|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima, afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni Neema yako yatutosha Mungu wetu..
Hufikiria kununua shamba, kisha hulinunua, na kulima zabibu kwa faida ya jasho lake. Huwa tayari kufanya kazi kwa nguvu na kuiimarisha mikono yake. Methali 31:16-17 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti, Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Hutambua kwamba shughuli zake zina faida; hufanya kazi hata usiku kwa mwanga wa taa yake. Husokota nyuzi kwa mikono yake mwenyewe, kwa vidole vyake mwenyewe husuka nguo zake. Methali 31:18-19 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Huufungua mkono wake kuwapa maskini, hunyosha mkono kuwasaidia fukara. Hawahofii watu wake ijapo baridi ya kipupwe, maana kila mmoja anazo nguo za kutosha. Methali 31:20-21 Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina....!!!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukae nanyi daima.... Nawapenda.
|
|
Yesu anapakwa marashi
(Mat 26:6-13; Marko 14:3-9)
1Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. 2Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. 3Basi, Maria alichukua nusu lita ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. 4Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, 5“Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari 300, wakapewa maskini?” 6Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. 7Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. 8Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.”
Njama za kumwua Lazaro
9Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu. 10Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, 11maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mat 21:1-11; Marko 11:1-11; Luka 19:28-40)
12Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. 13Taz Zab 118:25,26 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema:
“Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.
Abarikiwe mfalme wa Israeli.”
14Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
15“Usiogope mji wa Siyoni!
Tazama, Mfalme wako anakuja,
amepanda mwanapunda!”
16Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
17Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia. 18Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. 19Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”
Wagiriki kadhaa wanataka kumwona Yesu
20Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. 21Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.” 22Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. 23Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! 24Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. 25Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele. 26Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
Yesu anasema juu ya kifo chake
27“Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii. 28Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.”
29Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!” 30Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. 31Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. 32Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.” 33(Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani).
34 Taz Zab 110:4 Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?” 35Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. 36Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
Watu hawana imani
37Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. 38Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia:
“Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu?
Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?”
39Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena:
40“Mungu ameyapofusha macho yao,
amezipumbaza akili zao;
wasione kwa macho yao,
wasielewe kwa akili zao;
wala wasinigeukie, asema Bwana,
ili nipate kuwaponya.”
41Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
42Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. 43Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu.
Yesu alikuja kuuokoa ulimwengu
44Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. 45Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. 46Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. 47Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. 48Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. 49Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. 50Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.”
Yohane12;1-50
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe