Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 29 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 11...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Alimjulisha Mose mwongozo wake, aliwaonesha watu wa Israeli matendo yake. Mwenyezi-Mungu ni mwenye rehema na huruma; ni mvumilivu na mwingi wa fadhili.

Zaburi 103:7-8

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....




Hatukemeikemei daima, wala hasira yake haidumu milele. Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu.

Zaburi 103:9-10

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi.

Zaburi 103:11-12

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.




 Yesu anafundisha juu ya kusali

(Mat 6:9-13; 7:7-11)
1Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.” 2Yesu akawaambia, “Mnaposali, semeni:
‘Baba!
Jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike.
3Utupe daima chakula chetu cha kila siku.
4Utusamehe dhambi zetu,
maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea;
wala usitutie katika majaribu.’”
5Kisha akawaambia, “Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: ‘Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu, 6kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.’ 7Naye, akiwa ndani angemjibu: ‘Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!’ 8Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. 9Kwa hiyo, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni mlango nanyi mtafunguliwa. 10Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye mlango hufunguliwa. 11Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki? 12Na kama akimwomba yai, je, atampa nge? 13Kama nyinyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba.”
Yesu na Beelzebuli
(Mat 12:22-30; Marko 3:20-27)
14Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea, hata umati wa watu ukashangaa. 15Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” 16Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. 17Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia. 18Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? 19Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi. 20Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.
21“Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. 22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. 23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
Kurudi kwa pepo mbaya
(Mat 12:43-45)
24“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’ 25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. 26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.”
Furaha ya kweli
27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” 28Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
Wanataka ishara
(Mat 12:38-42)
29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya Yona. 30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. 31Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni na kumbe hapa pana mkuu kuliko Solomoni. 32Watu wa Ninewi watatokea wakati wa hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na kumbe hapa pana kikuu kuliko Yona!
Mwanga wa mwili
(Mat 5:15; 6:22-23)
33“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa debe, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga. 34Jicho lako ni taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza. 35Uwe mwangalifu basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. 36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utangaa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”
Yesu anawalaumu Mafarisayo na waalimu wa sheria
(Mat 23:1-36; Marko 12:38-40)
37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. 38Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza. 39Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. 40Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? 41Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu.
42“Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.
43“Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. 44Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”
45Mmoja wa waalimu wa sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.” 46Yesu akamjibu, “Na nyinyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku nyinyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. 47Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. 48Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. 49Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: ‘Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.’ 50Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; 51tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka ile ya Zekaria ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo hayo.
52“Ole wenu nyinyi waalimu wa sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; nyinyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie.”
53Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na waalimu wa sheria walianza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi 54ili wapate kumnasa kwa maneno yake.

Luka11;1-53
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Wednesday, 28 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 10...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote.

Zaburi 103:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake.

Zaburi 103:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao.

Zaburi 103:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.




Yesu anawatuma wafuasi sabini na wawili
1Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda. 2Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. 3Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma nyinyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwamwitu. 4Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani. 5Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: ‘Amani iwe katika nyumba hii!’ 6Kama akiwako mpenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni. 7Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile. 8Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni. 9Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.’ 10Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni: 11‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunayapangusa dhidi yenu. Lakini, jueni kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile ya watu wa Sodoma.
Ole kwa miji isiyotubu
(Mat 11:20-24)
13“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kukaa katika majivu kutubu. 14Hata hivyo, siku ya hukumu nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. 15Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu.”
16Halafu akasema, “Anayewasikiliza nyinyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea nyinyi, anakataa kunipokea mimi. Na yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma.”
Wale sabini na wawili wanarudi
17Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako.” 18Yeye akawaambia, “Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni. 19Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na nge, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru. 20Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Furaha ya Yesu
(Mat 11:25-27; 13:16-17)
21Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.”
22Kisha akasema, “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumfunulia.”
23Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, “Heri wanaoona yale mnayoyaona nyinyi! 24Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona nyinyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie.”
Mfano wa Msamaria mwema
25Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?” 26Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?” 27Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” 28Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.”
29Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” 30Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. 31Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. 32Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando. 33Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. 34Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza. 35Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’” 36Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?” 37Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”
Yesu nyumbani kwa Martha na Maria

38Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake. 39Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. 40Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.” 41Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi. 42Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyanganya.” 



Luka10;1-42

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe