kama Roho huyo akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana yeye anawafundisheni kila kitu, na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi, shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo. Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu siku ya kuja kwake.
Asante Mungu wetu yote tunayaweka mikononi mwako Tukishukuru na kuamini Mungu wetu u pamoja nasi.. Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele.. Amina..! Wapendwa katika Bwana niwatakiwe Amani ya Bwana.. iwe nanyi,Baraka na upendo wa Kristo uwe nanyi muingiapo/mtokapo Mungu awe nanyi daima.. Nawapenda. |
Mungu anamwamuru Yoshua kuiteka nchi ya Kanaani
1Baada ya kifo cha Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mose: 2“Mtumishi wangu Mose amefariki, sasa vukeni mto Yordani, wewe pamoja na Waisraeli wote hadi kwenye nchi ile ambayo ninawapa. 3Kila mahali mtakapokanyaga nimewapeni kama nilivyomwahidi Mose. 4Mipaka ya nchi yenu itakuwa hivi: Kusini ni jangwa, kaskazini ni milima ya Lebanoni, mashariki ni mto ule mkubwa Eufrate, kupitia nchi yote ya Wahiti hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. 5Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe. 6Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa. 7Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote aliyokuamuru mtumishi wangu Mose. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe utafanikiwa popote uendapo. 8Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo. 9Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”
Yoshua anawatayarisha watu kuvuka mto Yordani
10Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu, 11“Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.”
12 Taz Hes 32:28-32; Kumb 3:18-20; Yosh 22:1-6 Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase: 13“Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’. 14Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ngambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu. 15Mtawasaidia mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowapa ndugu zenu pia mahali pa kupumzikia, kama alivyowapa nyinyi, nao pia wamiliki nchi ambayo wanapewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kisha mtarudi katika nchi ambayo ni mali yenu na kuimiliki, nchi ambayo mlipewa na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, mashariki ya mto Yordani.”
16Wakamjibu Yoshua, “Mambo yote uliyotuamuru tutayafanya, na popote utakapotutuma tutakwenda. 17Kama vile tulivyomtii Mose katika mambo yote, ndivyo tutakavyokutii wewe; Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na Mose. 18Mtu yeyote atakayeasi amri yako au kukataa kutii maneno yako au jambo lolote unalomwamuru, atauawa. Wewe, lakini, uwe na nguvu na kuwa hodari.”
Yoshua 1;1-18
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Monday, 9 October 2017
Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 34 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)
Kifo cha Mose
1Basi, Mose akaondoka kwenye tambarare ya Moabu, akaenda mlimani Nebo, akapanda kilele cha Pisga kilicho mkabala wa Yeriko. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwonesha nchi yote: Toka Gileadi mpaka Dani; 2eneo lote la Naftali, eneo la Efraimu na Manase, eneo lote la Yuda mpaka Bahari ya Mediteranea; 3nyika ya Negebu na eneo la nyika ya bonde la Yeriko, mji wa mitende, mpaka Soari. 4Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Hii ndiyo nchi ile niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo kwamba nitawapa wazawa wao. Nimekuonesha uione kwa macho yako mwenyewe, lakini hutafika huko.”
5Basi, Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu akafariki huko nchini Moabu, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amemesema. 6Mwenyezi-Mungu akamzika34:6 akamzika: Kufuatana na baadhi ya hati za Kigiriki; Kiebrania: Akazika. katika bonde la Moabu, mkabala na mji wa Beth-peori; lakini mpaka leo, hakuna mtu ajuaye mahali alipozikwa. 7Mose alikuwa na umri wa miaka 120 alipofariki; macho yake yalikuwa hayajafifia, na alikuwa timamu na mwenye nguvu. 8Waisraeli waliomboleza kifo chake kwa muda wa siku thelathini kwenye nchi tambarare ya Moabu. Kisha siku za matanga na maombolezo ya kifo chake zikaisha.
9Yoshua mwana wa Nuni alijaa roho ya hekima, kwa kuwa Mose alikuwa amemwekea mikono yake. Hivyo Waisraeli walimtii Yoshua na kufuata amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa Mose.
10Hapajatokea tena nabii katika Israeli kama Mose, ambaye Mwenyezi-Mungu aliongea naye ana kwa ana. 11Hakuna nabii mwingine ambaye alifanya ishara na miujiza kama ile ambayo Mwenyezi-Mungu aliyomtuma Mose afanye juu ya mfalme wa Misri, wakuu wake na nchi yake yote. 12Hakuna nabii mwingine ambaye amefanya mambo makuu na ya kutisha kama alivyofanya Mose mbele ya Waisraeli wote.
Kumbukumbu la Sheria 34:1-12
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Subscribe to:
Posts (Atom)