Mungu atayahukumu mataifa
1“Wakati huo na siku hizo
nitakapoirekebisha hali ya Yuda na Yerusalemu,
2nitayakusanya mataifa yote,
niyapeleke katika bonde liitwalo,
‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu.
Huko nitayahukumu mataifa hayo,
kwa mambo yaliyowatendea watu wangu Israeli,
hao walio mali yangu mimi mwenyewe.
Maana waliwatawanya miongoni mwa mataifa,
waligawa nchi yangu
3na kugawana watu wangu kwa kura.
Waliwauza wavulana ili kulipia malaya,
na wasichana ili kulipia divai.
4“Mnataka kunifanya nini enyi Tiro na Sidoni na maeneo yote ya Filistia? Je, mna kisasi nami mnachotaka kulipiza? Kama mnalipiza kisasi, mimi nitawalipizeni mara moja! 5Mmechukua fedha na dhahabu yangu, na kuvibeba vitu vyangu vya thamani hadi kwenye mahekalu yenu. 6Mmewapeleka watu wa Yuda na Yerusalemu mbali na nchi yao, mkawauza kwa Wagiriki. 7Sasa, nitawarudisha watu wangu kutoka huko mlikowauza. Nitawalipizeni kisasi kwa yote mliyowatendea. 8Watoto wenu wa kiume na wa kike nitawafanya wauzwe kwa watu wa Yuda, nao watawauzia Washeba, watu wa taifa la mbali kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
9“Watangazieni watu wa mataifa jambo hili:
Jitayarisheni kwa vita,
waiteni mashujaa wenu;
askari wote na wakusanyike,
waende mbele.
10 Taz Isa 2:4; Mika 4:3 Majembe yenu yafueni yawe mapanga,
miundu yenu ya kupogolea iwe mikuki.
Hata aliye dhaifu na aseme:
‘Mimi pia ni shujaa’.
11Njoni haraka, enyi mataifa yote jirani,
kusanyikeni huko bondeni.”
Ee Mwenyezi-Mungu!
Teremsha askari wako dhidi yao!
12“Haya mataifa na yajiweke tayari;
yaje kwenye bonde liitwalo:
‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu’.
Huko, mimi Mwenyezi-Mungu,
nitaketi kuyahukumu mataifa yote ya jirani.
13 Taz Ufu. 14:14-16, 19-20 Haya! Chukueni mundu wa kuvuna,
kwani sasa ni wakati wa mavuno.
Ingieni! Wapondeni kama zabibu
ambazo zimejaza shinikizo.
Uovu wao umepita kiasi
kama mapipa yanayofurika.”
14Wanafika makundi kwa makundi
kwenye bonde la Hukumu,
maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia.
15Jua na mwezi vinatiwa giza,
na nyota zimeacha kuangaza.
Mungu atawabariki watu wake
16Mwenyezi-Mungu ananguruma huko Siyoni;
sauti yake inavuma kutoka Yerusalemu;
mbingu na dunia vinatetemeka.
Lakini Mwenyezi-Mungu ni kimbilio la watu wake,
ni ngome ya usalama kwa Waisraeli.
17“Hapo, ewe Israeli,
utajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
nakaa Siyoni, mlima wangu mtakatifu,
Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu;
na wageni hawatapita tena humo.
18“Wakati huo, milima itatiririka divai mpya,
na vilima vitatiririka maziwa.
Vijito vyote vya Yuda vitajaa maji;
chemchemi itatokea nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu,
na kulinywesha bonde la Shitimu.3:18 Shitimu: Kiebrania; au Mgunga.
19“Misri itakuwa mahame,
Edomu itakuwa jangwa tupu,
kwa sababu waliwashambulia watu wa Yuda
wakawaua watu wasio na hatia.
20Bali Yuda itakaliwa milele,
na Yerusalemu kizazi hata kizazi.
21Nitawaadhibu waliomwaga damu ya watu wa Yuda
wala sitawaachia wenye hatia.
Mimi, Mwenyezi-Mungu nakaa Siyoni.”
Yoeli3;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe