Yeremia anamhoji Mwenyezi-Mungu
1Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu,
ingawa nakulalamikia.
Lakini ningependa kutoa hoja zangu mbele yako:
Kwa nini waovu hufanikiwa katika mambo yao?
Mbona wote wenye hila hustawi?
2Unawaotesha nao wanaota;
wanakua na kuzaa matunda.
Wanakutaja kwa maneno yao,
lakini mioyo yao iko mbali nawe.
3Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu wanijua;
wayathibiti maelekeo yangu kwako.
Uwaokote hao kama kondoo wa kuchinjwa,
watenge kwa ajili ya wakati wa kuuawa.
4Mpaka lini nchi itaomboleza kwa ukame,
na nyasi za mashamba yote kunyauka?
Wanyama na ndege wanakufa kwa uovu wa wakazi wake;
wanasema: “Mungu hataona mwisho wetu.”12:4 Kiebrania: Mwisho wetu; baadhi ya tafsiri nyingine: Yale tunayofanya.
5Mwenyezi-Mungu asema,
“Ikiwa umeshindana na waendao kwa miguu ukachoka,
utawezaje kushindana na farasi?
Kama unaanguka katika nchi isiyo na vizuizi,
utafanyaje katika msitu wa Yordani?
6Hata ndugu zako, jamaa yako mwenyewe,
nao pia wamekutendea mambo ya hila;
wanakukemea waziwazi.
Usiwaamini hata kidogo,
japo wanakuambia maneno mazuri.”
Mungu anaiacha nyumba yake na watu wake
7Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nimeiacha nyumba yangu;
nimeitupa mali yangu mimi mwenyewe.
Israeli, mpenzi wangu wa moyo,
nimemtia mikononi mwa maadui zake.
8Wateule wangu wamenigeuka,
wamekuwa kama simba porini,
wameningurumia mimi;
ndiyo maana nawachukia.
9Wateule wangu wamekuwa ndege mzuri
wanaoshambuliwa na kozi pande zote.
Nenda ukawakusanye wanyama wote wakali
waje kushiriki katika karamu.
10Wachungaji wengi wameharibu shamba langu la mizabibu,
wamelikanyagakanyaga chini lililo mali yangu;
shamba langu zuri wamelifanya jangwa.
11Wamelifanya kuwa tupu;
katika ukiwa wake lanililia.
Nchi yote imekuwa jangwa,
wala hakuna mtu anayejali.
12Juu ya milima yote jangwani,
watu wamefika kuangamiza.
Upanga wangu unapita kuiangamiza nchi,
toka upande mmoja hadi mwingine,
wala hakuna mtu atakayeishi kwa amani.
13Walipanda ngano, lakini walivuna magugu;
walifanya bidii, lakini hawakupata kitu.
Kwa sababu ya hasira yangu kali,
mavuno watakayoyapata yatakuwa aibu tupu.”
Mungu na majirani wa Israeli
14Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya jirani wabaya wa watu wangu: “Wamekigusa kile kilicho changu, kile nilichowapa watu wangu Israeli! Basi nitawangoa kutoka katika nchi yao. Hata watu wa Yuda nitawangoa katika nchi yao. 15Lakini baada ya kuwangoa, nitawahurumia tena; nitalirudisha kila taifa katika sehemu yake na katika nchi yake. 16Na kama watajifunza njia za watu wangu kwa moyo wote, kama wataapa kwa jina langu kwa kusema, ‘Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu,’ kama vile walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa jina la mungu Baali, basi watajengeka miongoni mwa watu wangu. 17Lakini taifa lolote ambalo halitanitii, nitalingoa kabisa na kuliangamiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yeremia12;1-17
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.