Mfungo wa kweli
1Mwenyezi-Mungu asema:
“Piga kelele, wala usijizuie;
paza sauti yako kama tarumbeta.
Watangazie watu wangu makosa yao,
waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao.
2Siku hata siku wananijia kuniabudu,
wanatamani kujua mwongozo wangu,
kana kwamba wao ni taifa litendalo haki,
taifa lisilosahau sheria za Mungu wao.
Wananitaka niamue kwa haki,
na kutamani kukaa karibu na Mungu.
3“Nyinyi mnaniuliza:
‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni?
Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’
“Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga,
mnatafuta tu furaha yenu wenyewe,
na kuwakandamiza wafanyakazi wenu!
4Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi.
Mkifunga namna hiyo
maombi yenu hayatafika kwangu juu.
5Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha;
mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi,
na kulalia nguo za magunia na majivu.
Je, huo ndio mnaouita mfungo?
Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami?
6“La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu:
Kuwafungulia waliofungwa bila haki,
kuziondoa kamba za utumwa,
kuwaachia huru wanaokandamizwa,
na kuvunjilia mbali udhalimu wote!
7 58:7 Taz Mat 25:35 Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako,
kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao,
kuwavalisha wasio na nguo,
bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu.
8“Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko,
mkiwa wagonjwa mtapona haraka.
Matendo yenu mema yatawatangulia,
nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu.
9Ndipo mtakapoomba,
nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia;
mtalia kwa sauti kuomba msaada,
nami nitajibu, ‘Niko hapa!’
“Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu,
mkiacha kudharau wengine na kusema maovu,
10mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa,
mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki,
mwanga utawaangazia nyakati za giza,
giza lenu litakuwa kama mchana.
11Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima,
nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida.58:11 maana ya neno hili Kiebrania si dhahiri.
Nitawaimarisha mwilini,
nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji,
kama chemchemi ya maji
ambayo maji yake hayakauki kamwe.
12Magofu yenu ya kale yatajengwa;
mtajenga upya juu ya misingi iliyoachwa zamani.
Nanyi mtaitwa watu waliotengeneza upya kuta,
watu waliozifanya barabara za mji zipitike tena.
Tuzo kwa kuiadhimisha Sabato
13“Kama ukiacha kufanya kazi siku ya Sabato,
ukaacha shughuli zako siku yangu hiyo takatifu;
kama ukiifanya siku yangu kuwa ya furaha,
ukaiheshimu siku hiyo takatifu ya Mwenyezi-Mungu,
ukaacha na shughuli58:13 shughuli: Au anasa. zako na kupiga domo,
14utapata furaha yako kwangu mimi Mwenyezi-Mungu,
nitakupatia ushindi katika kila pingamizi nchini,
nitakulisha mali ya Yakobo, babu yako.
Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Isaya58;1-14
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.