Hosea anatangaza adhabu ya Israeli
1Msifurahi enyi Waisraeli!
Msifanye sherehe kama mataifa mengine;
maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu.
Mmefurahia malipo ya uzinzi,
kila mahali pa kupuria nafaka.
2Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha,
hamtapata divai mpya.
3Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu;
naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri;
watakula vyakula najisi huko Ashuru.
4Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai,
wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao.
Chakula chao kitakuwa kama cha matanga,
wote watakaokila watatiwa unajisi.
Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu,
hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.
5Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa,
au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu?9:5 Labda ni sikukuu iitwayo ya vibanda, Taz fahirisi.
6Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu,
Misri itawakaribisheni kwake,
lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi.
Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha,
miiba itajaa katika mahema yenu.
7Siku za adhabu zimewadia,
naam, siku za kulipiza kisasi zimefika;
Waisraeli lazima wautambue wakati huo!
Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu;
anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.”
Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa,
kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake.
8Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu;
lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege.
Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa.
9 Taz Amu 19:21 Nyinyi mmezama katika uovu,
kama ilivyokuwa kule Gibea.
Mungu atayakumbuka makosa yao,
na kuwaadhibu kwa dhambi zao.
Dhambi ya Israeli na matokeo yake
10Mwenyezi-Mungu asema:
“Nilipowakuta Waisraeli
walikuwa kama zabibu jangwani.
Nilipowaona wazee wenu
walikuwa bora kama tini za kwanza.
Lakini mara walipofika huko Baal-peori,
walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali,
wakawa chukizo kama hicho walichokipenda.
11Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege;
watoto hawatazaliwa tena,
hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa,
wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba!
12Hata kama wakilea watoto,
sitamwacha hai hata mmoja wao.
Ole wao, nitakapowaacha peke yao!”
13Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza,
Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri;
lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe.
14Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu!
Lakini utawaadhibu namna gani?
Uwafanye wanawake wao kuwa tasa;
uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao!
Hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwa Israeli
15Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Uovu wao wote ulianzia Gilgali;
huko ndiko nilipoanza kuwachukia.
Kwa sababu ya uovu wa matendo yao,
nitawafukuza nyumbani kwangu.
Sitawapenda tena.
Viongozi wao wote ni waasi.
16Watu wa Efraimu wamepigwa,
wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu,
hawatazaa watoto wowote.
Hata kama wakizaa watoto,
nitawaua watoto wao wawapendao.”
17Kwa vile wamekataa kumsikiliza,
Mungu wangu atawatupa;
wao watatangatanga kati ya mataifa.
Hosea9;1-17
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe