|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu katika yote....
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo... Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...
|
Fadhili zako zinijie, ee Mwenyezi-Mungu; uniokoe kama ulivyoahidi. Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana, maana mimi nina imani sana na neno lako.
Zaburi 119:41-42 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Unijalie kusema ukweli wako daima, maana tumaini langu liko katika maagizo yako. Nitatii sheria yako daima, nitaishika milele na milele. Nitaishi katika uhuru kamili, maana nazitilia maanani kanuni zako. Zaburi 119:43-45 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Nitawatangazia wafalme maamuzi yako, wala sitaona aibu. Furaha yangu ni kuzitii amri zako, ambazo mimi nazipenda. Naziheshimu na kuzipenda amri zako; nitayatafakari masharti yako. Zaburi 119:46-48 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
Paulo anajitetea mbele ya Agripa
1Basi, Agripa akamwambia Paulo, “Unaruhusiwa kujitetea.” Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi: 2“Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. 3Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.
4“Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. 5Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali kabisa katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo. 6Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidi babu zetu. 7Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo! 8Kwa nini nyinyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu? 9Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. 10Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. 11Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.
Paulo anaeleza alivyoongoka
(Mate 9:1-19; 22:6-16)
12“Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. 13Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. 14Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng'ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’ 15Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. 16Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha. 17Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. 18Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’
Paulo anaongea juu ya utumishi wake
19“Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni. 20Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. 21Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua. 22Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; 23yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.”
24Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!” 25Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu. 26Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.” 28Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!” 29Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.”
30Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. 31Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.” 32Naye Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.”
Matendo26;1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe