Israeli: Mwanga wa mataifa
1Nisikilizeni, enyi nchi za mbali,
tegeni sikio, enyi watu wa mbali!
Mwenyezi-Mungu aliniita kabla sijazaliwa,
alitaja jina langu nikiwa tumboni mwa mama yangu.
2Aliyapa ukali maneno yangu kama upanga mkali,
alinificha katika kivuli cha mkono wake;
aliufanya ujumbe wangu mkali kama ncha ya mshale,
akanificha katika podo lake.
3Aliniambia, “Wewe ni mtumishi wangu;
kwako, Israeli, watu watanitukuza.”
4Lakini mimi nikafikiri,
“Nimeshughulika bure,
nimetumia nguvu zangu bure kabisa.”
Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu atanipa haki yangu;
tuzo la kazi yangu liko kwa Mungu.
5Lakini asema sasa Mwenyezi-Mungu,
ambaye aliniita tangu tumboni mwa mama yangu
ili nipate kuwa mtumishi wake;
nilirudishe taifa la Yakobo kwake,
niwakusanye wazawa wa Israeli kwake.
Mwenyezi-Mungu amenijalia heshima mbele yake.
Mungu wangu amekuwa ndiye nguvu yangu.
6Yeye asema: “Haitoshi tu wewe kuwa mtumishi wangu,
uyainue makabila ya Yakobo,
na kurekebisha watu wa Israeli waliobaki.
Nitakufanya uwe mwanga wa mataifa,
niwaletee wokovu watu wote duniani.”49:6 sehemu hii imekaririwa katika Mate 13:47, 26:23. Luka naye anaigusia katika 2:32; Taz pia Isa 42:6.
7Mwenyezi-Mungu, Mkombozi na Mtakatifu wa Israeli,
amwambia hivi yule anayedharauliwa mno,
yule anayechukiwa na mataifa,
na ambaye ni mtumishi wa watawala:
“Wafalme watakuona nao watasimama kwa heshima,
naam, wakuu watainama na kukusujudia
kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu
ambaye hutimiza ahadi zangu;
kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli
ambaye nimekuteua wewe.”
Kujengwa upya kwa Yerusalemu
8Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wakati wa kufaa nilikujibu ombi lako;
wakati wa wokovu nilikusaidia.
Nimekuweka na kukufanya
uwe kiungo cha agano langu na mataifa yote:
Kuirekebisha nchi iliyoharibika,
na kuwarudishia wenyewe ardhi hiyo;
9kuwaambia wafungwa, ‘Tokeni humo gerezani’,
na wale walio gizani, ‘Njoni nje mwangani!’
Kila mahali watakapokwenda watapata chakula
hata kwenye vilima vitupu watapata malisho.
10Hawataona tena njaa wala kuwa na kiu.
Upepo wa hari wala jua havitawachoma,
mimi niliyewahurumia nitawaongoza
na kuwapeleka kwenye chemchemi za maji.
11Milima yote nitaifanya kuwa njia,
na barabara zangu kuu nitazitengeneza.
12Watu wangu watarudi kutoka mbali,
wengine kutoka kaskazini na magharibi,
wengine kutoka upande wa kusini.”49:12 kutoka upande wa kusini: Makala ya Kiebrania Sinimu mji uliokaliwa na Waisraeli kusini mwa Misri.
13Imbeni kwa furaha, enyi mbingu!
Shangilia ewe dunia.
Pazeni sauti mwimbe enyi milima,
maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,
naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka.
14Wewe Siyoni wasema:
“Mwenyezi-Mungu ameniacha;
hakika Bwana wangu amenisahau.”
15Lakini Mwenyezi-Mungu asema:
“Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya,
asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake?
Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe,
mimi kamwe sitakusahau.
16Nimekuchora katika viganja vyangu;
kuta zako naziona daima mbele yangu.
17Watakaokujenga49:17 Watakaokujenga: Kulingana na makala ya Kiebrania iliyopatikana Kumrani na hati nyingine za kale. Tafsiri za mapokeo: Watoto wako. upya wanakuja haraka,
wale waliokuharibu wanaondoka.
18Inua macho uangalie pande zote;
watu wako wote wanakusanyika na kukujia.
Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu,
watu wako watakuwa kwako kama mapambo,
utawafurahia kama afanyavyo bibi arusi na utaji wake.
19“Kweli umekumbana na uharibifu,
makao yako yamekuwa matupu,
na nchi yako imeteketezwa.
Lakini sasa itakuwa ndogo mno kwa wakazi wake;
na wale waliokumaliza watakuwa mbali.
20Wanao waliozaliwa uhamishoni,
watakulalamikia wakisema:
‘Nchi hii ni ndogo mno;
tupatie nafasi zaidi ya kuishi.’
21Hapo ndipo utakapojiuliza mwenyewe:
‘Nani aliyenizalia watoto wote hawa?
Nilifiwa na wanangu bila kupata wengine.
Nilipelekwa uhamishoni na kutupwa mbali;
nani basi aliyewalea watoto hawa?
Mimi niliachwa peke yangu,
sasa, hawa wametoka wapi?’”
22Bwana Mungu asema hivi:
“Nitayapungia mkono mataifa;
naam, nitayapa ishara,
nayo yatawabeba watoto wenu wa kiume,
kadhalika na watoto wenu wa kike
na kuwarudisha kwako.
23Wafalme watakushughulikia,
na malkia watakutengenezea chakula.
Watakusujudia na kukupa heshima,
na kuramba vumbi iliyo miguuni pako.
Hapo utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu;
wote wanaonitegemea hawataaibika.”
24Watu wa Yerusalemu walalamika:
“Je, shujaa aweza kunyanganywa nyara zake?
Au mateka wa mtu katili waweza kuokolewa?”
25Mwenyezi-Mungu ajibu:
“Naam! Hata nyara za shujaa zitachukuliwa,
mateka wa mtu katili wataokolewa.
Mimi mwenyewe nitawakabili maadui zako,
mimi mwenyewe nitawaokoa watoto wako.
26Nitawafanya wanaokukandamiza watafunane;
watalewa damu yao wenyewe kama divai.
Hapo binadamu wote watatambua kwamba
mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mwokozi wako,
mimi ni Mkombozi wako, Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
Isaya49;1-26
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.