Mawaidha ya Aguri
1Maneno ya Aguri, mwana wa Yake. Mawaidha ambayo mtu huyu alimwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.30:1 Ithieli, Ukali: Majina hayo yaweza kumaanisha Nimechoka ee Mungu; nimechoka na sina nguvu.
2Mimi ni mpumbavu mno, wala si mtu;
nayo akili ya binadamu sina.
3Sijajifunza hekima,
wala sijui kitu juu ya Mungu Mtakatifu.
4Ni nani aliyepanda juu mbinguni akashuka chini?
Ni nani aliyekamata upepo mkononi?
Ni nani aliyefunga maji katika kitambaa?
Ni nani aliyeiweka mipaka yote ya dunia?
Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe?
Niambie kama wajua!
5Maneno yote ya Mungu ni ya kuaminika;
yeye ni ngao yao wote wanaomkimbilia.
6Usiongeze neno katika maneno yake,
asije akakukemea, nawe ukaonekana mwongo.
7Mambo haya mawili nakuomba ee Mungu,
wala usinikatalie kabla sijafa:
8Uniondolee uongo na udanganyifu;
usinipe umaskini wala utajiri;
unipatie chakula ninachohitaji,
9nisije nikashiba nikakukana;
nikasema, “Mwenyezi-Mungu ni nani?”
Au nisije nikawa maskini nikaiba,
na kulikufuru jina lako ee Mungu wangu.
10Usimchongee mtumwa kwa bwana wake,
asije akakulaani, ukaonekana una hatia.
11Kuna watu ambao huwalaani baba zao,
wala hawana shukrani kwa mama zao.
12Kuna watu ambao hujiona kuwa wema,
kumbe bado hawajatakaswa uchafu wao.
13Kuna na wengine – kiburi ajabu!
Hudharau kila kitu wanachokiona.
14Kuna watu ambao meno yao ni kama upanga,
na magego yao ni kama visu.
Wako tayari kuwatafuna maskini wa nchi,
na wanyonge walio miongoni mwa watu!30:14 Picha tunayopewa hapa yahusu jinsi watu wengine wanavyowakandamiza maskini; Taz pia 12:18; Zab 55:22; 59:8.
Methali za kialfabeti
15Mruba anao binti wawili wasemao, “Nipe, nipe!”
Kuna vitu vitatu ambavyo kamwe havishibi,
naam, vitu vinne visivyosema, “Imetosha!”
16Kuzimu,
tumbo la mwanamke lisilozaa,
ardhi isiyoshiba maji,
na moto usiosema, “Imetosha!”
17Kama mtu akimdhihaki baba yake,
na kudharau utii kwa mama yake,
kunguru wa bondeni watamdonoa macho,
na kuliwa na tai.
18Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu,
naam, mambo manne nisiyoyaelewa:
19Njia ya tai angani,
njia ya nyoka mwambani,
njia ya meli baharini,
na kinachomvuta mwanamume kwa mwanamke.
20Mwenendo wa mwanamke mwasherati ni hivi:
Yeye hula, akajipangusa mdomo,
na kusema, “Sijafanya kosa lolote!”
21Kuna mambo matatu ambayo huitetemesha dunia,
naam, mambo manne ambayo haiwezi kuyastahimili:
22Mtumwa anayekuwa mfalme;
mpumbavu anayeshiba chakula;
23mwanamke asiyependwa anayeolewa;
na mjakazi achukuapo nafasi ya bibi yake.
24Kuna viumbe vinne vidogo sana duniani,
lakini vina akili sana:
25Sisimizi: Wadudu wasio na nguvu,
lakini hujihifadhia chakula wakati wa kiangazi;
26pelele: Wanyama wasio na uwezo,
lakini hujitengenezea makao miambani;
27nzige: Hawana mfalme,
lakini wote huenda pamoja kwa vikosi;
28mjusi: Waweza kumshika mkononi,
lakini huingia katika ikulu.
29Kuna viumbe vitatu vyenye mwendo wa kupendeza,
naam, kuna viumbe vinne vyenye mwendo mzuri;
30simba: Mnyama mwenye nguvu kuliko wote,
wala hamwogopi mnyama mwingine yeyote;
31jogoo aendaye kwa maringo;
tena beberu;
na mfalme mbele ya watu wake.
32Kama umekuwa mpumbavu hata ukajisifu,
au kama umekuwa unapanga maovu,
chunga mdomo wako.
33Maana ukisukasuka maziwa utapata siagi,
ukimpiga mtu pua atatoka damu;
kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.
Methali30;1-33
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.