Mungu na watu wake
(Utenzi wa Asafu)
1Sikieni mafundisho yangu, enyi watu wangu;
yategeeni sikio maneno ya kinywa changu.
2 Taz Mat 13:35 Nitasema nanyi kwa mafumbo,
nitasema mambo yaliyofichika tangu kale;
3mambo tuliyoyasikia na kuyajua,
mambo ambayo wazee wetu walitusimulia.
4Hatutawaficha watoto wetu;
ila tutakisimulia kizazi kijacho
matendo matukufu ya Mwenyezi-Mungu na uwezo wake;
tutawaambia maajabu yake aliyotenda.
5Aliwapa wazawa wa Yakobo masharti,
aliweka sheria katika Israeli,
ambayo aliwaamuru wazee wetu
wawafundishe watoto wao;
6ili watu wa kizazi kijacho,
watoto watakaozaliwa baadaye, wazijue,
nao pia wawajulishe watoto wao,
7ili wamwekee Mungu tumaini lao,
wasije wakasahau matendo ya Mungu,
bali wazingatie amri zake.
8Wasiwe kama walivyokuwa wazee wao,
watu wakaidi na waasi;
kizazi ambacho hakikuwa na msimamo thabiti,
ambacho hakikuwa na uaminifu kwa Mungu.
9Watu wa Efraimu, pinde na mishale mkononi,
walirudi nyuma, wakakimbia siku ile ya vita.
10Hawakulizingatia agano la Mungu;
walikataa kufuata sheria yake.
11Walisahau mambo aliyokuwa ametenda,
miujiza aliyokuwa amewaonesha.
12Alifanya maajabu mbele ya wazee wao,
kondeni Soani, nchini Misri.
13Aliigawa bahari, akawapitisha humo;
aliyafanya maji yasimame kama ukuta.
14Mchana aliwaongoza kwa wingu;
usiku kucha kwa mwanga wa moto.
15Aliipasua miamba kule jangwani,
akawanywesha maji kutoka vilindini.
16Alibubujisha vijito kutoka mwambani,
akatiririsha maji kama mito.
17Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu;
walimwasi Mungu Mkuu kule jangwani.
18Walimjaribu Mungu kwa makusudi;
wakidai wapewe chakula walichotaka.
19Walimkufuru Mungu wakisema:
“Je, Mungu aweza kutupa chakula jangwani?
20Ni kweli, aliupiga mwamba,
maji yakabubujika kama mto;
lakini, sasa aweza kweli kutupatia mkate,
na kuwapatia watu wake nyama?”
21Mwenyezi-Mungu, aliposikia hayo,
alijawa na ghadhabu,
moto ukawawakia wazawa wa Yakobo;
hasira yake ikawavamia watu wa Israeli,
22kwa sababu hawakuwa na imani naye,
wala hawakuamini nguvu yake ya kuokoa.
23Hata hivyo aliyaamuru mawingu ya juu,
akaifungua milango ya mbingu;
24 Taz Yoh 6:31 akawanyeshea mana wale,
akawapa nafaka kutoka mbinguni.
25Binadamu, wakala chakula cha malaika;
naye aliwapelekea chakula cha kutosha.
26Alivumisha upepo wa mashariki,
kwa nguvu yake akachochea pepo za kusini;
27akawanyeshea watu wake nyama kama vumbi,
ndege wengi kama mchanga wa pwani;
28ndege hao walianguka kambini mwao,
kila mahali kuzunguka makao yao.
29Watu walikula wakashiba;
Mungu aliwapa walichotaka.
30Lakini hata kabla ya kutosheleza hamu yao,
chakula kikiwa bado mdomoni mwao,
31hasira ya Mungu iliwaka juu yao;
akawaua wenye nguvu miongoni mwao,
na kuwaangusha vijana wa Israeli.
32Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu;
ijapokuwa alitenda maajabu, hawakuamini.
33Basi, akazikatisha siku zao kama pumzi,
miaka yao kwa maafa ya ghafla.
34Kila alipowaua, waliobaki walimgeukia;
walitubu, wakamgeukia Mungu kwa moyo.
35Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa mwamba wao;
Mungu Mkuu alikuwa mkombozi wao.
36Lakini walimdanganya kwa maneno yao;
kila walichomwambia kilikuwa uongo.
37Hawakuambatana naye kwa moyo,
hawakuwa waaminifu kwa agano lake.
38Lakini Mungu mwenye huruma alisamehe uovu wao,
na wala hakuwaangamiza.
Mara nyingi aliizuia hasira yake,
wala hakuiacha ghadhabu yake yote iwake.
39Alikumbuka kwamba wao ni watu tu;
ni kama upepo upitao na kutoweka.
40Mara ngapi walimwasi kule jangwani,
na kumchukiza hukohuko nyikani!
41Walimjaribu Mungu tena na tena,
wakamkasirisha huyo Mtakatifu wa Israeli.
42Hawakuikumbuka nguvu yake,
wala siku ile alipowaokoa na maadui zao,
43alipotenda maajabu nchini Misri,
na miujiza kondeni Soani!
44Aliigeuza ile mito kuwa damu,
Wamisri wasipate maji ya kunywa.
45Aliwapelekea makundi ya nzi waliowasumbua,
na vyura waliowatia hasara.
46Alituma nzige, wakala mavuno yao,
na kuharibu mashamba yao.
47Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe,
na mitini yao kwa baridi kali.
48Ngombe wao aliwaua kwa mvua ya mawe,
na kondoo wao kwa radi.78:48 kwa radi: Au Kwa tauni.
49Aliacha hasira yake kali iwawakie,
ghadhabu, chuki na dhiki,
na kundi la malaika waangamizi.
50Aliachilia hasira yake iendelee,
wala hakuwaepusha na kifo,
bali aliwaangamiza kwa tauni.
51Aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri;
naam, chipukizi wa kwanza kambini mwa Hamu.
52Kisha aliwahamisha watu wake kama kondoo,
akawaongoza jangwani kama kundi la mifugo.
53Aliwaogoza salama, wala hawakuogopa;
lakini bahari iliwafunika maadui zao.
54Aliwaleta katika nchi yake takatifu,
katika mlima aliouteka kwa nguvu yake.
55Aliyafukuza mataifa mbele yao,
akazitoa nchi zao ziwe mali ya Israeli,
akayakalisha makabila ya Israeli mahemani mwao.
56Hata hivyo walimjaribu na kumwasi Mungu Mkuu;
wala hawakuzingatia masharti yake.
57Ila waligeuka na kufanya mabaya kama wazee wao;
wakayumbayumba kama upinde usio imara.
58Walimkasirisha kwa madhabahu zao za miungu;
wakamchochea aone wivu kwa sanamu zao za kuchonga.
59Mungu alipoona hayo, akawaka hasira;
akamkataa Israeli katakata.
60Aliyaacha makao yake kule Shilo,
makao ambamo alikaa kati ya watu.
61Aliiacha ishara ya nguvu yake78:61 ishara ya nguvu yake: Yaani sanduku la agano. itekwe,
utukufu wake utiwe mikononi mwa maadui.
62Aliwakasirikia watu wake mwenyewe;
akawatoa waangamizwe kwa upanga.
63Moto ukawateketeza vijana wao wa kiume,
na wasichana wao wakakosa wachumba.
64Makuhani wao walikufa kwa upanga,
wala wajane wao hawakuomboleza.
65Kisha Bwana aliamka kama kutoka usingizini,
kama shujaa aliyechangamshwa na divai.
66Akawatimua maadui zake;
akawatia aibu ya kudumu milele.
67Lakini aliikataa jamaa ya Yosefu,
wala hakulichagua kabila la Efraimu.
68Ila alilichagua kabila la Yuda,
mlima Siyoni anaoupenda.
69Alijenga hapo hekalu lake kubwa kama mbingu,
kama dunia aliyoiweka imara milele.
70Alimchagua Daudi, mtumishi wake,
akamtoa katika kazi ya kuchunga kondoo.
71Alimtoa katika kazi ya kuchunga kondoo na wanakondoo,
awe na jukumu la kuchunga watu wa Yakobo taifa lake.
Achunge Israeli, watu wake Mungu mwenyewe.
72Daudi akawafunza kwa moyo wake wote,
akawaongoza kwa uhodari mkubwa.
Zaburi78;1-72
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.