Sala ya mtu anayedhulumiwa
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi)
1Ee Mungu, tega sikio usikie sala yangu;
usiangalie pembeni ninapokuomba.
2Unisikilize na kunijibu;
nimechoshwa na lalamiko langu.
3Nina hofu kwa vitisho vya maadui zangu,
na kwa kudhulumiwa na watu waovu.
Watu waovu wananitaabisha,
kwa hasira wananifanyia uhasama.
4Moyo wangu umejaa hofu,
vitisho vya kifo vimenisonga.
5Natetemeka kwa hofu kubwa,
nimevamiwa na vitisho vikubwa.
6Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa!
Ningeruka mbali na kupata pumziko;
7naam, ningesafiri mbali sana,
na kupata makao jangwani.
8Ningekimbilia mahali pa usalama,
mbali na upepo mkali na dhoruba.
9Ee Bwana, uwaangamize na kuvuruga lugha yao;
maana naona ukatili na ugomvi mjini,
10vikiuzunguka usiku na mchana,
na kuujaza maafa na jinai.
11Uharibifu umeenea pote mjini,
uhasama na udhalimu kila mahali.
12Kama adui yangu angenitukana,
ningeweza kustahimili hayo;
kama mpinzani wangu angenidharau,
ningeweza kujificha mbali naye.
13Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu;
ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!
14Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki;
pamoja tulikwenda nyumbani kwa Mungu.
15Acha kifo kiwafumanie maadui zangu;
washuke chini Kuzimu wangali hai;
maana uovu umewajaa moyoni mwao.55:15 maana … moyoni mwao: Kiebrania: Nyumba zao na mioyo yao vimejaa uovu.
16Lakini mimi namlilia Mungu,
naye Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
17Jioni, asubuhi na adhuhuri, nalalama na kulia,
naye ataisikia sauti yangu.
18Atanikomboa salama katika vita ninayoikabili,
kwa maana maadui zangu ni wengi.
19Mungu atawalaye tangu milele,
atanisikia na kuwaaibisha maadui zangu,
maana hawapendi kujirekebisha,
wala hawamwogopi Mungu.
20Mwenzangu amewashambulia rafiki yake,
amevunja mapatano yake.
21Maneno yake ni laini kuliko siagi,
lakini mawazo yake ni ya kufanya vita.
Maneno yake ni mororo kama mafuta,
lakini yanakata kama upanga mkali.
22Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako,
naye atakutegemeza;
kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
23Wewe, ee Mungu, utawaporomosha shimoni chini kabisa,
watu hao wauaji na wadanganyifu;
hao hawatafikia nusu ya maisha yao.
Lakini mimi nitakutumainia wewe ee Mungu!
Zaburi55;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.