1Watu wa Efraimu wananirundikia uongo,
na Waisraeli udanganyifu.
Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu.
2“Watu wa Efraimu wanachunga upepo
kutwa nzima wanafukuza upepo wa mashariki.
Wanazidisha uongo na ukatili,
wanafanya mkataba na Ashuru
na kupeleka mafuta Misri.”
3Mwenyezi-Mungu ana mashtaka dhidi ya Yuda;
atawaadhibu wazawa wa Yakobo kadiri ya makosa yao,
na kuwalipa kadiri ya matendo yao.
4Yakobo akiwa bado tumboni mwa mama yake,
alimshika kisigino kaka yake.
Na alipokuwa mtu mzima
alishindana na Mungu.
5Alipambana na malaika, akamshinda;
alilia machozi na kuomba ahurumiwe.
Huko Betheli, alikutana na Mungu,
huko Mungu aliongea naye.
6Mwenyezi-Mungu, wa majeshi,
Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake.
Lakini nyinyi mrudieni Mungu wenu.
Zingatieni upendo na haki,
mtumainieni Mungu wenu daima.
7“Efraimu ni sawa na mfanyabiashara
atumiaye mizani danganyifu,
apendaye kudhulumu watu.
8Efraimu amesema,
‘Mimi ni tajiri!
Mimi nimejitajirisha!
Hamna ubaya kupata faida.
Hata hivyo, hilo si kosa!’”
9Mwenyezi-Mungu asema, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;
mimi ndimi niliyekutoa nchini Misri!
Mimi nitakukalisha tena katika mahema,
kama ufanyavyo sasa kwa siku chache tu,
wakati wa sikukuu ya vibanda.
10Mimi niliongea na manabii;
ni mimi niliyewapa maono mengi,
na kwa njia yao natangaza mpango wangu.
11Huko Gileadi ni mahali pa dhambi;
huko Gilgali walitambika fahali,
kwa hiyo madhabahu zao zitakuwa marundo ya mawe kwenye mitaro shambani.”
12Yakobo alikimbia nchi ya Aramu
akiwa huko alifanya kazi apate mke,
akachunga kondoo ili apate mke.
13Kwa nabii Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri,
na kwa nabii Mungu aliwahifadhi.
14Waefraimu wamemchukiza Mwenyezi-Mungu sana.
Lakini Mwenyezi-Mungu atawalipiza makosa yao,
atawaadhibu kwa mambo maovu waliyotenda.
Hosea12;1-14
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe