Mwenyezi-Mungu ataiadhibu dunia
1Sasa Mwenyezi-Mungu anaiharibu dunia
na kuifanya tupu.
Atausokota uso wa dunia
na kuwatawanya wakazi wake.
2Kila mtu atapatwa na mambo yaleyale:
Mtu wa kawaida na kuhani;
mtumwa na bwana wake;
mjakazi na bibi yake;
mnunuzi na mwuzaji;
mkopeshaji na mkopaji;
mdai na mdaiwa.
3Dunia itaharibiwa kabisa na kuangamizwa;
Mwenyezi-Mungu ametamka hayo.
4Dunia inakauka na kunyauka;
ulimwengu unafadhaika na kunyauka;
mbingu zinafadhaika pamoja na dunia.
5Watu wameitia najisi dunia
maana wamezivunja sheria za Mungu,
wamezikiuka kanuni zake,
wamelivunja agano lake la milele.
6Kwa sababu hiyo laana inaitokomeza dunia,
wakazi wake wanateseka kwa makosa yao.
Wakazi wa dunia wamepungua,
ni watu wachache tu waliosalia.
7Mizabibu inanyauka,
divai inakosekana.
Wote waliokuwa wenye furaha
sasa wanasononeka kwa huzuni.
8Mdundo wa vigoma umekoma,
nderemo na vifijo vimetoweka;
midundo ya vinubi imekomeshwa.
9Hakuna tena kunywa divai na kuimba;
mvinyo umekuwa mchungu kwa wanywaji.
10Mji uliohamwa umejaa uharibifu;
kila nyumba imefungwa asiingie mtu.
11Kuna kilio barabarani kwa kukosa divai;
shangwe yote imekoma,
furaha imetoweka duniani.
12Mji ni magofu matupu;
malango yake yamevunjwavunjwa.
13Kama vile zeituni chache tu juu ya mzeituni
au tini chache tu juu ya mtini
baada ya kumaliza mavuno,
ndivyo itakavyokuwa katika nchi zote:
Watu wachache watabakia hai.
14Watakaosalia watapaza sauti,
wataimba kwa shangwe.
Kutoka magharibi watatangaza ukuu wa Mwenyezi-Mungu,
15nao wakazi wa mashariki watamsifu.
Watu wa mbali watalisifu
jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
16Tunasikia nyimbo za sifa kutoka miisho ya dunia,
nyimbo za kumsifu Mungu aliye mwadilifu.
Lakini mimi ninanyongonyea,
naam, ninanyongonyea.
Ole wangu mimi!
Wasaliti wanaendelea kuwa wasaliti,
usaliti wao unazidi kuwa mbaya zaidi.
17Hofu, mashimo na mitego,
hivi ndivyo vinavyowangojeni enyi wakazi wa dunia.
18Atakayeikimbia hofu atatumbukia shimoni;
atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni.
Madirisha ya mbinguni24:18 Madirisha ya mbinguni: Yaani tufani au gharika, Taz Mwa 7:11; 8:2. yamefunguliwa,
misingi ya dunia inatikisika.
19Dunia inavunjikavunjika,
inapasuka na kutikiswatikiswa.
20Inapepesuka kama mlevi,
inayumbayumba kama kibanda.
Imelemewa na mzigo wa dhambi zake
nayo itaanguka wala haitainuka tena.
21Siku ile Mwenyezi-Mungu ataliadhibu jeshi la angani24:21 jeshi la angani: Yaani jua, mwezi na nyota ambavyo baadhi ya watu wa nyakati hizo walifikiri kuwa pepo wabaya.
kadhalika na wafalme wa duniani.
22Wote watakusanywa kama wafungwa shimoni;
watafungwa gerezani pamoja kwa miaka mingi,
na baada ya muda huo atawaadhibu.
23Kisha mwezi utaaibishwa,
nalo jua litaona aibu kuangaza,
kwa kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi
atatawala huko Yerusalemu katika mlima Siyoni;
ataonesha wazee wa watu wake utukufu wake.
Isaya24;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.