Onyo kwa ufalme wa kaskazini
1Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu,
fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka!
Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba;
na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia!
2Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu,
ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali,
kama tufani ya mafuriko makubwa;
kwa mkono wake atawatupa chini ardhini.
3Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu
yatakanyagwakanyagwa ardhini,
4fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka;
fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba
itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi;
mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja.
5Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu,
kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai.
6Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki,
nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
Isaya na manabii walevi wa Yuda
7Lakini wako wengine waliolewa divai
na kuyumbayumba kwa sababu ya pombe;
naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo,
wamevurugika kwa divai.
Wanayumbayumba kwa pombe kali;
maono yao yamepotoka,
wanapepesuka katika kutoa hukumu.
8Meza zote zimetapakaa matapishi,
hakuna mahali popote palipo safi.
9Wao wananidhihaki na kuuliza:
“Huyu nabii ataka kumfundisha nani?
Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake?
Je, sisi ni watoto wachanga
walioachishwa kunyonya juzijuzi?
10Anatufundisha kama watoto wadogo:
Sheria baada ya sheria,
mstari baada ya mstari;
mara hiki, mara kile!”
11 28:11-12 Taz 1Kor 14:21 Haya basi!
Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa
kwa njia ya watu wa lugha tofauti
wanaoongea lugha ngeni.
12Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi:
“Nitawaonesheni pumziko,
nitawapeni pumziko enyi mliochoka.
Hapa ni mahali pa pumziko.”
Lakini wao hawakutaka kunisikiliza.
13Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu:
Sheria sheria, mstari mstari;
mara hiki, mara kile!
Nao watalazimika kukimbia
lakini wataanguka nyuma;
watavunjika, watanaswa na kutekwa.
Jiwe la msingi Siyoni
14Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,
enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu,
15“Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo,
mmefanya mapatano na Kuzimu!
Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata,
kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu,
na udanganyifu kuwa kinga yenu!”
16 28:16 Taz Zab 118:22-23; Rom 9:33; 10:11; 1Pet 2:6 Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu:
“Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi,
jiwe ambalo limethibitika.
Jiwe la pembeni, la thamani,
jiwe ambalo ni la msingi thabiti;
jiwe lililo na maandishi haya:
‘Anayeamini hatatishika.’
17Nitatumia haki kama kipimo changu,
nitatumia uadilifu kupimia.”
Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea,
na mafuriko yataharibu kinga yenu.
18Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa,
na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa.
Janga lile kuu litakapokuja
litawaangusheni chini.
19Kila litakapopitia kwenu litawakumba;
nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku.
Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho.
20Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno,
au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno!
21 28:21 Taz Yos 10:10-12; 2Sam 5:20; 1Nya 14:11 Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu;
atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni.
Atatekeleza mpango wake wa ajabu;
atatenda kazi yake ya kustaajabisha.
22Basi, nyinyi msiwe na madharau
vifungo vyenu visije vikakazwa zaidi.
Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi
ameazimia kuiangamiza nchi yote.
Hekima ya Mungu
23Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni;
sikilizeni kwa makini hotuba yangu.
24Je, alimaye ili kupanda hulima tu?
Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake?
25La! Akisha lisawazisha shamba lake,
hupanda mbegu za bizari na jira,
akapanda ngano na shayiri katika safu,
na mipakani mwa shamba mimea mingineyo.
26Mtu huyo huwa anajua la kufanya,
kwa sababu Mungu wake humfundisha.
27Bizari haipurwi kwa mtarimbo
wala jira kwa gari la ng'ombe!
Ila bizari hupurwa kwa kijiti
na jira kwa fimbo.
28Mkulima apurapo ngano yake,
haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake.
Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu,
bila kuziharibu punje za ngano.
29Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Mipango yake Mungu ni ya ajabu,
hekima yake ni kamilifu kabisa.
Isaya28;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.