Yafaa kumsifu Mungu
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu!
Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa.
2Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu;
anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni.
3Anawaponya waliovunjika moyo;
na kuwatibu majeraha yao.
4Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota,
na kuzipa zote majina yao.
5Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi;
maarifa yake hayana kipimo.
6Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu,
lakini huwatupa waovu mavumbini.
7Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani,
mpigieni kinubi Mungu wetu!
8Yeye hulifunika anga kwa mawingu,
huitengenezea nchi mvua,
na kuchipusha nyasi vilimani.
9Huwapa wanyama chakula chao,
na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia.
10Yeye hataki nguvu za farasi,
wala hapendezwi na ushujaa wa askari;
11lakini hupendezwa na watu wamchao,
watu wanaotegemea fadhili zake.
12Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu!
Umsifu Mungu wako, ee Siyoni!
13Maana yeye huimarisha milango yako,
huwabariki watu waliomo ndani yako.
14Huweka amani mipakani mwako;
hukushibisha kwa ngano safi kabisa.
15Yeye hupeleka amri yake duniani,
na neno lake hufikia lengo lake haraka.
16Hutandaza theluji kama pamba,
hutawanya umande kama majivu.
17Huleta mvua ya mawe kama kokoto
na kwa ubaridi wake maji huganda.
18Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka;
huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka.
19Humjulisha Yakobo ujumbe wake,
na Israeli masharti na maagizo yake.
20Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine;
watu wengine hawayajui maagizo yake.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Zaburi147;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.