Mwito wa toba
1Kusanyikeni, kusanyikeni enyi taifa la watu wasio na aibu,
2kabla hamjapeperushwa mbali kama makapi,2:2 kabla … makapi: Makala ya Kiebrania si dhahiri.
kabla haijawajia siku ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu,
kabla haijawajia siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
3Mtafuteni Mwenyezi-Mungu enyi wanyenyekevu wote nchini,
enyi mnaozitii amri zake.
Tafuteni uadilifu, tafuteni unyenyekevu;
labda mtaiepa siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
Maangamizi kwa mataifa ya jirani
4Mji wa Gaza utahamwa,
Ashkeloni utakuwa tupu.
Wakazi wa Ashdodi watatimuliwa mchana,
na wale wa Ekroni watang'olewa.
5Ole wenu wakazi wa nchi za pwani,
watu mnaoishi huko Krete!
Mwenyezi-Mungu ametamka dhidi yenu
enyi wakazi wa Kanaani, nchi ya Filistia:
Mimi nitawaangamiza asibaki hata mkazi mmoja!
6Nanyi nchi za pwani mtafanywa kuwa malisho;
mtakuwa vibanda vya wachungaji
na mazizi ya kondoo.
7Nchi ya pwani itamilikiwa na mabaki ya ukoo wa Yuda.
Watachunga mifugo yao huko.
Nyumba za mji wa Ashkeloni
zitakuwa mahali pao pa kulala.
Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wao atawakumbuka
na kuwarudishia hali yao njema.
8“Nimeyasikia masuto ya Moabu
na dhihaka za Waamoni;
jinsi walivyowasuta watu wangu,
na kujigamba kuiteka nchi yao.
9Kwa hiyo, niishivyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
mimi Mungu wa Israeli,
Moabu itakuwa kama Sodoma
na Amoni itakuwa kama Gomora.
Nchi zake zitakuwa za viwavi na mashimo ya chumvi,
zitakuwa ukiwa milele.
Watu wangu watakaobaki wataziteka nyara,
watu wa taifa langu waliosalia watazimiliki.”
10Hayo yatakuwa malipo ya kiburi chao,
kwa sababu waliwadhihaki na kujigamba
dhidi ya watu wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
11Mwenyezi-Mungu atakuwa wa kutisha dhidi yao;
miungu yote ya dunia ataikondesha.
Mataifa yote duniani yatamsujudia;
kila taifa katika mahali pake.
12Nanyi watu wa Kushi pia
mtauawa kwa upanga wake.
13Mwenyezi-Mungu atanyosha mkono wake kaskazini,
na kuiangamiza nchi ya Ashuru.
Ataufanya mji wa Ninewi kuwa ukiwa,
kuwa mahali pakavu kama jangwa.
14Makundi ya mifugo yatalala humo,
kadhalika kila mnyama wa porini.
Tai na yangeyange na korongo wataishi juu ya nguzo zake,
bundi watalia kwenye madirisha yake,
kunguru watalia kwenye vizingiti,
maana nyumba zake za mierezi zitakuwa tupu.
15Je, huu ndio mji uliojivuna na kuishi kwa usalama,
mji uliojisemea, “Ni mimi tu, hakuna mwingine!”
Jinsi gani umekuwa mtupu
na makao ya wanyama wa mwituni!
Kila apitaye karibu atauzomea na kuudharau.
Sefania2;1-15
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe