Ukame wa kutisha
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia kuhusu ule ukame:
2“Watu wa Yuda wanaomboleza,
na malango yao yanalegea.
Watu wake wanaomboleza udongoni
na kilio cha Yerusalemu kinapanda juu.
3Wakuu wake wanawatuma watumishi wao maji;
watumishi wanakwenda visimani,
lakini maji hawapati;
wanarudi na vyombo vitupu.
Kwa aibu na fadhaa wanafunika vichwa vyao.
4Wakulima wanahuzunika na kufunika vichwa vyao
kwa kuona jinsi ardhi ilivyonyauka.
5Hata kulungu porini anamwacha mtoto wake mchanga,
kwa sababu hakuna nyasi.
6Pundamwitu wanasimama juu ya vilele vikavu,
wanatweta kwa kukosa hewa kama mbweha;
macho yao yanafifia kwa kukosa chakula.
7“Nao watu wanasema:
Ingawa dhambi zetu zashuhudia dhidi yetu,
utusaidie ee Mwenyezi-Mungu kwa heshima ya jina lako.
Maasi yetu ni mengi,
tumetenda dhambi dhidi yako.
8Ewe uliye tumaini la Israeli,
mwokozi wetu wakati wa taabu,
utakuwaje kama mgeni nchini mwetu,
kama msafiri alalaye usiku mmoja?
9Utakuwaje kama mtu uliyechanganyikiwa,
kama shujaa asiyeweza kusaidia mtu?
Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi;
sisi twaitwa kwa jina lako, usituache.”
10Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya watu hawa:
“Kweli wamependa sana kutangatanga,
wala hawakujizuia;
kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu siwapokei.
Sasa nitayakumbuka makosa yao,
na kuwaadhibu kwa dhambi zao.”
11Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Usiwaombee watu hawa fanaka. 12Hata wakifunga, sitayasikiliza maombi yao, na hata wakinitolea sadaka za kuteketeza na za nafaka, mimi sitazikubali. Bali nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
13Kisha mimi nikasema, “Tazama, ee Bwana Mwenyezi-Mungu! Manabii wanawaambia watu hawa kwamba hapatakuwa na vita wala njaa, kwa sababu umeahidi kuwa patakuwa na amani tu katika nchi yetu.”
14Naye Mwenyezi-Mungu, akaniambia: “Hao manabii wanatoa unabii wa uongo kwa jina langu. Mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi yasiyo na maana yoyote, uongo wanaojitungia wenyewe. 15Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi kuhusu hao manabii wanaotabiri kwa jina langu, ingawa mimi sikuwatuma, na wanaosema kwamba hapatakuwa na vita wala njaa katika nchi hii: Manabii hao wataangamia kwa upanga na kwa njaa. 16Na hao ambao waliwatabiria mambo hayo, watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu wakiwa wamekufa kwa njaa na vita, wala hapatakuwa na mtu wa kuwazika. Hayo yatawapata wao wenyewe, wake zao, watoto wao wa kike na wa kiume; maana mimi nitawamwagia uovu wao wenyewe.
17Hivi ndivyo utakavyowaambia:
Laiti macho yangetoa machozi kutwa kucha,
wala yasikome kububujika,
maana, watu wangu wamejeruhiwa vibaya,
wamepata pigo kubwa sana.
18Nikienda nje mashambani,
naiona miili ya waliouawa vitani;
nikiingia ndani ya mji,
naona tu waliokufa kwa njaa!
Manabii na makuhani wanashughulikia mambo yao nchini,
wala hawajui wanalofanya.”14:18 Manabii … wanalofanya: Au Manabii na makuhani wameburutwa hadi katika nchi wasiyoifahamu kabisa.
Watu wanamsihi Mungu
19Ee Mwenyezi-Mungu, je, umemkataa Yuda kabisa?
Je, moyo wako umechukizwa na Siyoni?
Kwa nini umetupiga vibaya,
hata hatuwezi kupona tena?
Tulitazamia amani, lakini hatukupata jema lolote;
tulitazamia wakati wa kuponywa, badala yake tukapata vitisho.
20Tunakiri uovu wetu, ee Mwenyezi-Mungu,
tunakiri uovu wa wazee wetu,
maana, tumekukosea wewe.
21Usitutupe, kwa heshima ya jina lako;
usikidharau kiti chako cha enzi kitukufu.
Ukumbuke agano ulilofanya nasi, wala usilivunje.
22Je miungu ya uongo ya mataifa
yaweza kuleta mvua?
Au, je, mbingu zaweza kutoa manyunyu?
Je, si wewe ee Mwenyezi-Mungu uliye Mungu wetu?
Tunakuwekea wewe tumaini letu,
maana wewe unayafanya haya yote.
Yeremia14;1-22
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.