Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 16 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 23...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



“Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!

Mathayo 7:15-16

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.

Mathayo 7:17-18

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.

Mathayo 7:19-20

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

 Yesu anapelekwa kwa Pilato


(Mat 27:1-2, 11-14; Marko 15:1-5; Yoh 18:28-38)
1Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato. 2Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.” 3Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.” 4Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.” 5Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.”
Yesu anapelekwa kwa Herode
6Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?” 7Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
8Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza. 9Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno. 10Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana. 11Basi, Herode pamoja na askari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato. 12Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki.
Yesu anahukumiwa kuuwa
(Mat 27:15-26; Marko 15:6-15; Yoh 18:39–19:16)
13Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu, 14akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake. 15Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo. 16Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.” [ 17Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.]
18Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!” ( 19Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena; 21lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!” 22Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya ubaya gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
23Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda. 24Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe. 25Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa kusababisha uasi na mauaji; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
Yesu anasulubiwa
(Mat 27:32-44; Marko 15:21-32; Yoh 19:17-27)
26Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. 27Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. 28Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. 29Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: ‘Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!’ 30Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: ‘Tuangukieni!’ Na vilima, ‘Tufunikeni!’ 31Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?”
32Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. 33Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. 34Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. 35Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!” 36Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki 37wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
38Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”
39Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.” 40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo. 41Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.” 42Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” 43Yesu akamjibu, “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.”
Yesu anakufa msalabani
(Mat 27:45-56; Marko 15:33-41; Yoh 19:28-30)
44Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa, 45na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili. 46Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
47Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.” 48Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. 49Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
Yesu anazikwa
(Mat 27:57-61; Marko 15:42-47; Yoh 19:38-42)
50Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika. 51Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao. 52Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. 53Kisha akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika. 54Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza.
55Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa. 56Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi ya kuupaka mwili wa Yesu.
Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.

Luka23;1-56
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Friday, 13 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 22...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.

Mathayo 7:13

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.

Mathayo 7:14

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.





Mpango wa kumwua Yesu
(Mat 26:1-5; Marko 14:1-2; Yoh 11:45-53)
1Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. 2Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu.
Yuda anakubali kumsaliti Yesu
(Mat 26:14-16; Marko 14:10-11)
3Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. 4Yuda akaenda, akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. 5Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. 6Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua.
Maandalio ya karamu ya Pasaka
(Mat 26:17-25; Marko 14:12-21; Yoh 13:21-30)
7Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa. 8Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.” 9Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?” 10Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. 11Mwambieni mwenye nyumba: ‘Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ 12Naye atawaonesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.” 13Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
Karamu ya Bwana
(Mat 26:26-30; Marko 14:22-26; 1Kor 11:23-25)
14Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. 15Akawaambia, “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika ufalme wa Mungu.”
17Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akasema, “Pokeeni, mgawane. 18Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” 20Akafanya vivyo hivyo na kikombe cha divai baada ya chakula, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.22:19b-20 Huu ni mwili…inayomwagika kwa ajili yenu: Makala nyingine hazina maneno haya ya Yesu.
21“Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. 22Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti.”
23Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo.
Ubishi juu ya ukuu
24Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu kuliko wengine. 25Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. 26Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. 27Kwa maana, ni nani aliye mkuu: Yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi.
28“Nyinyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; 29na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi ufalme, vivyo hivyo nami ninawakabidhi nyinyi ufalme. 30Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
Yesu anabashiri kwamba Petro atamkana
(Mat 26:31-35; Marko 14:27-31; Yoh 13:36-38)
31“Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta nyinyi kama mtu anavyopepeta ngano. 32Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.” 33Naye Petro akamjibu, “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa.” 34Yesu akamjibu, “Nakuambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu.”
Wakati wa hatari
35Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.” 36Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. 37Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.” 38Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”
Yesu anasali bustanini Gethsemane
(Mat 26:36-46; Marko 14:32-42)
39Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata. 40Alipofika huko akawaambia, “Salini, msije mkaingia katika kishawishi.” 41Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali: 42“Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu.” 43Hapo, malaika kutoka mbinguni akamtokea ili kumtia moyo. 44Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.22:43-44 Baadhi ya hati hazina aya hizi.
45Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni. 46Akawaambia, “Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi.”
Yesu anatiwa nguvuni
(Mat 26:47-56; Marko 14:43-50; Yoh 18:3-11)
47Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu. 48Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?” 49Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?” 50Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia. 51Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo, akaliponya.
52Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? 53Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.”
Petro anamkana Yesu
(Mat 26:57-58; Marko 14:53-54,66-72; Yoh 18:12-18,25-27)
54Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali. 55Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja, naye Petro akiwa miongoni mwao. 56Mtumishi mmoja wa kike alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu pia alikuwa pamoja na Yesu.” 57Lakini Petro akakana akisema, “Wee! Simjui mimi.” 58Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, “Wewe ni mmoja wao.” Lakini Petro akajibu “Bwana wee; si mimi!”
59Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, “Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati.” 60Lakini Petro akasema, “Bwana wee; sijui hata unachosema!” Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.
61Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” 62Hapo akatoka nje, akalia sana.
Yesu anadhihakiwa na kupigwa
(Mat 26:67-68; Marko 14:65)
63Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki. 64Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri, tuone!” 65Wakamtolea maneno mengi ya matusi.
Yesu mbele ya Baraza
(Mat 26:59-66; Marko 14:55-64; Yoh 18:19-24)
66Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo. 67Nao wakamwambia, “Tuambie! Je, wewe ndiwe Kristo?” Lakini Yesu akawaambia, “Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki; 68na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu. 69Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenye Nguvu.”

70Hapo wote wakasema, “Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?” Naye akasema, “Nyinyi mnasema kwamba mimi ndiye.” 71Nao wakasema, “Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe.” 

Luka22;1-70

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe