1“Nimejifunga rasmi mimi mwenyewe,
macho yangu yasimtazame msichana kwa tamaa.
2Au je, nangojea nini kutoka kwa Mungu aliye juu?
Mungu Mwenye Nguvu ameniwekea kitu gani?
3Je, maafa hayawapati watu waovu
na maangamizi wale watendao mabaya?
4Je, Mungu haoni njia zangu,
na kujua hatua zangu zote?
5“Kama nimeishi kwa kufuata uongo,
kama nimekuwa mbioni kudanganya watu,
6Mungu na anipime katika mizani ya haki,
naye ataona kwamba sina hatia.
7Kama hatua zangu zimepotoka,
moyo wangu ukafuata tamaa za macho yangu;
kama mikono yangu imechafuliwa na dhambi,
8jasho langu na liliwe na mtu mwingine,
mazao yangu shambani na yangolewe.
9“Kama moyo wangu umevutwa kwa mke wa mtu,
kama nimenyemelea mlangoni kwa jirani yangu,
10basi, mke wangu na ampikie mume mwingine,
na wanaume wengine wamtumie.
11Jambo hilo ni kosa kuu la jinai,
uovu ambao hakimu lazima atoe adhabu.
12Kosa langu lingekuwa kama moto,
wa kuniteketeza na kuangamiza,
na kuchoma kabisa mapato yangu yote.
13Kama nimekataa kesi ya mtumishi wangu
wa kiume au wa kike,
waliponiletea malalamiko yao,
14nitafanya nini basi Mungu atakaponikabili?
Je, akinichunguza nitamjibu nini?
15Maana Mungu ndiye aliyeniumba mimi na mtumishi wangu;
yeye ndiye aliyetuumba sisi wote.
16 Taz Yobu 4:7-11,16 “Je, nimepata kumnyima maskini mahitaji yake
au kuwafanya wajane watumaini bure?
17Je, nimekula chakula changu peke yangu,
bila kuwaachia yatima nao wapate chochote?
18La! Tangu ujana wangu nimekuwa mlezi wao,
tangu utoto wangu nimewaongoza wajane.
19Je, nilimwona mtu anakufa kwa kukosa nguo,
au maskini ambaye hana nguo ya kuvaa,
20bila kumpa joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu
naye akanitakia baraka za shukrani ya moyo?
21Kama nimenyosha mkono mahakamani dhidi ya yatima,
nikijua nitapendelewa na mahakimu,
22basi, bega langu na lingoke,
mkono wangu na ukwanyuke kiwikoni mwake.
23Maana maafa kutoka kwa Mungu ni kitisho kwangu;
mimi siwezi kuukabili ukuu wake.
24 Taz Sir 31:5-10 “Je, tumaini langu nimeliweka katika dhahabu,
au, nimeiambia dhahabu safi, ‘Wewe ni usalama wangu?’
25Je, nimepata kufurahia wingi wa utajiri wangu
au kujivunia mapato ya mikono yangu?
26Kama nimeliangalia jua likiangaza,
na mwezi ukipita katika uzuri wake,
27na moyo wangu ukashawishika kuviabudu,
nami nikaibusu mikono yangu kwa heshima yake,
28huo pia ungekuwa uovu wa kuadhibiwa na mahakimu
maana ningekuwa mwongo mbele ya Mungu aliye juu.
29“Je, nimefurahia kuangamia kwa adui yangu,
au kufurahi alipopatwa na maafa?
30La! Sikuruhusu kinywa changu kumtakia mabaya,
kwa kumlaani ili afe.
31Watumishi wangu wote wanasema wazi
kila mgeni amekaribishwa nyumbani mwangu.
32Msafiri hakulala nje ya nyumba yangu,
nilimfungulia mlango mpita njia.
33Je nimeficha makosa yangu kama wengine?
Je nimekataa kukiri dhambi zangu?
34Sijaogopa kusimama mbele ya umati wa watu,
wala kukaa kimya au kujifungia ndani,
eti kwa kuogopa kutishwa na dharau zao.
35Laiti angekuwapo mtu wa kunisikiliza!
Naweza kutia sahihi yangu katika kila nilichosema.
Namwambia Mungu Mwenye Nguvu anijibu!
Laiti mashtaka wanayonitolea maadui zangu yangeandikwa!
36Ningeyavaa kwa maringo mabegani
na kujivisha kichwani kama taji.
37Ningemhesabia Mungu kila kitu nilichofanya,
ningemwendea kama mwana wa mfalme.
38Kama nimeiiba ardhi ninayoilima,
nikasababisha mifereji yake iomboleze,
39kwa kufaidika na mazao yake bila kulipa
na kusababisha kifo cha wenyewe,
40basi miiba na iote humo badala ya ngano,
na magugu badala ya shayiri.”
Mwisho wa hoja za Yobu.
Yobu31;1-40
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.