Hukumu ya Yerusalemu
1Ole wake mji wa Yerusalemu,
mji mchafu, najisi na mdhalimu.
2Hausikilizi onyo lolote,
wala haukubali kukosolewa.
Haukumtegemea Mwenyezi-Mungu kamwe,
wala kumkaribia Mungu wake.
3Viongozi wake ni simba wangurumao,
mahakimu wake ni mbwamwitu wenye njaa jioni
wasioacha chochote mpaka asubuhi.
4Manabii wake ni watu wasiojali na wadanganyifu.
Makuhani wake wamevitia unajisi vitu vitakatifu
na kuihalifu sheria kwa nguvu.
5Lakini Mwenyezi-Mungu aliye mjini humo ni mwadilifu,
yeye hatendi jambo lolote baya.
Kila siku asubuhi hudhihirisha kauli yake,
naam, kila kunapopambazuka huitekeleza.
Lakini wahalifu hawana aibu hata kidogo.
6Mwenyezi-Mungu asema:
“Nimeyafutilia mbali mataifa;
kuta zao za kujikinga ni magofu.
Barabara zao nimeziharibu,
na hamna apitaye humo.
Miji yao imekuwa mitupu,
bila watu, na bila wakazi.
7Nilisema, ‘Hakika mji huu watanicha
na kukubali kukosolewa;
hautaacha kukumbuka mara hizo zote nilizowaadhibu.’
Lakini watu wake walizidisha tamaa zao
za kufanya matendo yao kuwa upotovu.
8“Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu,
ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka.
Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme,
kuyamwagia ghadhabu yangu,
kadhalika na ukali wa hasira yangu.
Dunia yote itateketezwa
kwa moto wa ghadhabu yangu.
9“Wakati huo nitaibadili lugha ya watu,
nitawawezesha kusema lugha adili
ili waniite mimi Mwenyezi-Mungu,
na kuniabudu kwa moyo mmoja.
10Kutoka ng'ambo ya mito ya Kushi
watu wangu wanaoniomba ambao wametawanyika,
wataniletea sadaka yangu.
11“Siku hiyo, haitakulazimu kuona aibu,
kutokana na matendo yako ya kuniasi,
maana nitawaondoa miongoni mwako
wale wanaojigamba na kujitukuza
nawe hutakuwa na kiburi tena katika mlima wangu mtakatifu.
12Nitakuachia watu wapole na wanyenyekevu
ambao watakimbilia usalama kwangu mimi Mwenyezi-Mungu.
13Waisraeli watakaobaki,
hawatatenda mabaya wala hawatasema uongo;
wala kwao hatapatikana mdanganyifu yeyote.
Watapata malisho na kulala
wala hakuna mtu atakayewatisha.”
Wimbo wa furaha
14Imba kwa sauti, ewe Siyoni,
paza sauti ee Israeli.
Furahi na kushangilia kwa moyo wote, ewe Yerusalemu!
15Mwenyezi-Mungu amekuondolea hukumu iliyokukabili,
amewageuzia mbali adui zako.
Mwenyezi-Mungu, mfalme wa Israeli yuko pamoja nawe
hutaogopa tena maafa.
16Siku hiyo, mji wa Yerusalemu utaambiwa:
“Usiogope, ee Siyoni,
usilegee mikono.
17Mwenyezi-Mungu, Mungu wako yu pamoja nawe
yeye ni shujaa anayekuletea ushindi.
Yeye atakufurahia kwa furaha kuu,
kwa upendo wake atakujalia uhai mpya.
Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa,
18kama vile katika siku ya sikukuu.”
Mwenyezi-Mungu asema:
“Nitakuondolea maafa yako,
nawe hutahitaji kuona aibu kwa ajili yake.
19Wakati huo, nitawaadhibu wote wanaokukandamiza.
Nitawaokoa vilema na kuwakusanya waliotupwa,
na kubadili aibu yao kuwa sifa
na fahari duniani kote.
20Wakati huo nitawakusanya,
na kuwafanya mjulikane na kusifiwa,
miongoni mwa watu wote duniani
nitakapowarudishia hali yenu njema
nanyi muone kwa macho yenu wenyewe.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Sefania3;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe