Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu pekee
1“Sikiliza ewe taifa Israeli mtumishi wangu;
sikiliza ewe kizazi cha Yakobo mteule wangu.
2Mimi, Mwenyezi-Mungu Muumba wako,
niliyekufanya tangu tumboni mwa mama yako,
nimekuja kukusaidia wewe.
Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:
Usiogope, ewe taifa la Yakobo, mtumishi wangu,
naam, usiogope ewe Yeshuruni mteule wangu.
3“Nitaimwagilia maji nchi iliyokauka,
na kutiririsha mto katika nchi kame.
Nitawamiminia roho yangu wazawa wako,
nitawamwagia watoto wako baraka yangu.
4Watachipua kama nyasi penye maji mengi,
kama majani kandokando ya vijito.
5“Mmoja atasema: ‘Mimi ni wa Mwenyezi-Mungu’,
mwingine atajiita kwa jina la Yakobo,
mwingine ataandika mkononi mwake, ‘Wa Mwenyezi-Mungu’,
na kujitambulisha kwa jina la Israeli.”
6Mwenyezi-Mungu, Mfalme na Mkombozi wa Israeli,
naam, Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Mimi ni wa kwanza na wa mwisho;
hakuna Mungu mwingine ila mimi.
7Ni nani Mungu aliye kama mimi?
Mwache atangaze na kusema wazi mbele yangu.
Nani alitangaza hapo kale mambo ambayo yatatukia?
Na watuambie yale ambayo bado kutokea.44:7 aya ya 7 Kiebrania si dhahiri.
8Enyi watu wangu, msiogope wala msiwe na hofu,
Je, sikuwaambia tangu zamani mambo yatakayotokea?
Nyinyi ni mashahidi wangu.
Je, yuko Mungu mwingine ila mimi?
Je, kuna mwenye nguvu mwingine?
Huyo simjui!”
Upumbavu wa kuabudu sanamu
9Watu wote wanaotengeneza sanamu za miungu ni bure kabisa; na vitu hivyo wanavyovifurahia haviwafai chochote. Wanaoshuhudia hiyo miungu ya uongo ni vipofu na wajinga. Kwa hiyo hao wataaibishwa! 10Ajabu ya mtu kutengeneza sanamu au kinyago cha mungu ambaye hawezi kumsaidia chochote! 11Hakika wote wanaomheshimu wataaibishwa, tena hao mafundi wa sanamu ni binadamu tu. Basi, wakutane wote, wajitokeze, nao watatishika na kuaibishwa.
12Mfuachuma huchukua madini, akayayeyusha motoni na kufua sanamu. Huigongagonga kwa nyundo ili kuipa umbo kwa mikono yake yenye nguvu. Wakati wote huo yeye huona njaa na kuchoka; huona kiu na nguvu kumwishia. 13Kadhalika naye seremala hupima kipande cha mbao, akakitia alama kwa kalamu yake, kisha kwa vifaa vyake hukichonga na kukipa umbo la binadamu na sura ya kupendeza; kisha akaiweka sanamu hiyo ya mungu mahali pake pa pekee. 14Mtu hukata mti wa mwerezi ili autumie, au huchagua mberoshi au mwaloni. Huuacha ukue kati ya miti ya msituni. Au hupanda mwerezi na mvua huustawisha. 15Sehemu ya mti huo itatumiwa kama kuni; mtu huota moto wake na kuoka mikate yake juu yake. Sehemu nyingine ya mti huohuo, mtu hujichongea sanamu ya mungu, akainakshi, halafu akaiabudu. 16Kisha huchukua kuni zake akaoka nazo moto, akachoma nyama juu yake, akala, akashiba. Halafu hukaa hapo akiota moto na kusema, “Naam! Ama kweli nimepata joto! Huo ndio moto!” 17Sehemu iliyobaki ya mti huohuo, hujichongea sanamu ya mungu, kinyago chake, kisha huisujudia na kuiabudu. Huiomba akisema, “Wewe ni mungu wangu, niokoe!”
18Watu hao hawajui wala hawaelewi kitu chochote. Wamefumbwa macho wasiweze kuona; kadhalika na akili zao wasiweze kufahamu. 19Hakuna awezaye kutafakari; au kuwa na akili na kufikiri na kusema: “Nusu ya mti huo niliwashia moto; tena nikaoka mikate juu ya makaa yake, nikachoma nyama, nikala. Je, sehemu iliyobaki nitatengeneza sanamu ambayo ni chukizo na kukisujudia hicho kipande cha mti?”
20La! Fikira zake zimeambatana na hicho ambacho ni majivu tu! Mtu huyo amepotoka hata hawezi kujiokoa mwenyewe na kusema: “Kweli ninachoshika mkononi ni udanganyifu mtupu!”
Mwenyezi-Mungu, hatawasahau Waisraeli
21Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Ewe taifa la Yakobo kumbuka;
naam, kumbuka ewe Israeli:
Wewe ni mtumishi wangu.
Nilikuumba ili uwe mtumishi wangu,
nami kamwe sitakusahau.
22Nimeyafagilia mbali makosa yako kama wingu,
nimezifanya dhambi zako zitoweke kama ukungu.
Rudi kwangu maana mimi nimekukomboa.”
23Imbeni kwa furaha enyi mbingu,
kwa sababu ya hayo aliyotenda Mwenyezi-Mungu.
Pazeni sauti enyi vilindi vya dunia!
Imbeni kwa furaha enyi milima!
Enyi misitu na miti yote iliyomo, imbeni.
Maana Mwenyezi-Mungu amewakomboa wazawa wa Yakobo,
naye atatukuka katika nchi ya Israeli.
24Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wako,
aliyekuumba tangu tumboni mwa mama yako, asema:
“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyeumba vitu vyote.
Mimi peke yangu nilizitandaza mbingu,
niliiumba dunia kwa nguvu yangu mwenyewe!
25 44:25 Taz 1Kor 1:20 Mimi huzivuruga ishara za watabiri waongo
na kuwapumbaza waaguzi.
Mimi huyakanusha maneno ya wenye hekima
na kufanya ujuzi wao kuwa upumbavu.
26Lakini huuthibitisha ujumbe wa mtumishi wangu,
na kukamilisha maaguzi ya wajumbe wangu.
Mimi ndimi niuambiaye mji wa Yerusalemu:
Wewe Yerusalemu, utakaliwa tena na watu.
Na miji ya Yuda:
Nyinyi mtajengeka tena:
Magofu yenu nitayarekebisha tena.
27Mimi ndimi ninayeviamuru vilindi:
Kaukeni.
28Ndimi nimwambiaye Koreshi:
Wewe utawachunga watu kwa niaba yangu.
Wewe utatekeleza mipango yangu yote.
Ndimi ninayesema kuhusu Yerusalemu:
Wewe Yerusalemu utajengwa tena upya;
na juu ya hekalu: Msingi wako utawekwa tena.”
Isaya44;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.