|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Waroma" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Wakorintho" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe; mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu; ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni.
Methali 18:7-8
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Mtu mvivu kazini mwake ni ndugu yake mharibifu. Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara; mwadilifu huukimbilia akawa salama. Methali 18:9-10 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake; anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda. Majivuno ya moyoni huleta maangamizi, lakini unyenyekevu huleta heshima. Methali 18:11-12 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
1Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene, 2tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Nyinyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia.
3Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
Baraka za Mungu
4Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia nyinyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu. 5Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri. 6Maana ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu, 7hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. 8Yeye atawaimarisheni nyinyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. 9Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.
Mgawanyiko katika jumuiya ya waumini
10Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: Pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja. 11Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu. 12Nataka kusema hivi: Kila mmoja anasema chake: Mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.” 13Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo. 15Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. ( 16Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote). 17Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu, kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe.
Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu
18Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu. 19Maana Maandiko Matakatifu yasema:
“Nitaiharibu hekima yao wenye hekima,
na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali.”
20Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu.
21Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. 22Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; 23lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; 24lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu.
26Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: Wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu. 27Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. 28Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. 29Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu. 30Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha nyinyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa. 31Basi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Mwenye kutaka kujivuna,
na ajivunie kazi ya Bwana.”
Wakorintho1;1-31
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe