Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote.. Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na Mbingu Muumba wa vyote vilivyopo,vinavyoonekana na visivyo onekana. Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa walio hai na si Mungu wa wafu,Mungu wa majeshi,Maana wewe si Mungu wa fujo ila ni wa amani,Mungu mwokozi,Mungu uponyaye, kimbilio letu,Matendo yako ni makuu sana,matendo yako ni ya ajabu, hakuna kama wewe Mungu wetu,enyi Mataifa yote msifuni Mwenyezi-Mungu,Enyi watu wote Mhimidini...!!
Yesu alipokuwa anatoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!” Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.”
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu.. Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote.. Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii,si kwamba sisi tumetenda mema sana si kwa nguvu zetu wala utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa neema/rehema zako Mungu wetu,ni kwa mapenzi yako Jehovah.. Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu Mungu wetu,sifa na utukufu ni wako Baba wa Mbinguni..
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?” Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, kila mmoja akisema kuwa yeye ni mimi! Nao watawapotosha watu wengi. Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. “Lakini nyinyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, ili mpate kunishuhudia kwao. Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si nyinyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanawe; watoto nao watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah.. Tunakuja mbele zako Yahweh tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu.. Baba tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu BABA utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
“Mtakapoona ‘Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. Kama Bwana asingepunguza siku hizo hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. “Basi mtu akiwaambieni, ‘Tazama, Kristo yupo hapa,’ au ‘Yupo pale,’ msimsadiki. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, kwa ajili ya kuwapotosha wateule wa Mungu kama ikiwezekana. Lakini nyinyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Baba ukabariki ridhiki zetu zote ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
“Basi, siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. Kisha atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba ulinzi wako wakati wote,Baba tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Upendo,amani,utuwema,fadhili,hekima busara na tukapate kutambua/kujitambua,tukachukuliane na kuonyana/kuelimishana kwa upendo.. Baba wa Mbinguni ukatawale katika maisha yetu ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
“Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa wenye njaa,wenye shida/tabu waliokata tamaa ukawape tumaini,walio katika vifungo vya yule mwovu Baba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,wote wakapate uponyaji wa mwili na roho pia,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,ukapokee maombi/sala za watoto wako wanaokuomba kwa imani/kuamini wanaokutafuta kwa bidii bila kuchoka Mungu wetu ukaonekane katika shida/mapito yao,ee Baba tunaomba usikie kulia kwao tunaomba ukawafute machozi yao,Wafiwa ukawe mfariji wao.. Tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi na tunakushuru daima..
“Lakini, juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia na mlinzi wa mlango awe macho. Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. Ninayowaambieni nyinyi, nawaambia wote: Kesheni!”
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele.. Amina..!!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami Mungu aendele kuwabariki na msipungukiwe katika mahitaji yenu na Mungu Baba akawape sawasawa na mapenzi yake Baraka na amani ya Kristo Yesu iwe nanyi daima.. Nawapenda. |