Mungu mtawala mkuu
1Mwenyezi-Mungu anatawala!
Furahi, ee dunia!
Furahini enyi visiwa vingi!
2Mawingu na giza nene vyamzunguka;
uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake.
3Moto watangulia mbele yake,
na kuwateketeza maadui zake pande zote.
4Umeme wake wauangaza ulimwengu;
dunia yauona na kutetemeka.
5Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu;
naam, mbele ya Bwana wa dunia yote.
6Mbingu zatangaza uadilifu wake;
na mataifa yote yauona utukufu wake.
7Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa,
naam, wote wanaojisifia miungu duni;
miungu yote husujudu mbele zake.
8Watu wa Siyoni wanafurahi;
watu wa Yuda wanashangilia,
kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu.
9Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote;
wewe watukuka juu ya miungu yote.
10Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu,
huyalinda maisha ya watu wake;
huwaokoa makuchani mwa waovu.
11Mwanga humwangazia mtu mwadilifu,
na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu;
mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu.
Zaburi97;1-12
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.