Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 1 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 17...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Ni siku/mwezi Mwingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Tumempa nini Mungu?Tumetenda wema gani?Tumekuwa wazuri sana?
Tumekuwa wenye nguvu/utashi ndiyo maana ametutendea haya?
Tumetenda yote yanayompendeza Mungu?Tumekuwa kiroho?
Hapana si kwamba sisi si wakosaji au wema sana zaidi ya wengine
ambao leo hii hawakuweza kuiona siku hii,na wengine wapo hoi
vitandani hawawezi hata kujigeuza,wengine hawana kauli ya hata kumuita
Mungu na kutubu,Mimi na wewe ni nani na jee tumechukuliaje Neema/rehema hii? kwa maana ni kwa mapenzi yake sisi kuwa hivi
tulivyo leo,Kwake yeye yote yanawezekana,tuwe tayari hatujui
muda wala siku Mwana wa Mungu yuaja...

“Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao! Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”


Asante Baba wa Mbinguni kwa  wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe ee Baba wa Mbinguni,Unastahili
kuabudiwa Jehovah,Unastahili kuheshimiwa Yahweh,Unastahili
kuhimidiwa Mungu wetu,Unatosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako
ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu...!!

Haleluya! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Ni nani awezaye kutaja matendo ya Mwenyezi-Mungu? Ni nani awezaye kumsifu kama anavyostahili? Heri wale wanaotekeleza haki, wanaotenda daima mambo yaliyo sawa. Unikumbuke ee Mwenyezi-Mungu unapowafadhili watu wako; unisaidie wakati unapowaokoa; ili niweze kuona fanaka ya wateule wako, nipate kufurahia furaha ya taifa lako, na kuona fahari pamoja na watu wako.

Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni
siku nyingine Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha,tujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya kwakuwaza,
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua...
Baba wa Mbinguni tunaomba nasi utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe  katika majaribu Baba na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote...
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
tunaomba
  utufunike kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,
mashamba,masomo na yote tunayoenda kufanya/kutenda
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehova nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..

Jishughulishe na biashara hata kama kwa kubahatisha; yawezekana baadaye ukapata chochote kile. Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako, maana, hujui balaa litakalofika duniani. Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha; mti ukiangukia kusini au kaskazini, hapo uangukiapo ndipo ulalapo. Anayengoja upepo hatapanda mbegu, anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu. Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu. Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri. Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho. Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure.


Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyo kupendeza wewe..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na
wote wanaotuzunguka,Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi
wako kwetu na vyote tunavyovimiliki,Yahweh ukatamalaki na kutuatamia
Jehovah ukatupe neema ya kusimamia Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,Baba wa mbinguni tukawe na shauku/kiu
ya kusoma Neno lako,kufuata njia zako na ukatupe neema
ya kukumbushana/kuelimishana kwa upendo,amani katika mioyo yetu,
tuka nene yaliyo yako,tukapate kutambua/kujitambua..

Kisha, nilitoa maagizo kuwa sote tufike karibu na mto Ahava ili tufunge na kujinyenyekeza mbele za Mungu wetu na kumwomba atulinde na kutuongoza katika safari yetu pamoja na watoto wetu. Ingekuwa aibu kubwa kwangu kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapandafarasi wa kutulinda na adui njiani maana nilikuwa nimekwisha mwambia kuwa Mungu wetu huwabariki wote wanaomtafuta, lakini huwachukia na kuwaadhibu wote wanaomwacha. Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu atulinde, naye aliyasikia maombi yetu.

Ee Baba tunaomba upokee sala/maombi yetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu na uponyaji,Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa,
Baba wa Mbinguni ukawatendee na kuwapa maarifa wenye njaa
Jehovah tunaomba ukawafungue walio katika vifungo mbalimbali
vya yule mwovu,Yahweh ukwape tunaini wale wote walikata tamaa..
Baba wa Mbinguni ukawaponye kiro/mwili na ukasikie kulia kwao
Yahweh ukawafute machozi ya watoto wako ukapokee sala/maombi
yao na ukawape neema ya kujiombea,wakasimamie njia zako
Nuru ikaangaze katika maisha yao..
Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako Jehovah..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Amani ikatawale katika maisha yenu,Baraka na upendo,
Na Mungu aendelee kuwatendea katika yote yampendezayo yeye
Nawapenda..

1Watu wa kabila la Manase ambaye alikuwa mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, pia walipewa eneo lao kwa kura. Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase na baba yake Gileadi, alikwishapewa kwa kura miji ya Gileadi na Bashani, maana alikuwa hodari vitani. 2Wengine waliobaki wa kabila la Manase walipewa sehemu yao kwa kura kulingana na koo zao. Koo hizo zilikuwa zile za Abiezeri, Heleki, Asrieli, Shekemu, Heferi na Shemida ambao wote walikuwa wazawa wa kiume wa Manase mwana wa Yosefu.
3Lakini Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na watoto wa kiume, bali alikuwa na watoto wa kike tu, nao walikuwa: Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirza. 4Taz Hes 27:1-7 Mabinti hao wakamjia kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, na viongozi wengine wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose atugawie na sisi sote nchi kama wagawiwavyo wanaume wa kabila letu.” Basi kufuatana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Yoshua akawapatia sehemu yao kama alivyowapa wanaume wa kabila lao. 5Kwa hiyo kabila la Manase liliongezewa sehemu mbili zaidi yaani nchi ya Gileadi na Bashani iliyoko upande mwingine wa mto Yordani, 6kwa sababu binti za Manase waligawiwa sehemu zao kama walivyogawiwa wanaume wa kabila lao. (Nchi ya Gileadi walipewa wazawa wengine wa Manase).
7Eneo la kabila la Manase lilianzia Asheri na kwenda hadi Mikmethathi mashariki ya Shekemu; halafu mpaka wao ukaendelea kusini hadi kwenye nchi ya wakazi wa En-tapua. 8Nchi ya Tapua ilikuwa mali yake Manase, lakini mji wa Tapua, ambao ulikuwa mpakani, ulikuwa mali ya wazawa wa Efraimu. 9Mpaka huo uliendelea hadi kijito cha Kana. Miji iliyokuwa kusini ya Kana ilikuwa ya Waefraimu hata ingawa ilikuwa katika nchi ya kabila la Manase. Halafu mpaka ukapita kaskazini ya kijito Kana na kuishia bahari ya Mediteranea. 10Eneo la kusini lilikuwa la kabila la Efraimu na eneo la kaskazini lilikuwa la kabila la Manase, mpaka wake ukiwa bahari ya Mediteranea kwa upande wa magharibi. Kabila la Asheri lilikuwa kaskazini-magharibi ya eneo la Manase na kaskazini-mashariki lilikuwa kabila la Isakari. 11Vilevile katika nchi ya kabila la Isakari na kabila la Asheri, kabila la Manase lilipatiwa miji ya Beth-sheani na Ibleamu pamoja na vijiji vyake, na miji ya Dori, En-dori, Taanaki na Megido pamoja na wakazi na vijiji vyake; na pia theluthi ya Nafathi.17:11 makala ya Kiebrania si dhahiri. 12Taz Amu 1:27-28 Lakini wazawa wa Manase hawakuweza kuwafukuza wakazi wa miji hiyo, Wakanaani wakaendelea kuishi humo, 13ingawa hata baada ya Waisraeli kuwa na nguvu zaidi, hawakuweza kuwafukuza ila tu waliwafanyisha kazi za kulazimishwa.
14Watu wa kabila la Yosefu walimwendea Yoshua, wakamwambia, “Kwa nini umetugawia sehemu moja tu ya nchi sisi ambao Mwenyezi-Mungu ametubariki hata akatufanya tuwe wengi sana?” 15Yoshua akawajibu, “Kama mmekuwa wengi hivyo, hata nchi ya milima ya Efraimu haiwatoshi tena, basi nendeni msituni katika nchi ya Waperizi na ya Warefai, mkaufyeke msitu huo na kufanya makao yenu huko.” 16Nao wakamjibu, “Ni kweli kwamba nchi hii ya milima haitutoshi; hata hivyo wale Wakanaani wote wanaokaa kwenye tambarare wana magari ya chuma, vilevile wale wote wanaokaa Beth-sheani pamoja na vijiji vyake, na wale wanaoishi katika Bonde la Yezreeli.”
17Basi, Yoshua akawaambia wazawa wa Yosefu, yaani kabila la Efraimu na Manase, “Kweli nyinyi mmekuwa wengi na wenye uwezo mkubwa. Haifai mpate sehemu moja tu, 18bali pia nchi ya milima itakuwa yenu. Ingawa sasa ni msitu, mtaifyeka na kuimiliki yote toka upande huu hadi upande mwingine. Mtawaondoa Wakanaani, hata kama wana magari ya chuma na ni wenye nguvu.”


Yoshua 17;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 31 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 16...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tusalimiane na kukumbushana wema wa Mungu na fadhili zake..

Jee unamkumbuka Ndugu yako katika Kristo katika lipi?
kwa wema wake?kujitoa katika kazi ya Mungu /kanisa?
kujitoa kwa wapendwa wengine ndani na nje ya kanisa?
Hekima,Busara,uvumilivu,upatanishi,uongozi bora,Upendo,ucheshi,
unyenyekevu,amani,ukweli,uimbaji wake? na vingine vingi unaweza kusema ambavyo mimi sikuviweka...

Jee asipokuwepo kunakuwa na pengo,upweke,kupwaya na kuhisi
kunaupungufu kidogo?

Au unamkumbuka Ndugu yako katika Kristo kwa baya lipi?
Makwazo,ugombanishi,uongo,uzushi,ukorofi,kisirani,unafiki?na vingine
vingi unavyoona vibaya ambavyo mimi sikuviweka wewe unaviju..

Jee umechukua hatua gani? Umemsifia kwa mema/mazuri
 anayoyafanya na kumuombea aendelee kusimamia hayo na
Mungu aendelee kumuongoza katika yote yampendezayo?

Jee kwa mabaya pia umechukua hatua gani?
Au unaendeleza nawe ubaya na kusengenya pembeni?
Umejaribu kumshauri hiyo njia siyo?na kumuonya/kumuelisha
kwa upendo,hekima na busara?

Jee unampenda?au unamdanganya na unajidanganya mwenyewe
kwa sababu upendo wa kweli ni kumwambia ukweli naye anaweza
kujirudi hata kama kwa wakati ule alihamaki lakini atajifikiria
na kuchukua hatua....

Ebu tujaribu leo kwa watu 2 wa karibu yako iwe kwa mazuri yao
au mabaya yao,unaweza kufikiri kwamba alikuwa anatenda
vibaya kwa jambo unaloliona wewe lakini kumbe anasababu na anaweza
kukupa sababu ya kufanya hivyo..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tunayoenda kufanya/kutenda,
kunena na tukanene yaliyo yake..
Mungu ni pendo apenda watu...
Nakupenda..
Tuendelee...

Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea. Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia. Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu. Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine. Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao. Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni wa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo. Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu. Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi. Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana. Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku. Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo. Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana. Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia. Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao. Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao. Salimianeni nyinyi kwa nyinyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo.
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuina leo hii..Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwa
nguvu/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa neema/rehema
zako Mungu wetu ni kwa mapenzi yako...

Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachlia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah 
utufunikekwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Ndugu zangu, nawasihi mwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao, maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu. Kila mtu amesikia juu ya utii wenu katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya. Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipateri, wananchi wenzangu, wanawasalimu. Nami Tertio, ninayeandika barua hii, nawasalimuni kwa jina la Bwana. Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu. [ Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.]
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Yahweh tukatende
kama inavyo kupendeza wewe..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na
wote wanaotuzunguka Yahweh tunaomba ulinzi wako,
Baba tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,ukatubariki,
Baba wa Mbinguni tukawe na kiu/shauku ya kujua/kufuata njia zako,
 kusoma Neno lako na likawe taa na Nuru kwenye maisha yetu
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu..
Tukawe barua njema na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tukawe na kiasi...
Ee Baba ukasikie kuomba kwetu na ukapokee maombi/sala zetu..

Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita. Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirishwa kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii. Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina.

Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,walio
katika vifungo mbalimbali,wanaopitia magumu/majaribu,
waliokata tamaa Baba wa Mbinguni ukawape tumaini
Yahweh ukawape neema ya kujiombea,kusimamia njia zako
ukawaguse na mkono wako wenye nguvu Yahweh wakapate
kupona kimwili na kiroho pia,ukawape ubunifu katika kazi,kilimo,
biashara na ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana asanteni kwakuwa pamoja nami
Mungu wa Upendo akadumu katika maisha yenu...
aendelee kuwabariki nanyi mkawe baraka kwa wengine..
Nawapenda.

Nchi ya Efraimu na ya Manase

1Sehemu waliyogawiwa wazawa wa Yosefu kwa kura ilianzia karibu na mto Yordani, mashariki ya chemchemi ya Yeriko, na kupitia jangwani, hadi kwenye sehemu za milima mpaka Betheli. 2Kutoka Betheli mpaka ulielekea Luzu ukapita Atarothi ambako waliishi Waarki. 3Kisha ukashuka magharibi katika nchi ya Wayafleti hadi Beth-horoni ya Chini na Gezeri na kuishia kwenye bahari ya Mediteranea. 4Wazawa wa Yosefu, yaani kabila la Manase na kabila la Efraimu, walipewa nchi hiyo kuwa milki yao.

Nchi ya kabila la Efraimu

5Watu wa kabila la Efraimu kulingana na jamaa zao walipata sehemu yao ambayo mpaka wake upande wa mashariki ulipita Ataroth-adari hadi Beth-horoni ya Juu, 6na kuishia bahari ya Mediteranea. Kwa upande wa kaskazini mpaka ulipita Mikmethathi na kwa mashariki yake ulizunguka na kuelekea Taanath-shilo ambako ulipita upande wa mashariki hadi Yanoa. 7Kutoka Yanoa ulikwenda hadi Atarothi na Naara, hata kufika Yeriko, ambako uliishia katika mto Yordani. 8Kutoka Tapua, mpaka ulikwenda magharibi hadi kijito cha Kana na kuishia bahari ya Mediteranea. Hii ndiyo nchi waliyopewa watu wa kabila la Efraimu kulingana na jamaa zao, 9pamoja na miji na vijiji ambavyo waliongezewa kutoka kwenye nchi ya kabila la Manase. 10Taz Amu 1:29 Waefraimu hawakuwafukuza Wakanaani walioishi Gezeri. Wakanaani hao waliendelea kukaa miongoni mwa watu wa Efraimu mpaka leo, wakiwa watumwa wa kuwafanyia kazi za kulazimishwa.


Yoshua 16;1-10

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 30 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 15...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni wiki/siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na
ametupa kibali chakuendelea kuona leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..

Asante Mungu wetu kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kutuamsha salama na tukiwa
tayari kwa majukumu yetu..

Utukuzwe ee Mwenyezi-Mungu,Utukuzwe ee Mwenyezi-Mungu juu
ya Mbinguni,Utukufu  wako uenee duniani kote..
Utukuzwe ee Mwenyezi-Mungu utufundishe masharti yako..
Utukuzwe ee Mwenyezi-Mungu kwasababu ya nguvu yako!
Tutaimba na kuusifu uwezo wako..
Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu ,Sio sisi, bali wewe peke yako Utukuzwe,
Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako..
Utukuzwe milele na milele ee Mwenyezi-Mungu Mungu wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo,Baba yetu,Muumba wetu,Unatosha Baba wa Mbinguni..


Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake; yajulisheni mataifa mambo aliyotenda! Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu! Jisifieni jina lake takatifu; wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi. Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu; mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima. Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda, miujiza yake na hukumu alizotoa, enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake; Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; hukumu zake zina nguvu duniani kote. Yeye hulishika agano lake milele, hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu. Hushika agano alilofanya na Abrahamu, na ahadi aliyomwapia Isaka. Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, alimhakikishia Israeli agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.”
Sifa na utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu..

Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya Jehovah na
 kesho ni siku nyingine Yahweh..!
Tunakuja mbele zako tukijinyeyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wote
waliotukosea..
Baba wa Mbimnguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..

Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.” Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.” Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.” Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.”

Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
tunaomba utufunike kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na
 Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu na vyote
tunavyoenda kufanya kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..
BABA tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu,Yahweh
ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Mungu wetu tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote
wanaotuzunguka...
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia,Baba tunamba ulinzi wako
Yahweh tunaomba utupe neema ya hekima,busara,utu wema na fadhili..
Jehovah utupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Ee Bwana, tangu vizazi vyote, wewe umekuwa usalama wetu. Kabla ya kuwapo milima, kabla hujauumba ulimwengu; wewe ndiwe Mungu, milele na milele. Wamwambia binadamu, “Rudi mavumbini!” Naye binadamu hurudi mavumbini alimotoka! Kwako miaka elfu ni kama siku moja tu, ni kama jana ambayo imekwisha pita; kwako ni kama mkesha mmoja wa usiku! Wawafutilia mbali watu kama ndoto! Binadamu ni kama nyasi zinazochipua asubuhi: Asubuhi huchipua na kuchanua, jioni zimekwisha nyauka na kukauka. Hasira yako inatuangamiza; tunatishwa na ghadhabu yako. Maovu yetu umeyaweka mbele yako; dhambi zetu za siri ziko wazi mbele yako. Kwa hasira yako maisha yetu yatoweka, yanaisha kama pumzi. Miaka ya kuishi ni sabini, au tukiwa wenye afya, themanini; lakini yote ni shida na taabu! Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara! Nani anayetambua uzito wa hasira yako? Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako? Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima. Urudi, ee Mwenyezi-Mungu! Utakasirika hata lini? Utuonee huruma sisi watumishi wako. Utushibishe fadhili zako asubuhi, tushangilie na kufurahi maisha yetu yote. Utujalie sasa miaka mingi ya furaha, kama ulivyotupa miaka mingi ya shida na taabu. Utuoneshe matendo yako sisi watumishi wako; uwaoneshe wazawa wetu uwezo wako mtukufu. Utufadhili ee Bwana, Mungu wetu; uzitegemeze kazi zetu, uzifanikishe shughuli zetu.
Baba tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
na ukawape uponyaji wa mwili na roho wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa,walio katika
vifungo vya yule mwovu Yahweh tunaomba ukawafungue na wakawe
huru,Baba tazama wenye njaa tunaomba ukawatendee katika
mapito yao,ukabariki mashamba yao,kazi zao,biashara na ukawape
ubunifu katika utendaji wao..Baba ukawape neema ya kujiombea
na kufuata njia zako,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Baba ukapokee sala/maombi ya watoto wako wote wanaokuomba
na kukutafuta kwa bidii,Imani/kuamini Mungu wetu mwenye huruma
tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa
na mapenzi yake..
sina neno zuri la kusema zaidi yakusema..
Nawapenda.

Eneo walilopewa watu wa Yuda

1Eneo la nchi waliyopewa kwa kura watu wa kabila la Yuda kulingana na jamaa zake lilienea tangu kusini-mashariki hadi mpakani mwa Edomu. Sehemu ya kusini kabisa ilikuwa jangwa la Sini. 2Mpaka wao upande wa kusini ulianza pembe ya kusini ya Bahari ya Chumvi, 3ukaendelea kusini hadi mwinuko wa Akrabimu, ukapitia kando ya Sini, na kusini ya Kadesh-barnea, ukipitia Hesroni hadi Adari na kisha ukageuka kuelekea Karka. 4Kutoka hapo ulipita karibu na Asmoni na kufuata kijito cha Misri hadi kufikia kwenye bahari ya Mediteranea. Hapo ndipo ulipopita mpaka wa kusini wa Yuda. 5Mpaka wao wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi hadi pale mto Yordani unapoingilia baharini. Na mpaka wao upande wa kaskazini ulipita kutoka pembe ya Bahari ya Chumvi mahali ambapo mto Yordani unaingilia baharini. 6Mpaka huo ukapita Bethi-hogla na kaskazini ya Beth-araba hadi kwenye jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 7Kutoka hapo, uliendelea hadi Debiri kwenye bonde la Akori na kaskazini kuelekea Gilgali, ulio karibu na mwinuko wa Adumimu ambao uko kusini mwa kijito, kisha ukaelekea kwenye chemchemi za En-shemeshi na kuishia En-rogeli. 8Kisha, mpaka huo ulipitia kwenye Bonde la Hinomu, upande wa kusini mwa kilima cha Wayebusi, yaani Yerusalemu, kuelekea kilele cha mlima ulio magharibi ya bonde la Hinomu na kufika mwishoni mwa bonde la Refaimu. 9Kutoka hapo, ulielekea mlimani hadi chemchemi za Neftoa, mpaka kwenye miji ya mlima wa Efroni. Hapo mpaka uligeuka na kuelekea Baala, yaani Kiriath-yearimu, 10ambako ulipinda magharibi kuelekea Mlima Seiri; ukapita kaskazini ya mlima wa Yerimu, yaani Kesaloni, na kuteremka hadi Beth-shemeshi ambapo ulipita karibu na Timna. 11Kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Ekroni, ukazunguka kuelekea Shikroni ambapo ulipita karibu na mlima Baala hadi Yabneeli ukaishia katika bahari ya Mediteranea. 12Mpaka wa magharibi ulikuwa bahari ya Mediteranea. Ndivyo ilivyokuwa mipaka ya eneo walilopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zao.

Watu wa Kalebu wanamiliki eneo la Hebroni

13 Taz Amu 1:20 Kalebu mwana wa Yefune, alipewa sehemu ya nchi ya Yuda kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Alipewa Kiriath-arba au mji wa Arba ambaye alikuwa babu wa Anaki. Mji huo sasa unaitwa Hebroni. 14Kalebu alizifukuza kutoka mji huo koo tatu za Anaki yaani ukoo wa Sheshai, ukoo wa Ahimani na ukoo wa Talmai. 15Kutoka Hebroni alikwenda kuwashambulia wakazi wa Debiri, mji ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. 16Kalebu akatangaza kwamba atamwoza binti yake Aksa kwa mwanamume yeyote atakayeuteka mji wa Kiriath-seferi. 17Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, akauteka mji huo, naye Kalebu akamwoza bintiye. 18Katika siku yao ya harusi, Aksa alimwambia Othnieli amwombe Kalebu shamba. Aksa alikuwa amepanda punda, na alipokuwa anashuka chini, Kalebu akamwuliza, “Unataka nikupe nini?” 19Aksa akamjibu, “Nipe zawadi; nipe sehemu yenye maji kwa kuwa huko Negebu ulikonipa ni kukavu.” Basi, Kalebu akampa chemchemi za maji zilizokuwa kwenye nyanda za juu na za chini.
20Hii ndiyo nchi waliyopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zake. 21Miji iliyokuwa upande wa kusini kabisa wa nchi ya Yuda kuelekea mpaka wa Edomu ilikuwa: Kabseeli, Ederi, Yaguri, 22Kina, Dimona, Adada, 23Kedeshi, Hazori, Ithnani, 24Zifu, Telemu, Bealothi, 25Hazor-hadata, Kerioth-hezroni (yaani Hazori), 26Amamu, Shema, Molada, 27Hasar-gada, Heshmoni, Beth-peleti, 28Hasar-shuali, Beer-sheba, Biziothia, 29Baala, Iyimu, Ezemu, 30Eltoladi, Kesili, Horma, 31Siklagi, Madmana, Sansana, 32Lebaothi, Shilhimu, Aini na Rimoni. Jumla ya miji waliyopewa ni ishirini na tisa pamoja na vijiji vyake.
33Miji iliyokuwa kwenye tambarare ilikuwa: Eshtaoli, Sora, Ashna, 34Zanoa, Enganimu, Tapua, Enamu, 35Yarmuthi, Adulamu, Soko, Azeka, 36Shaaraimu, Adithaimu, Gedera na Gederothaimu. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na minne pamoja na vijiji vyake.
37Walipewa pia miji ya Senani, Hadasha, Migdal-gadi, 38Dileani, Mizpa, Yoktheeli, 39Lakishi, Boskathi, Egloni, 40Kaboni, Lahmamu, Kithlishi, 41Gederothi, Beth-dagoni, Naama na Makeda. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na sita pamoja na vijiji vyake. 42Tena walipewa miji ya Libna, Etheri, Ashani, 43Yifta, Ashna, Nezibu, 44Keila, Akzibu na Maresha. Jumla ya miji waliyopewa ni tisa pamoja na vijiji vyake. 45Vilevile walipewa Ekroni pamoja na miji yake midogo na vijiji, 46miji yote na vijiji vilivyokuwa karibu na Ashdodi kati ya Ekroni na bahari, 47Ashdodi na Gaza pamoja na miji na vijiji vyake, mpaka kijito cha Misri hadi pwani ya bahari ya Mediteranea.
48Miji iliyokuwa kwenye eneo la milimani ni Shamiri, Yatiri, Soko, 49Dana, Kiriath-sana (yaani Debiri), 50Anabu, Eshtemoa, Animu, 51Gosheni, Holoni na Gilo. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mmoja pamoja na vijiji vyake. 52Walipewa pia miji ya Arabu, Duma, Eshani, 53Yanimu, Beth-tapua, Afeka, 54Humta, Kiriath-arba (yaani Hebroni) na Siori. Jumla ya miji waliyopewa ni tisa pamoja na vijiji vyake. 55Pia walipewa miji ya Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta, 56Yezreeli, Yokdeamu, Zanoa, 57Kaini, Gibea na Timna. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi pamoja na vijiji vyake. 58Vilevile miji ya Halhuli, Beth-suri, Gedori, 59Maarathi, Beth-anothi na Eltekoni. Jumla ya miji waliyopewa ni sita pamoja na vijiji vyake. 60Kadhalika walipewa Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, na Raba. Jumla ya miji waliyopewa ni miwili pamoja na vijiji vyake.
61Miji ya nyikani ilikuwa Beth-araba, Midini, Sekaka, 62Nibshani, Mji wa Chumvi na Engedi. Jumla ya miji waliyopewa ni sita pamoja na vijiji vyake.
63 Taz Amu 1:21; 2Sam 5:6; 1Nya 11:4 Lakini watu wa Yuda hawakuweza kuwafukuza Wayebusi, ambao ndio waliokuwa wenyeji wa Yerusalemu, na mpaka leo Wayebusi bado wanaishi mjini humo pamoja na watu wa Yuda.


Yoshua 15;1-63

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday, 27 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 14...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Asante Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na Mbingu
Asante Mwokozi wetu,Mlinzi wetu,Tunakusifu Mungu wetu,
Tunakuabudu Mungu wetu Mtakatifu,Wewe ni Mungu wetu Milele utakuwa kiongozi wetu,Tukutumikie Mungu wetu na kukutii Mungu wetu,Twakili hakuna mwingine kama wewe Mungu wetu..
Nani aliye Mungu ispokuwa Mungu wetu ?Nani aliye mwamba wa usalama isipokuwa Mungu wetu?
Mungu wetu ndiye Mungu wakutuokoa,Kila ufanyacho ee Mungu nikitakatifu Ni Mungu gani aliye mkuu kama Mungu wetu?
Mwenyezi -Mungu amejaa wema na uaminifu Mungu wetu ni mwenye huruma,Matendeo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu..
Unatosha Baba wa Mbinguni..!!


“Tazameni mtumishi wangu ninayemtegemeza; mteule wangu ambaye moyo wangu umependezwa naye. Nimeiweka roho yangu juu yake, naye atayaletea mataifa haki. Hatalia wala hatapiga kelele, wala hatapaza sauti yake barabarani. Mwanzi uliochubuka hatauvunja, utambi ufukao moshi hatauzima; ataleta haki kwa uaminifu. Yeye hatafifia wala kufa moyo, hata atakapoimarisha haki duniani. Watu wa mbali wanangojea mwongozo wake.”
Asante kwa wema na Fadhili zako wetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii Mungu wetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari katika majukumu yetu

Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu aliyeziumba mbingu, akazitandaza kama hema, yeye aliyeiunda nchi na vyote vilivyomo, yeye awapaye watu waliomo pumzi, na kuwajalia uhai wote waishio humo: “Mimi Mwenyezi-Mungu nimekuita kutenda haki, nimekushika mkono na kukulinda. Kwa njia yako nitaweka ahadi na watu wote, wewe utakuwa mwanga wa mataifa. Utayafumbua macho ya vipofu, utawatoa wafungwa gerezani, waliokaa gizani utawaletea uhuru. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu; utukufu wangu sitampa mwingine, wala sifa zangu sanamu za miungu. Tazama, mambo niliyotabiri yametukia; na sasa natangaza mambo mapya, nakueleza hayo kabla hayajatukia.”
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
 tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Dunia yote iimbe sifa zake: Bahari na vyote vilivyomo, nchi za mbali na wakazi wake; jangwa na miji yake yote ipaaze sauti, vijiji vya wakazi wa Kedari vimsifu, wakazi wa Sela waimbe kwa shangwe; wapaaze sauti kutoka mlimani juu. Wote wakaao nchi za mbali, na wamtukuze na kumsifu Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ajitokeza kama shujaa; kama askari vitani ajikakamua kupigana. Anapaza sauti kubwa ya vita, na kujionesha mwenye nguvu dhidi ya maadui zake.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Yahweh tukatende sawasawa na mapezni yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Jehova tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Jehovah tuyakabidhi maisha yetu mikononi mwako,tunaomba
ukabariki nyumba/ndoa zetu watoto,wazazi wetu,familia/ndugu
na wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba ulinzi wako
Baba tunaomba amani yako ikatawale,Yahweh tunaomba utupe
neema ya kusimamia Neno lako Amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu...
Baba ukatufanye chombo chema nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwa muda mrefu sasa nimenyamaza, nimekaa kimya na kujizuia; lakini sasa nitalia kama mama anayejifungua, anayetweta pamoja na kuhema. Nitaharibu milima na vilima, na majani yote nitayakausha. Mito ya maji nitaigeuza kuwa nchi kavu, na mabwawa ya maji nitayakausha. “Nitawaongoza vipofu katika njia wasiyoifahamu, nitawaongoza katika njia ambazo hawazijui. Mbele yao giza nitaligeuza kuwa mwanga, na mahali pa kuparuza patakuwa laini. Huo ndio mpango wangu wa kufanya, nami nitautekeleza. Wote wanaotegemea sanamu za miungu, wote wanaoziambia: Nyinyi ni miungu yetu; watakomeshwa na kuaibishwa.
Baba wa Mbinguni tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya
yule mwovu na waliokata tamaa na wote walio katika mapito
mbalimbali,Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye
nguvu,ukawape uponyaji wa mwili na roho pia,ukawape neema
ya kukujua wewe,kukutafuta wewe,kufuata njia zako na
wakaweze kujiombea....
  Mungu wetu tunaomba ukapokee sala/maombi
ya watoto wako wanaokutafuta kwa bidii,imani/kuamini..
ee Baba uwainue na kuwapa mwanga kwenye maisha yao..
Asante Baba wa Mbinguni,sifa na utukufu tunakurudishia wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako,Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa katika Bwana nawatakia kila lililo la kheri
Baraka,Amani na Mungu aendelee kuonekana katika maisha yenu
Nawapenda.



Kugawanywa kwa nchi ya Kanaani

1Yafuatayo ni maeneo ya nchi ambayo walipewa Waisraeli katika nchi ya Kanaani. Kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa koo za makabila ya Waisraeli waliwagawia Waisraeli. 2Taz Hes 26:52-56; 34:13 Sehemu yao hiyo waligawiwa kwa kura kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose awape yale makabila tisa na nusu. 3Taz Hes 32:33; 34:14-15; Kumb 3:12-17 Mose alikuwa ameyapa yale makabila mawili na nusu sehemu yao mashariki ya Yordani, lakini Walawi hawakuwa wamepewa sehemu yao pamoja nao. 4Wazawa wa Yosefu walikuwa makabila mawili: Manase na Efraimu. Kabila la Lawi halikupewa sehemu yoyote ya nchi, ila miji tu ya kuishi na sehemu za malisho kwa ajili ya wanyama wao na riziki zao. 5Basi, Waisraeli wakaigawanya nchi kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kalebu anapewa mji wa Hebroni

6 Taz Hes 14:30 Siku moja watu wa kabila la Yuda walimwendea Yoshua huko Gilgali. Kalebu mwana wa Yefune, ambaye alikuwa Mkenizi, akamwambia Yoshua, “Bila shaka unakumbuka jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, mtu wa Mungu, juu yangu na wewe tulipokuwa Kadesh-barnea: 7Taz Hes 13:1-30 Nilipokuwa na umri wa miaka arubaini, Mose mtumishi wa Mungu, alinituma kutoka Kadesh-barnea, kwenda kuipeleleza nchi. Niliporudi nilimletea habari za mambo ya huko kadiri nilivyoamini moyoni mwangu, 8hali wale wenzangu waliokwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo, lakini mimi nilimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kwa uaminifu. 9Taz Hes 14:24 Siku hiyo Mose aliniapia, ‘Hakika sehemu ya nchi ile ambayo ulipita itakuwa yako wewe na wazawa wako milele. Kwa sababu ya uaminifu wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako’. 10Lakini sasa tazama! Ni muda wa miaka arubaini na mitano tangu Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose, wakati Waisraeli walipokuwa wanapitia jangwani. Tangu wakati huo Mwenyezi-Mungu, kama alivyoahidi, amenihifadhi hai mpaka leo, na sasa mimi nina umri wa miaka themanini na mitano. 11Lakini bado nina nguvu kama nilivyokuwa wakati ule Mose aliponituma. Hata sasa nina nguvu za kuweza kupigana vita au kufanya kazi nyingine yoyote. 12Sasa naomba unipe nchi hii ya milima ambayo Mwenyezi-Mungu aliniahidi siku ile. Wewe ulisikia siku ile kwamba Waanaki waliishi humo katika miji yenye ngome; huenda Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.”
13Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune na kumpa mji wa Hebroni kuwa sehemu yake. 14Kwa hiyo, mji wa Hebroni ni sehemu yao wazawa wa Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi mpaka hivi leo, kwa sababu Kalebu alikuwa mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. 15Mji wa Hebroni hapo awali uliitwa Kiriath-arba.14:15 Kiriath-arba: Maana yake mji wa Arba. Arba alikuwa mtu maarufu kuliko wote kati ya Waanaki. Nchi nzima ikawa tulivu bila vita.


Yoshua 14;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Thursday, 26 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 13...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na Mbingu
Muumba wa vyote vilivyopo,vinavyoonekana na visivyo onekana.
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa walio hai
na si Mungu wa wafu,Mungu wa majeshi,Maana wewe si Mungu
wa fujo  ila ni wa amani,Mungu mwokozi,Mungu uponyaye,
kimbilio letu,Matendo yako ni makuu sana,matendo yako ni ya ajabu,
hakuna kama wewe Mungu wetu,enyi Mataifa yote msifuni Mwenyezi-Mungu,Enyi watu wote Mhimidini...!!

Yesu alipokuwa anatoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!” Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.”
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii,si kwamba sisi tumetenda mema sana
si kwa nguvu zetu wala utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo
ni kwa neema/rehema zako Mungu wetu,ni kwa mapenzi yako Jehovah..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Mungu wetu,sifa na utukufu ni wako Baba wa Mbinguni..

Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?” Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, kila mmoja akisema kuwa yeye ni mimi! Nao watawapotosha watu wengi. Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. “Lakini nyinyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, ili mpate kunishuhudia kwao. Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si nyinyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanawe; watoto nao watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.

Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni
siku nyingine Jehovah..
Tunakuja mbele zako Yahweh tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Baba tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu BABA
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona...

“Mtakapoona ‘Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. Kama Bwana asingepunguza siku hizo hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. “Basi mtu akiwaambieni, ‘Tazama, Kristo yupo hapa,’ au ‘Yupo pale,’ msimsadiki. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, kwa ajili ya kuwapotosha wateule wa Mungu kama ikiwezekana. Lakini nyinyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Baba
ukabariki ridhiki zetu zote ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi
tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


“Basi, siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. Kisha atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na
wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba ulinzi wako
wakati wote,Baba tunaomba utupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako Amri na sheria zako siku
zote za maisha yetu,Upendo,amani,utuwema,fadhili,hekima
busara na tukapate kutambua/kujitambua,tukachukuliane
na kuonyana/kuelimishana kwa upendo..
Baba wa Mbinguni ukatawale katika maisha yetu
ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama
 inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

“Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wote wanaopitia
magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa wenye njaa,wenye shida/tabu
waliokata tamaa ukawape tumaini,walio katika vifungo vya yule mwovu
Baba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,wote wakapate uponyaji wa mwili na roho pia,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,ukapokee maombi/sala
za watoto wako wanaokuomba kwa imani/kuamini
wanaokutafuta kwa bidii bila kuchoka Mungu wetu ukaonekane
katika shida/mapito yao,ee Baba tunaomba usikie kulia kwao
 tunaomba ukawafute machozi yao,Wafiwa ukawe mfariji wao..
Tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi na tunakushuru daima..

“Lakini, juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia na mlinzi wa mlango awe macho. Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. Ninayowaambieni nyinyi, nawaambia wote: Kesheni!”

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami
Mungu aendele kuwabariki na msipungukiwe katika mahitaji
yenu na Mungu Baba akawape sawasawa na mapenzi yake
Baraka na amani ya Kristo Yesu iwe nanyi daima..
Nawapenda.

Eneo lililokuwa bado kutwaliwa

1Wakati huu, Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe sasa umekuwa mzee wa miaka mingi, na kumebaki bado sehemu kubwa za nchi ambazo hazijatwaliwa. 2Sehemu hizo ni: Nchi yote ya Wafilisti na nchi yote ya Wageshuri, 3yaani eneo lijulikanalo kama la Wakanaani, kuanzia kijito cha Shihori mpakani mwa Misri hadi eneo la Ekroni huko kaskazini. Maeneo yote ya watawala watano wa Ufilisti: Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni pamoja na eneo la Avi, 4upande wa kusini. Hali kadhalika nchi za Wakanaani kuanzia Ara13:4 kuanzia Ara: Au na Meara. ya Wasidoni mpaka Afeka mpakani mwa Waamori; 5vilevile eneo la Gebali na Lebanoni mashariki ya Baal-gadi chini ya mlima Hermoni mpaka Lebo-hamathi; 6Taz Hes 33:54 pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru. 7Utayagawia nchi hizo makabila tisa na nusu ya kabila la Manase ambayo bado hayajapata kitu.”

Mgawanyo wa mashariki ya Yordani

8 Taz Hes 32:33; Kumb 3:12 Makabila ya Reubeni, Gadi na nusu nyingine ya kabila la Manase yalikuwa yamepewa nchi iliyo mashariki ya mto Yordani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, mtumishi wake. 9Eneo lao lilikuwa kuanzia Aroeri ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ule ulio katikati ya bonde, na nchi ile yote ya tambarare tangu Medeba mpaka Diboni, 10pamoja na miji ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala huko Heshboni hadi mpakani mwa Waamoni, 11pamoja na nchi za Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaakathi, mlima wa Hermoni na nchi yote ya Bashani mpaka Saleka; 12na ufalme wote wa Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala huko Ashtarothi na Edrei katika Bashani. Mose alikuwa amewashinda hao wote na kuwafukuzia mbali. 13Hata hivyo, Wageshuri na Wamaaka hawakufukuzwa bali wanaishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo.
14 Taz Kumb 18:1 Mose hakuwapa watu wa kabila la Lawi nchi yoyote. Bali tambiko walizomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli kwa moto, hizo ndizo zilizokuwa fungu lao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose.
15Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Reubeni kulingana na jamaa zao, 16ilikuwa kuanzia Aroeri kando ya bonde la Arnoni na mji uliokuwa katika bonde hilo pamoja na nchi yote ya tambarare ya Medeba. 17Ilikuwa pia pamoja na Heshboni na miji yake yote iliyo katika sehemu tambarare: Yaani Diboni, Bamoth-baali, Beth-baal-meoni, 18Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, 19Kiriathaimu, Sibma, Sereth-shahari, huko kilimani bondeni, 20Beth-peori, miteremko ya mlima Pisga, Beth-yeshimothi 21na miji yote ya tambarare, nchi yote ya mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alitawala huko Heshboni; Mose alikuwa amemshinda huyu Sihoni pamoja na viongozi wa Midiani, Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, ambao walitawala nchi kwa niaba ya mfalme Sihoni. 22Balaamu, mtabiri, mwana wa Beori ambaye Waisraeli walimuua alikuwa mmoja wao. 23Mpaka wa nchi ya kabila la Reubeni upande wa magharibi ulikuwa mto Yordani. Miji na maeneo yaliyotajwa hapa ndiyo sehemu waliyopewa watu wa koo za kabila la Reubeni.
24Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao 25ilikuwa Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Waamoni hadi Aroeri iliyo mashariki ya Raba, 26vilevile kuanzia Heshboni hadi Ramath-mizpe, Betonimu, na kutoka Mahanaimu mpaka wa Debiri, 27kadhalika miji iliyokuwa katika bonde la Beth-haramu, Beth-nimra, Sukothi na Zafoni na nchi yote iliyokuwa ya mfalme Sihoni wa Heshboni; eneo hilo lilikuwa upande wa mashariki wa Yordani na kupakana na upande wa kusini wa bahari ya Kinerethi. 28Miji na vijiji hivyo ndivyo walivyopewa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao.
29Tena, Mose alikuwa ameipatia nusu ya kabila la Manase kulingana na koo zake, 30eneo la nchi kuanzia Mahanaimu hadi kuingia katika nchi yote iliyokuwa ya mfalme Ogu katika Bashani, pamoja na miji sitini ya Yairi, 31nusu ya Gileadi, Ashtarothi, Edrei, ambayo ilikuwa chini ya himaya ya mfalme Ogu wa Bashani; Eneo hili walipewa nusu ya wazawa wa Makiri mwana wa Manase, kulingana na koo zao.
32Mose alikuwa amewagawia sehemu hizo mbalimbali za nchi iliyokuwa mashariki ya Yeriko na Yordani, wakati alipokuwa kwenye tambarare za Moabu. 33Taz Hes 18:20; Kumb 18:2 Lakini kabila la Lawi, Mose hakulipa sehemu yao ya nchi, maana aliwaambia kwamba sehemu yao itakuwa kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.




Yoshua 13;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.