Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 25 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 6...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Onesha fadhili zako za ajabu, uwaokoe kutoka kwa adui zao, wale wanaokimbilia usalama kwako. Unilinde kama mboni ya jicho; unifiche kivulini mwa mabawa yako,

Zaburi 17:7-8

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


mbali na mashambulio ya waovu, mbali na maadui zangu hatari wanaonizunguka. Hao hawana huruma yoyote moyoni; wamejaa maneno ya kujigamba.

Zaburi 17:9-10


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Wananifuatia na kunizunguka; wananivizia waniangushe chini. Wako tayari kunirarua kama simba: Kama mwanasimba aviziavyo mawindo.

Zaburi 17:11-12

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Yesu anawapa chakula watu elfu tano

(Mat 14:13-21; Marko 6:30-44; Luka 9:10-17)
1Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia). 2Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. 3Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. 4Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. 5Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?” 6(Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) 7Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!” 8Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, 9“Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?” 10Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000. 11Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. 12Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.” 13Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. 14Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.” 15Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.
Yesu anatembea juu ya maji
(Mat 14:22-33; Marko 6:45-52)
16Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani, 17wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado. 18Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. 20Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!” 21Basi wakataka kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walikokuwa wanakwenda.
Watu wanamtafuta Yesu
22Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao. 23Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu. 24Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
Yesu mkate wa uhai
25Wale watu walipomkuta Yesu ngambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?” 26Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.” 28Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?” 29Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu mwifanye: Kumwamini yule aliyemtuma.”
30Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani? 31Taz Zab 78:24 Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: ‘Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.’”
32Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.” 34Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.” 35Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe. 36Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. 37Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu, 38kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. 39Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho. 40Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
41Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?” 43Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho. 45Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. 46Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. 47Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele. 48Mimi ni mkate wa uhai. 49Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. 50Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife. 51Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.”
52Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?” 53Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu. 54Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake. 57Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu. 58Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.” 59Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
Maneno yaletayo uhai wa milele
60Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?” 61Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananungunika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka? 62Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza? 63Roho ndiyo iletayo uhai; mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai. 64Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti). 65Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.”
66Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena. 67Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?” 68Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele. 69Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu” 70Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua nyinyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!” 71Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.

Yohane6;1-71
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Tuesday, 24 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 5...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Ee Mwenyezi-Mungu usikie kisa changu cha haki, usikilize kilio changu, uitegee sikio sala yangu isiyo na hila. Haki yangu na ije kutoka kwako, kwani wewe wajua jambo lililo la haki.

Zaburi 17:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Wewe wajua kabisa moyo wangu; umenijia usiku, kunichunguza, umenitia katika jaribio; hukuona uovu ndani yangu, sikutamka kitu kisichofaa. Kuhusu matendo watendayo watu; mimi nimeitii amri yako, nimeepa njia ya wadhalimu.

Zaburi 17:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Nimefuata daima njia yako; wala sijateleza kamwe. Nakuita, ee Mungu, kwani wewe wanijibu; unitegee sikio, uyasikie maneno yangu.

Zaburi 17:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Yesu anamponya mtu karibu na bwawa la maji

1Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu. 2Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao. 3Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: Vipofu, viwete na waliopooza. [Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe, 4maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.] 5Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. 6Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo na kujua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?” 7Naye akajibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.” 8Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.” 9Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato. 10Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako.”
11Lakini yeye akawaambia, “Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee.’” 12Nao wakamwuliza, “Huyo mtu aliyekuambia: ‘Chukua mkeka wako, utembee,’ ni nani?” 13Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu. 14Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa hekaluni, akamwambia, “Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi.” 15Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.
16Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu. 17Basi, Yesu akawaambia, “Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi.”
18Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumuua Yesu; si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
Mamlaka ya Mwana wa Mungu
19Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile. 20Baba ampenda Mwana, na humwonesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu. 21Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda. 22Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana, 23ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
24“Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai. 25Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi. 26Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai. 27Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu. 28Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, 29nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
Mashahidi wa Yesu
30“Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. 31Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. 32Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. 33Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. 34Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. 35Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. 36Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. 37Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, 38na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. 39Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! 40Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai.
41“Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. 42Lakini nawajua nyinyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. 44Mwawezaje kuamini, hali nyinyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu nyinyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? 45Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye nyinyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. 46Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia, maana Mose aliandika juu yangu. 47Lakini hamyaamini yale aliyoandika; mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?”


Yohane5;1-47
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe