Kumrudia Mungu na hali mpya
1Enyi Waisraeli,
mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Mmejikwaa kwa sababu ya uovu wenu.
2Ombeni toba kwake,
mrudieni na kumwambia:
“Utusamehe uovu wote,
upokee zawadi zetu,
nasi tutakusifu kwa moyo.
3Ashuru haitatuokoa,
hatutategemea tena farasi wa vita.
Hatutaviita tena: ‘Mungu wetu’
hivyo vinyago tulivyochonga wenyewe.
Kwako ee Mungu yatima hupata huruma.”
4Mwenyezi-Mungu asema,
“Nitaponya utovu wao wa uaminifu;
nitawapenda tena kwa hiari yangu,
maana sitawakasirikia tena.
5Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli
nao watachanua kama yungiyungi,
watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni.
6Chipukizi zao zitatanda na kuenea,
uzuri wao utakuwa kama mizeituni,
harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni.
7Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu,
watastawi kama bustani nzuri.
Watachanua kama mzabibu,
harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni.
8Enyi watu wa Efraimu,
mna haja gani tena na sanamu?
Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu,
mimi ndiye ninayewatunzeni.
Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi,
kutoka kwangu mtapata matunda yenu.
9Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya,
mtu aliye na busara ayatambue.
Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu;
watu wanyofu huzifuata,
lakini wakosefu hujikwaa humo.”
Hosea14;1-9
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe