Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 2 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 13...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Mwenyezi-Mungu ameweka kiti chake cha enzi mbinguni; yeye anatawala juu ya vitu vyote. Enyi malaika wakuu, msifuni Mwenyezi-Mungu; mnaotimiza amri zake na kutekeleza neno lake!

Zaburi 103:19-20



Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Enyi jeshi lote la mbinguni, msifuni Mwenyezi-Mungu; enyi watumishi wake mnaotekeleza matakwa yake!

Zaburi 103:21

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Msifuni Mwenyezi-Mungu enyi viumbe vyake vyote; msifuni popote mlipo katika milki yake. Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu!

Zaburi 103:22

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Acheni dhambi zenu au mtakufa
Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko. 2Naye Yesu akawaambia, “Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo? 3Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu mtaangamia kama wao. 4Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu, wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu? 5Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao.”
Mfano wa mtini usiozaa
6Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini shambani mwake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja. 7Basi, akamwambia mfanyakazi wake: ‘Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, bila kupata chochote. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?’ 8Lakini yeye akamjibu: ‘Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea. 9Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata.’”
Yesu anamponya mama mmoja siku ya Sabato
10Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato. 11Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima. 12Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, “Mama, umeponywa ugonjwa wako.” 13Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu. 14Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya huyo mama siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu waliokusanyika pale, “Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato.”
15Hapo Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato? 16Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?” 17Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.
Mfano wa mbegu ndogo ya haradali
(Mat 13:33)
18Yesu akauliza: “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini? 19Ni kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota na kuwa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake.”
Mfano wa chachu
(Mat 13:31-32; Marko 4:30-32)
20Tena akauliza: “Nitaulinganisha ufalme wa Mungu na nini? 21Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga madebe mawili na nusu kisha unga wote ukaumuka.”
Mlango mwembamba
(Mat 7:13-14,21-23)
22Yesu aliendelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri. 23Mtu mmoja akamwuliza, “Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?” 24Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. 25Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Nyinyi mtasimama nje na kuanza kubisha mlango mkisema: ‘Bwana, tufungulie mlango.’ Lakini yeye atawajibu: ‘Sijui mmetoka wapi.’ 26Nanyi mtaanza kumwambia: ‘Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.’ 27Lakini yeye atasema: ‘Sijui nyinyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.’ 28Ndipo kutakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo na manabii wote wapo katika ufalme wa Mungu, lakini nyinyi wenyewe mmetupwa nje! 29Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini na kukaa kwenye karamu katika ufalme wa Mungu. 30Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Upendo wa Yesu kwa Yerusalemu
(Mat 23:37-39)
31Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua.” 32Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: ‘Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.’ 33Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu.
34“Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. 35Haya! Utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Basi, nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: ‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’”

Luka13;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Friday, 30 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 12...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao. Mungu ajua mfumo wa nafsi zetu; ajua kwamba sisi ni mavumbi.

Zaburi 103:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Walakini binadamu, maisha yake ni kama nyasi tu; huchanua kama ua shambani: Upepo huvuma juu yake nalo latoweka; na mahali lilipokuwa hapaonekani tena.

Zaburi 103:15-16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Lakini fadhili za Mwenyezi-Mungu hudumu milele, kwa wale wote wanaomheshimu; na wema wake wadumu vizazi vyote, kwa wote wanaozingatia agano lake, wanaokumbuka kutii amri zake.

Zaburi 103:17-18

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Onyo kuhusu unafiki

1Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. 2Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. 3Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonongona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.
Anayestahili kuogopwa
(Mat 10:28-31)
4“Nawaambieni nyinyi rafiki zangu: Msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. 5Nitawaonesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. 6Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa sarafu ndogo kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. 7Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi!
Kumkiri na kumkana Kristo
(Mat 10:32-33; 12:32; 10:19-20)
8“Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. 9Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
10“Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
11“Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. 12Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.”
Mfano wa tajiri mpumbavu
13Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.” 14Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?”
15Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” 16Kisha akawaambia mfano: “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. 17Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? 18Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. 19Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’ 20Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’” 21Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.”
Mtumaini Mungu
(Mat 6:25-34)
22Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. 23Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. 24Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! 25Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? 26Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? 27Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. 28Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
29“Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. 30Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. 31Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada.
Utajiri mbinguni
(Mat 6:19-21)
32“Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. 33Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. 34Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
Watumishi waangalifu
35“Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; 36muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha. 37Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. 38Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao! 39Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. 40Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
Mtumishi mwaminifu na asiye mwaminifu
(Mat 24:45-51)
41Petro akamwambia, “Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?” 42Bwana akajibu, “Ni nani, basi, aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao? 43Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote. 45Lakini, kama mtumishi huyo akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia sana kurudi;’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa, 46bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamwadhibu mtumishi huyo vibaya12:46 atamwadhibu…vibaya: Neno kwa neno: Atamkata vipande vipande. na kumweka fungu moja na wasioamini. 47Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. 48Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atadaiwa vingi; aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi.
Yesu ni sababu ya utengano na watu
(Mat 10:34-36)
49“Nimekuja kuwasha moto duniani; laiti ungekuwa umewaka tayari! 50Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike! 51Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano. 52Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. 53Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mamamkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mamamkwe wake.”
Kufahamu majira
(Mat 16:2-3)
54Yesu akayaambia tena makundi ya watu, “Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: ‘Mvua itanyesha,’ na kweli hunyesha. 55Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema ‘Kutakuwa na joto,’ na ndivyo inavyokuwa. 56Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia hali ya nchi na anga; kwa nini, basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?
Patana na adui yako
(Mat 5:25-26)
57“Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya? 58Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani. 59Hakika hutatoka huko, nakuambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho.”

Luka12;1-59

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe