Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima, afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni Neema yako yatutosha Mungu wetu..
Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwanga katika njia yangu. Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu, kwamba nitashika maagizo yako adili. Zaburi 119:105-106 |
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti, Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Ee Mwenyezi-Mungu, ninateseka mno; unijalie uhai kama ulivyoahidi. Ee Mwenyezi-Mungu, upokee sala yangu ya shukrani; na kunifundisha maagizo yako. Maisha yangu yamo hatarini daima, lakini siisahau sheria yako. Zaburi 119:107-109 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Waovu wamenitegea mitego, lakini sikiuki kanuni zako. Maamuzi yako ni riziki kubwa kwangu milele; hayo ni furaha ya moyo wangu. Nimekusudia kwa moyo wote kufuata masharti yako milele. Zaburi 119:110-112 Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina....!!!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukae nanyi daima.... Nawapenda. |
|
Kielelezo kutokana na maisha ya ndoa
1Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. 2Mathalani: Mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuwa hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. 3Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi. 4Hali kadhalika nyinyi ndugu zangu: Nyinyi pia mmekufa kuhusu sheria kwa kuwa nyinyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu. 5Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo. 6Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya sheria iliyoandikwa.
Sheria na dhambi
7Je, tuseme basi, kwamba sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama sheria isingalikuwa imesema: “Usitamani.” 8Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila sheria dhambi ni kitu kilichokufa. 9Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka, 10nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo. 11Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua.
12Basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri. 13Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Ilivyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno.
Vita ndani ya mtu
14Tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi. 15Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachokichukia ndicho nikifanyacho. 16Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile sheria ni nzuri. 17Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi inayokaa ndani yangu. 18Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza. 19Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka. 20Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
21Basi, nimegundua kanuni hii: Ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua. 22Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu. 23Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu. 24Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka mwili huu unaonipeleka kifoni? 25Shukrani kwa Mungu afanyaye hivyo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Hii basi, ndiyo hali yangu: Mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu ninaitumikia sheria ya dhambi.
Waroma7;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe