Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 21 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 13...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana Tumshukuru katika yote

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa Pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwa nguvu zetu
utashi wetu,Si kwa uwezo wetu na akili zetu sisi kuwa hivi 
tulivyo leo hii ni kwa rehema/neema zako ni kwa mapenzi
yako Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Utukuzwe eeMungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Jehovah,
Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha...
Neema yako yatutosha ee Mungu nwetu...!!

Yesu aliposhuka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata. Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia na kusema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake. Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mapinga Kristo
zishindwe katika jina lililokuu jina la Bwana wetu Yesu Kristo
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.” Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa
zetu,Mungu wetu tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu
na wote wanaotuzunguka,Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa
vyote tunavyovimiliki,Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki vyote
tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba ukavitakase na 
kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu tukawe
salama rohoni Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Yahweh popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni,Jehovah ukatupe neema
ya kutambua mema na mabaya,Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata
njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku
zote za maisha yetu...
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.”

Mungu wetu tazama wenye shida/tabu Yahweh tunaomba ukawaguse
kwa mkono wako wenye nguvu Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa na ukawape tumaini,imani  wanao wauguza Jehovah ukawaponye kimwili na kiroho pia...
Wenye njaa baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki mashamba/vyanzo
vyao wakapate chakula cha kutosha kuweka akiba na kubariki wengine
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wote wanaopitia
magumu/majaribu mbalimbali waliokata tamaa,walio kataliwa,
wenye hofu na mashaka Mungu wetu ukawe tumaini lao
Tazama walio katika vifungo vya yule mwovu walio magerezani
pasipo na hatia Mungu wetu tunaomba ukawafungue na kuwaweka huru
Baba wa Mbinguni haki ikatendeke
Yahweh tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume
nawe,Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata
njia zako nazo zikawaweke huru
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha ya watoto wako
wanaokutafuta kwa bidii na imani Mungu wetu ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbiguni tunaomba ukawafute machozi yao...
Mungu wetu ukawape neema ya kukujua wewe wale wote
wasio amani Mungu wetu ukawape ufahamu na kujitambua
Yahweh ukawahurumie  na kuwaokoa Jehovah ukawatue mizigo
waliyoibeba,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,amani ikatawale
Jehovah tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu nwetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina....!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
vikawe nanyi Daima...
Nawapenda.


Nabii alaani ibada huko Betheli

1Siku moja Yeroboamu alikuwa amesimama kando ya madhabahu ili afukize ubani. Basi, mtu wa Mungu kutoka Yuda akawasili hapo Betheli na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. 2Mtu huyo akailaani ile madhabahu akisema, “Ee madhabahu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Atazaliwa mtoto katika ukoo wa Daudi, jina lake Yosia. Huyo atawatwaa makuhani wanaohudumu mahali pa ibada na kufukiza ubani juu yako, na kutambika juu yako; naam, mifupa ya watu itateketezwa juu yako!’” 3Mtu huyo akatoa ishara siku ileile, akasema: “Hii ndiyo ishara aliyotamka Mwenyezi-Mungu: ‘Madhabahu itabomoka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.’”
4Mfalme Yeroboamu aliposikia maneno hayo ya mtu wa Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono akasema, “Mkamateni huyo!” Na mara huo mkono wake aliounyosha, ukakauka, asiweze tena kuukunja. 5Madhabahu nayo ikabomoka, na majivu yake yakamwagika chini, kama ishara ile aliyoitoa huyo mtu wa Mungu na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. 6Basi, mfalme Yeroboamu akamwambia nabii, “Tafadhali, umsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, uniombee mkono wangu upate kupona.” Naye nabii akamwomba Mwenyezi-Mungu, na mkono wa mfalme ukapona, ukarudia hali yake ya hapo awali. 7Ndipo mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Karibu nyumbani kwangu kula chakula, nami nikupe zawadi.” 8Lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Hata kama ukinipa nusu ya milki yako, sitakwenda pamoja nawe. Sitakula wala kunywa maji mahali hapa, 9kwani Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji, wala nisirudi kwa njia ileile niliyoifuata kuja hapa.” 10Basi, mtu huyo akaenda zake, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

Nabii mzee wa Betheli

11Wakati huo, palikuwa na nabii mmoja mzee huko Betheli. Wanawe wakamwendea, wakamweleza mambo yote aliyotenda yule mtu wa Mungu siku hiyo, huko Betheli; wakamwambia pia yale maneno yule mtu aliyomwambia mfalme Yeroboamu. 12Baba yao akawauliza, “Amefuata njia ipi?” Nao wakamwonesha njia aliyoifuata huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda. 13Naye akawaambia watoto wake, “Nitandikieni huyo punda.” Nao wakamtandikia punda, na mzee akapanda juu yake. 14Akamfuata yule mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mti wa mwaloni. Basi, akamwuliza, “Je, wewe ndiwe yule mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Naye akamjibu, “Naam! Mimi ndiye.” 15Huyo mzee akamwambia, “Karibu nyumbani kwangu, ukale chakula.” 16Lakini yeye akamwambia, “Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia nyumbani kwako. Siwezi kula chakula au kunywa maji mahali hapa, 17maana, Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji mahali hapa, wala nisirudi kwa njia niliyoijia.” 18Huyo mzee wa Betheli akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama wewe, na Mwenyezi-Mungu amenena nami kwa njia ya malaika akisema, ‘Mrudishe nyumbani kwako, ale chakula na kunywa maji.’” Lakini huyo nabii mzee alikuwa anamdanganya tu. 19Basi, mtu wa Mungu akarudi pamoja naye, akala chakula na kunywa maji kwa huyo mzee.
20Walipokuwa mezani, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia huyo nabii mzee, 21naye akamwambia kwa sauti huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda: “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Wewe umeacha kutii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu; wewe hukufuata amri aliyokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. 22Badala yake, umerudi hapa, ukala chakula na kunywa maji mahali hapa ambapo uliambiwa usile chakula wala kunywa maji. Basi, mwili wako hautazikwa kwenye kaburi la babu zako.’” 23Walipomaliza kula, huyo nabii mzee akamtandikia punda huyo mtu wa Mungu, naye akaondoka.
24Alipokuwa anakwenda zake, simba akakutana naye njiani, akamuua; mwili wake ukawa umetupwa hapo barabarani; punda wake na huyo simba wakawa wamesimama kando yake. 25Watu waliopitia hapo na kuiona maiti barabarani, na simba amesimama karibu nayo, wakaenda mpaka mjini alimokuwa anakaa yule nabii, wakawaambia watu. 26Nabii yule ambaye alikuwa amemkaribisha nyumbani kwake aliposikia habari hiyo, akasema, “Huyo ni yuleyule mtu wa Mungu aliyekataa kutii neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu amemtuma simba, akamshambulia na kumwua kama alivyokuwa amemwambia.” 27Hapo akawaambia wanawe “Nitandikie punda.” Nao wakamtandikia. 28Mzee akaenda, akaikuta maiti ya mtu wa Mungu barabarani, simba na punda wake kando yake; huyo simba hakuila maiti wala hakumshambulia punda. 29Basi, huyo nabii mzee akaitwaa maiti ya mtu wa Mungu, akaiweka juu ya punda wake, akairudisha mjini Betheli, kuomboleza kifo chake na kumzika. 30Basi, akamzika katika kaburi lake, naye pamoja na wanawe wakaomboleza kifo chake wakisema, “Aa! Ndugu yangu!” 31Baada ya mazishi, nabii huyo akawaambia wanawe, “Nikifa, nizikeni katika kaburi hilihili alimozikwa mtu wa Mungu; mifupa yangu kando ya mifupa yake. 32Mambo yote aliyoagizwa na Mwenyezi-Mungu dhidi ya madhabahu ya Betheli, na mahali pote pa kutambikia vilimani Samaria, hakika yatatimia.”
33Yeroboamu hakuuacha upotovu wake; aliendelea kuteua watu wa kawaida kuwa makuhani, wahudumie mahali pa kutambikia vilimani. Mtu yeyote aliyejitolea, alimweka wakfu kuwa kuhani wa mahali pa kutambikia huko vilimani. 34Tendo hili likawa dhambi ambayo ilisababisha ukoo wa Yeroboamu ufutiliwe mbali na kuangamizwa.




1Wafalme13;1-34


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 20 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 12...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu, Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...!!
Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Uzima,Muweza wa yote,
Alfa na Omega,Neema yako yatutosha Mungu wetu...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu...


Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake. Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.” Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyatenda
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Mungu wetu utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu. Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu. Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.” Kundi la watu likajiunga likawashambulia; na wale mahakimu wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakaamuru wapigwe viboko. Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali. Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah
ukatupe kama inavyokupendeza wewe.....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,
wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa
vyote tunavyovimiliki Mungu wetu tunaomba
ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba ukabariki
vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu tunaomba
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Jehovah ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh tukawe salama rohoni
Mungu wetu tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya
kusikia sauti yako na kuitii,Baba wa Mbinguni ukatupe neema
ya kutambua mema na mabaya,Jehovah amani yako ikatawale
katika maisha yetu,Upendo ukadumu kati yetu...
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako sikuzote za 
maisha yetu,Jehovah ukaonekane katika maisha yetu popote 
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe....
Roho Mtakatifu ukatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana. Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua. Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.” Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu. Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?” Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.” Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake. Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. [ Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu]. Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, “Wafungueni wale watu.” Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: “Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani.” Lakini Paulo alimjibu, “Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie.” Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa. Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule. Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.


Yahweh tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
walio kata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio kataliwa,
walio katika vifungo vya yule mwovu na walio magerezani pasipo
na hatia,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokwama
kibiashara,wanaotafuta kazi,waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu 
tunaomba ukawasamehe,Yahweh tunaomba ukawaguse kwa makono wako wenye nguvu Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Jehovah ukabariki mashamba yao/vyanzo vyao Mungu wetu ukawape
Ubunifu na maarifa,Yahweh ukawaweke huru na haki ikatendeke
Baba wa Mbinguni ukamtendee kila mmoja na mahitaji yake
Jehovah ukaonekane katika maisha yao,Mungu wetu ukawainue
na kuwaokoa Baba wa Mbinguni ukawape macho ya rohoni
Yahaweh ukawape kutambua/kujitambua Mungu wetu ukawape
Neema ya kufuata njia zako nazo ziwaweke huru,Mungu wetu
ukawape neema ya kujiombea,Amani na Nuru
yako ikaangaze katika maisha yao..
Ee Baba wa Mbinguni tunakuomba ukasikie na ukapokee
sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na 
mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami
Mungu aendelee kuwalinda na kuwabariki katika yote
yanayompendeza yeye,Amani ya Bwana wetuYesu Kristo ikawe nanyi daima..
Nawapenda.


Uasi wa makabila ya kaskazini

(2Nya 10:1-19)

1Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme. 2Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (maana alikuwa bado Misri ambako alikwenda alipomkimbia Solomoni), alirudi kutoka12:2 alirudi kutoka: Kiebrania: Aliishi. Misri. 3Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na jumuiya yote ya Israeli, walimwendea Rehoboamu, wakamwambia, 4“Baba yako alitutwisha mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.” 5Naye Rehoboamu akawaambia, “Nendeni, mrudi kwangu kesho kutwa.” Basi, wakaondoka. 6Baadaye Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake Solomoni, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?” 7Wazee hao wakamjibu, “Leo ukiwa mtumishi wa watu hawa, ukawatumikia na kuongea nao vizuri unapowajibu, hapo watakuwa watumishi wako daima.”
8Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee; badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake. 9Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia niwapunguzie mzigo ambao baba yangu aliwatwika?” 10Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia baba yako aliwatwika mzigo mzito, wakakuomba uwapunguzie mzigo huo, wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu. 11Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”
12Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza. 13Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee, 14akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.”
15Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo.
16Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali, walimwambia,
“Hatuna uhusiano wowote na Daudi!
Hatuna sehemu yetu kutoka kwa huyo mwana wa Yese.
Rudini nyumbani, enyi watu wa Israeli!
Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.”
Hivyo, watu wa Israeli wakarudi makwao. 17Watu wa Israeli waliokuwa wanakaa katika miji ya Yuda, ndio hao tu waliobaki chini ya utawala wa Rehoboamu. 18Mfalme Rehoboamu alipomtuma Adoramu,12:18 Adoramu: Au Adoniramu Taz 1Fal 4:6. aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wote wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Naye Rehoboamu alipanda haraka gari lake la kukokotwa, akakimbilia Yerusalemu. 19Hivyo watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya uasi dhidi ya ukoo wa Daudi mpaka leo.
20Watu wote wa Israeli walipopata habari kwamba Yeroboamu alikuwa amerudi kutoka Misri, walimwita katika mkutano wa hadhara, wakamtawaza kuwa mfalme wa Israeli yote. Hakuna kabila lingine lililojiunga na ukoo wa Daudi isipokuwa tu kabila la Yuda.

Unabii wa Shemaya

(2Nya 11:1-4)

21Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi 180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na utawala wa Israeli, ili aurudishe utawala kwake yeye mwenyewe Rehoboamu, mwana wa Solomoni. 22Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya, mtu wa Mungu: 23“Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda, na watu wote wa kabila la Yuda na Benyamini na watu wengine, 24kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: ‘Msiende, wala msipigane na ndugu zenu, watu wa Israeli. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni mpango wangu.’” Basi, wakaufuata ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani tena, kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza.

Yeroboamu anamwasi Mwenyezi-Mungu

25Baadaye mfalme Yeroboamu akaujenga upya mji wa Shekemu kwenye mlima wa Efraimu; akakaa huko. Kisha akaenda akajenga mji wa Penueli. 26Ndipo Yeroboamu akaanza kufikirifikiri: “Sasa ufalme utarudi kwa jamaa ya mfalme Daudi 27kama watu hawa wataendelea kwenda kutambikia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Mioyo yao itamgeukia bwana wao Rehoboamu mfalme wa Yuda, nao wataniua mimi.”
28Basi, baada ya kushauriana na wengine, akatengeneza sanamu za ndama mbili za dhahabu. Kisha akawaambia watu, “Enyi watu wa Israeli, hii ndiyo miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri! Hakuna sababu ya kwenda Yerusalemu kutambikia huko.” 29Akaweka sanamu moja ya ndama wa dhahabu mjini Betheli, na ya pili mjini Dani. 30Tendo hili likawa dhambi, maana watu waliandamana kwenda kuzitambikia sanamu hizo huko Betheli na Dani.12:30 Huko Betheli na Dani: Kiebrania: Walikwenda moja kwa moja mpaka Dani. 31Vilevile, Yeroboamu alijenga mahali pa kutambikia vilimani, akateua makuhani, watu ambao hawakuwa wa ukoo wa Lawi. 32Yeroboamu pia aliamuru siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane iwe sikukuu sawa na ile sikukuu iliyokuwa inafanyika huko Yuda. Alitoa tambiko kwenye madhabahu aliyotengeneza huko Betheli mbele ya zile sanamu za ndama alizozitengeneza, akaweka wale makuhani aliowateua wahudumu kila mahali pa kutolea tambiko alikotengeneza vilimani. 33Siku hiyo ya kumi na tano ya mwezi wa nane, aliibuni yeye mwenyewe, naye akaenda Betheli kutambikia. Ndivyo alivyoiimarisha sikukuu hiyo aliyoiweka kwa ajili ya watu wa Israeli, naye mwenyewe akapanda kuiendea madhabahu, kufukiza ubani.




1Wafalme12;1-33


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 19 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 11...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki  nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Si kwamba sisi ni wema sana kuliko wengine waliotangulia/kufariki
leo hii,Si kwamba sisi ni wazuri mno,si kwa nguvu zetu wala utashi
wetu,si kwa akili zetu wala uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Asante kwa jinsi tulivyo Mungu wetu ni kwa neema zako tuu..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Baba wa Mbinguni
Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unastahili kuhimidiwa Jehovah
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,Mamtendo yako
yanatisha,Hakuna linaloshindikana mbele zako,Hakuna lililo gumu mbele zako Mungu wetu,Neema yako yatutosha Mungu wetu...


Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Mungu wetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote wealiotukosea
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazaret yeye aliteseka kwanza li sisi tupate
kupona...


Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.” Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza 
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ndoa/nyumba zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tukawe salama rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatupe macho ya kuona,Masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,Yahweh
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba
upo Baba wa Mbinguni,Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya..
Mkono wako wenye nguvu ukaguse maisha yetu
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli. Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa. Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo. Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema. Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.


Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako kila mmoja na
mahitaji yake,Jehovah ukaonekane katika shida zao Mungu wetu ukawaongoze na kuwaokoa Baba wa Mbinguni ukawape neema ya
kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru
Yahweh tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawasimamishe na kuwalinda,Jehovah ukawaponye
kimwili na kiroho pia,Ee Baba tunaomba ukasikie  kuomba kwetu na
ukapoke sala/maombi yetu,Mungu wetu naukawatendee sawasawa na 
mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu na baraka akawaguse kwa mkono wake wenye
nguvu na akawatendee kama inavyompendeza yeye..
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe nanyi daima...
Nawapenda.



Solomoni anamwasi Mungu

1Solomoni alipenda sana wanawake wa kigeni: Binti Farao, wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni, na Wahiti; 2wanawake wa mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza Waisraeli akisema, “Msioe kwao wala wao wasioe kwenu kwa sababu wanawake hao watapotosha mioyo yenu ili muitumikie miungu yao.” Solomoni aliwapenda sana wanawake hao. 3Solomoni akawa na wanawake 700, wote mabinti wa kifalme; na masuria 300. Hao wanawake wakampotosha. 4Maana, alipokuwa mzee, wake zake walimpotosha hata akaitumikia miungu mingine, wala hakuwa mwaminifu kabisa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama baba yake Daudi alivyokuwa mwaminifu. 5Solomoni alimtumikia Ashtarothi aliyekuwa mungu wa kike wa Wasidoni, na alimfuata Milkomu11:5 Milkomu (aya 5) na Moleki (aya 7): Ni majina ya mungu yuleyule. chukizo la Waamoni. 6Hivyo, Solomoni alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wala hakufuata kwa ukamilifu matakwa ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake Daudi alivyokuwa amefanya. 7Juu ya mlima ulio mashariki ya Yerusalemu, Solomoni alijenga mahali pa kumtambikia Kemoshi, chukizo la Wamoabu, na mahali pa kumtambikia Moleki, chukizo la Waamoni. 8Kadhalika, aliwajengea wake zake wote wa kigeni mahali pa kufukizia ubani na kuitambikia miungu yao.
9Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimkasirikia Solomoni, kwa sababu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ingawa yeye alikuwa amemtokea mara mbili, 10na kumwamuru asiiabudu miungu ya kigeni; Solomoni hakutii amri ya Mwenyezi-Mungu. 11Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa umeamua kufanya hivyo, ukavunja agano langu nawe, na kuasi amri zangu nilizokupa, hakika nitakunyanganya huo utawala na kumpa mtumishi wako. 12Hata hivyo, kwa ajili ya baba yako Daudi, sitafanya hivyo maishani mwako, bali nitauondoa utawala huo mikononi mwa mwanao. 13Hata yeye sitamnyanganya milki yote, bali nitamwachia mwanao kabila moja, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu.”

Maadui wa Solomoni

14Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni. 15Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu. 16(Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.) 17Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake. 18Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi. 19Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi. 20Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme.
21Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.” 22Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.”
23Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba. 24Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko. 25Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu.

Ahadi ya Mungu kwa Yeroboamu

26Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme. 27Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi, 28Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu. 29Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani. 30Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili, 31halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’ 32Lakini yeye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu katika makabila yote ya Israeli. 33Nitafanya hivyo kwa sababu Solomoni ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Ashtarothi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi, mungu wa Wamoabu na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomoni ameniasi, ametenda maovu mbele yangu, na wala hakutii sheria zangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya. 34Hata hivyo, sitamnyanganya milki yote, wala sitamwondolea mamlaka maishani mwake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi ambaye nilimchagua, na ambaye alifuata amri zangu na maongozi yangu. 35Lakini, nitamnyanganya mwanawe ufalme huo, nami nitakupatia wewe Yeroboamu makabila kumi. 36Huyo mwanawe Solomoni nitamwachia kabila moja, ili wakati wote mzawa wa mtumishi wangu Daudi awe anatawala Yerusalemu, awe taa inayoangaza daima mbele yangu katika mji ambao nimeuchagua uwe mahali pa kuniabudia. 37Basi, wewe Yeroboamu, nitakufanya kuwa mfalme wa Israeli, nawe utatawala kama upendavyo. 38Na kama utazingatia yote nitakayokuamuru, kama utaishi kulingana na matakwa yangu, kama utatenda mema mbele zangu kwa kushika maongozi yangu na amri zangu, kama mtumishi wangu Daudi alivyofanya, mimi nitakuwa pamoja nawe daima. Na nitakupatia nchi ya Israeli na kuufanya utawala wako uwe thabiti kama nilivyomfanyia Daudi. 39Kutokana na hayo, nitawaadhibu wazawa wa Daudi, lakini si daima.”
40Kwa sababu hiyo, Solomoni alijaribu kumuua Yeroboamu; lakini Yeroboamu akakimbilia Misri kwa Shishaki mfalme wa Misri, akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki.

Kifo cha Solomoni

(2Nya 9:29-31)

41Mambo mengine ya Solomoni, yote aliyotenda na hekima yake, yameandikwa katika Kitabu cha Matendo ya Solomoni. 42Kwa muda wa miaka arubaini, Solomoni aliitawala nchi yote ya Israeli; makao yake yakiwa Yerusalemu. 43Hatimaye, Solomoni alifariki, akazikwa katika mji wa baba yake Daudi. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, akatawala mahali pake.



1Wafalme11;1-43


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.