Yerusalemu mpya
1Inuka ee Siyoni uangaze;
maana mwanga unachomoza kwa ajili yako,
utukufu wa Mwenyezi-Mungu unakuangaza.
2Tazama, giza litaifunika dunia,
giza nene litayafunika mataifa;
lakini wewe, Mwenyezi-Mungu atakuangazia,
utukufu wake utaonekana kwako.
3Mataifa yataujia mwanga wako,
wafalme waujia mwanga wa pambazuko lako.
4Inua macho utazame pande zote;
wote wanakusanyika waje kwako.
Wanao wa kiume watafika toka mbali,
wanao wa kike watabebwa mikononi.
5Utaona na uso wako utangara,
moyo wako utasisimka na kushangilia.
Maana utajiri wa bahari utakutiririkia,
mali za mataifa zitaletwa kwako.
6Makundi ya ngamia yataifunika nchi yako,
naam, ndama wa ngamia kutoka Midiani na Efa;
wote kutoka Sheba watakuja.
Watakuletea dhahabu na ubani,
wakitangaza sifa za Mwenyezi-Mungu.
7Makundi ya kondoo wa Kedari yatakusanywa kwako,
utaweza kuwatumia kondoo madume wa Nebayothi kuwa kafara;
utawatoa kuwa tambiko inayokubalika madhabahuni pa Mungu,
naye ataitukuza nyumba yake tukufu.
8Nani hao wanaopepea kama mawingu,
kama njiwa wanaoruka kwenda viotani mwao?
9Ni meli zitokazo nchi za mbali,
zikitanguliwa na meli za Tarshishi.
Zinawaleta watoto wako,
pamoja na fedha na dhahabu yao,
kwa sifa ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
kwa sifa ya Mungu, Mtukufu wa Israeli,
maana amewafanya mtukuke.
10Mwenyezi-Mungu asema:
“Wageni watazijenga upya kuta zako,
wafalme wao watakutumikia.
Maana kwa hasira yangu nilikupiga,
lakini kwa fadhili yangu nimekuhurumia.
11 60:11 Taz Ufu 21:25-26 Malango yako yatakuwa wazi daima;
usiku na mchana hayatafungwa,
ili watu wakuletee utajiri wa mataifa,
pamoja na wafalme wao katika maandamano.
12Kila ufalme au taifa lisilokutumikia litaangamia;
mataifa hayo yatatokomezwa kabisa.
13“Utaletewa fahari ya msitu wa Lebanoni:
Mbao za miberoshi, mivinje na misonobari,
zitumike kupamba mahali pa maskani yangu;
nami nitaparembesha hapo ninapokaa.
14 60:14 Taz Ufu 3:9 Wazawa wa wale waliokudhulumu,
watakuja na kukuinamia kwa heshima.
Wote wale waliokudharau,
watasujudu mbele ya miguu yako.
Watakuita: ‘Mji wa Mwenyezi-Mungu’,
‘Siyoni, Mji wa Mtakatifu wa Israeli’.
15“Wewe ulikuwa umeachwa na kuchukiwa,
hakuna aliyependa hata kupitia kwako.
Lakini sasa nitakufanya uwe na fahari milele,
utakuwa mji wa furaha kizazi hata kizazi.
16Utaletewa chakula na watu wa mataifa,
naam, wafalme watakupatia chakula bora.
Hapo utatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mwokozi wako;
mimi Mwenye Nguvu wa Yakobo ni Mkombozi wako.
17“Badala ya shaba nitakuletea dhahabu,
badala ya chuma nitakuletea fedha,
badala ya miti, nitakuletea shaba,
na badala ya mawe nitakuletea chuma.
Amani itatawala juu yako,
uadilifu utakuongoza.
18Ukatili hautasikika tena nchini mwako;
wala uharibifu na maangamizi ndani ya mipaka yako.
Utaweza kuziita kuta zako: ‘Wokovu’,
na malango yako: ‘Sifa’.60:18 Wokovu, Sifa: Majina mapya yanamaanisha hali mpya.
19Hutahitaji tena jua kukuangazia mchana,
wala mwezi kukumulikia usiku;
maana mimi Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele;
mimi Mungu wako nitakuwa fahari yako.
20Mwanga wako mchana hautatua kama jua,
wala mwangaza wako usiku kufifia kama mbalamwezi;
maana Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele,
nazo siku zako za kuomboleza zitakoma.
21Watu wako wote watakuwa waadilifu,
nao wataimiliki nchi milele.
Hao ni chipukizi nililopanda mimi,
kazi ya mikono yangu kwa ajili ya utukufu wangu.
22Aliye mdogo kati yenu atakuwa ukoo,
aliye mdogo kuliko wote atakuwa taifa kubwa.
Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu;
wakati ufikapo nitayatekeleza hayo haraka.”
Isaya60;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.