Mungu amepanga kila kitu
1Kila kitu kina majira yake,
kila jambo duniani lina wakati wake:
2Wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa;
wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna kilichopandwa;
3wakati wa kuua na wakati wa kuponya;
wakati wa kubomoa na wakati wa kujenga;
4wakati wa kulia na wakati wa kucheka;
wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza;
5wakati wa kutupa mawe na wakati wa kuyakusanya mawe pamoja;
wakati wa kukumbatia na wakati wa kuacha kukumbatia;
6wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza;
wakati wa kuhifadhi na wakati wa kutupa;
7wakati wa kurarua na wakati wa kushona;
wakati wa kukaa kimya na wakati wa kuongea;
8wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia;
wakati wa vita na wakati wa amani.
9Mfanyakazi hufaidi nini kutokana na juhudi zake hizo? 10Mimi nimeiona kazi ambayo binadamu amepewa na Mungu. 11Mungu amekifanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Amempa binadamu hamu ya kujua mambo ya baadaye, lakini hajamjalia fursa ya kuelewa matendo yake Mungu tangu mwanzo mpaka mwisho. 12Najua kwamba, kwa binadamu, liko jambo moja tu la kumfaa; kufurahi na kujifurahisha muda wote aishipo. 13Sote inatupasa kula na kunywa na kufurahia matunda ya kazi zetu. Hayo ni majaliwa ya Mungu.
14Najua kwamba lolote atendalo Mungu linadumu milele. Hakuna kinachoweza kuongezwa wala kupunguzwa; Mungu amefanya mambo yawe hivyo kusudi wanadamu wamche yeye. 15Kinachotukia sasa, kilikwisha tukia; kitakachotukia baadaye kilikwisha tukia; na Mungu hukifanya kitu kilekile kitukie tena na tena.
Ukosefu wa uadilifu duniani
16Zaidi ya hayo, nimegundua duniani kwamba, mahali pa haki na uadilifu, uovu unatawala. 17Basi, nikasema moyoni mwangu, “Haidhuru! Mungu atawahukumu waadilifu, hali kadhalika na waovu, maana amepanga wakati maalumu kwa kila jambo na kwa kila kazi.” 18Nikasema moyoni mwangu, “Mungu anawajaribu binadamu, ili kuwaonesha kwamba wao ni sawa tu na wanyama.” 19Mwisho wa binadamu na mwisho wa mnyama ni uleule. Jinsi anavyokufa binadamu ndivyo anavyokufa mnyama. Wote hupumua namna ileile; binadamu si bora kuliko mnyama. Kwao yote ni bure kabisa. 20Wote hufa na kwenda mahali pamoja. Wote wametoka mavumbini; na wote watarudi mavumbini, 21Nani ajuaye, basi, kama kweli roho ya mtu hupaa juu, na roho ya mnyama hudidimia chini ardhini? 22Ndipo nikatambua kwamba hakuna jambo lililo bora zaidi kwa binadamu kufanya kuliko kufurahia kazi yake, kwa sababu amepangiwa hivyo. Nani awezaye kumjulisha binadamu yale yatakayokuwa baada ya kufa kwake?
Mhubiri3;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.