Mungu ataiadhibu Babuloni
1 13:1--14:23 Taz Isa 47:1-15; Yer 50:1--51:64
Kauli ya Mungu dhidi ya Babuloni ambayo Isaya, mwana wa Amozi, alipewa katika maono:
2Mungu asema:
“Twekeni bendera juu ya mlima usio na miti.
Wapaazieni sauti askari
wapungieni watu mkono
waingie malango ya mji wa wakuu.
3Mimi nimewaamuru wateule wangu,
nimewaita mashujaa wangu,
hao wenye kunitukuza wakishangilia,
waje kutekeleza lengo la hasira yangu.”
4Sikilizeni kelele milimani
kama za kundi kubwa la watu!
Sikilizeni kelele za falme,
na mataifa yanayokusanyika!
Mwenyezi-Mungu wa majeshi
analikagua jeshi linalokwenda vitani.
5Wanakuja kutoka nchi za mbali,
wanatoka hata miisho ya dunia:
Mwenyezi-Mungu na silaha za hasira yake
anakuja kuiangamiza dunia.
6 13:6 Taz Yoe 1:15 Lieni maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia;
inakuja kama maafa kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu.
7Kwa hiyo mikono ya kila mtu italegea,
kila mtu atakufa moyo.
8Watu watafadhaika,
watashikwa na hofu na maumivu,
watakuwa na uchungu kama mama anayejifungua.
Watatazamana kwa mashaka,
nyuso zao zitawaiva kwa haya.
9Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,
siku kali, ya ghadhabu na hasira kali.
Itaifanya nchi kuwa uharibifu,
itawaangamiza wenye dhambi wake.
10 13:10 Taz Eze 32:7; Mat 24:29; Marko 13:24-25; Luka 21:25; Ufu 6:12-13 Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza;
jua linapochomoza litakuwa giza,
na mwezi hautatoa mwanga wake.
11Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitauadhibu ulimwengu kwa uovu wake,
waovu kwa sababu ya makosa yao.
Nitakikomesha kiburi cha wenye majivuno,
na kuporomosha ubaradhuli wa watu katili.
12Nitawafanya watu kuwa wachache kuliko dhahabu safi;
binadamu watakuwa wachache kuliko dhahabu ya Ofiri.
13Nitazitetemesha mbingu
nayo nchi itatikisika katika misingi yake
kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu
siku ile ya hasira yangu kali.
14“Kama swala anayewindwa,
kama kondoo wasio na mchungaji,
kila mmoja atajiunga na watu wake
kila mtu atakimbilia nchini mwake.
15Yeyote atakayeonekana atatumbuliwa,
atakayekamatwa atauawa kwa upanga.
16Watoto wao wachanga watapondwapondwa mbele yao,
watanyanganywa nyumba zao,
na wake zao watanajisiwa.
17“Ninawachochea Wamedi dhidi yao;
watu ambao hawajali fedha
wala hawavutiwi na dhahabu.
18Mishale yao itawaua vijana,
hawatakuwa na huruma kwa watoto,
wala kuwahurumia watoto wachanga.
19 13:19 Taz Mwa 19:24 Babuloni johari ya falme zote
na umaarufu wa kiburi cha Wakaldayo
utakuwa kama Sodoma na Gomora,
wakati Mungu alipoiangamiza.
20Kamwe hautakaliwa tena na watu,
watu hawataishi humo katika vizazi vyote.
Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake humo,
wala mchungaji atakayechunga wanyama wake humo.
21 13:21 Taz Isa 34:14; Sef 2:14; Ufu 18:2 Badala yake watakuwamo wanyama wakali wa porini,
bundi watajaa katika nyumba zake.
Mbuni13:21 Mbuni: Au pepo wabaya. wataishi humo,
na majini13:21 majini: Au Ibilisi; namna ya pepo wa hadithi za Babuloni. yatachezea humo.
22Mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake,
mbweha wataonekana ndani ya nyumba zao za anasa.
Wakati wa Babuloni umekaribia,
wala siku zake hazitaongezwa.”
Isaya13;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.