Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na ametupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii.. Tumshukuru Mungu wetu katika yote.. Utukuzwe Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.. Mungu wa walio hai,Mungu wa yatima,Mungu wa wajane, Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye ezi... Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vote vilivyomo vinavyooneka na visivyooneka..Unastahili sifa,unastahili kuabudiwa,Unastahili kuhimidiwa,Unastahili shukrani,Unatosha baba wa Mbinguni..
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: Wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu.. Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote.. Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. “Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi. Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.
Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako.. Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Yahweh utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akilizetu Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
“Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa. Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. “Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa. “Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika. “Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?
Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu .. Baba wa Mbinguni tunaomba utupe neema ya ubunifu,maarifa katika kufanya/kutenda nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo,Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..
“Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinongonezwa, litangazeni hadharani. Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi.
Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako, Baba tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu, familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwavyote tunavyovimiliki,Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Yahweh nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,upendo ukadumu kati yetu,utu wema,fadhili na vyote vinavyokupendeza wewe..
“Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. “Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa wakapate uponyaji wako,wenye njaa ukawapatie chakula,waliokata tamaa wakapate tumaini lako,waliokatika vifungo vya yule mwovu Baba tunaomba ukawafungue na wakawe huru,ukawape neema ya kujiombea kujua njia zako na wema wako,wakasimamie Neno lako, walioanguka/waliopotea Mungu wetu tunaomba ukawaguse na ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,ukasikie kulia kwao Jehovah ukawafute machozi yao,Baba ukapokee sala/maombi ya watoto wako wanaokutafuta,kukuomba kwa bidii na imani .. Ee Baba tunaomba utusikie..!!
“Anayewapokea nyinyi, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Anayempokea nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayempokea mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hakika hatakosa kamwe kupata tuzo lake.”
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele.. Amina..!
Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami.. Mungu awabariki na kuwainua,msipungukiwe katika mahitaji yenu,Baraka na amani ya Kristo iwe nanyi daima.. Nawapenda. |