Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "1Wakorintho" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"2Wakorintho" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya. Hesabu 22:32 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.” Hesabu 22:33 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.” Hesabu 22:34 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda.
|
|
1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya. 2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Shukrani kwa Mungu
3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. 4Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. 5Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye. 6Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji nyinyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi. 7Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.
8Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi. 9Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe. 10Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena, 11nyinyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.
Badiliko katika safari ya Paulo
12Sisi tunajivunia kitu kimoja: Dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali na neema ya Mungu. 13Tunawaandikia nyinyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa, 14maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea nyinyi fahari.
15Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu. 16Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea. 17Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema “Ndiyo” na “Siyo” papo hapo? 18Mungu ni ukweli tupu; basi, kile tulichowaambia nyinyi si jambo la “Ndiyo” na “Siyo”. 19Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa “Ndiyo” na “Siyo;” bali yeye daima ni “Ndiyo” ya Mungu. 20Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa “Ndiyo”. Kwa sababu hiyo, “Amina” yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. 21Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na nyinyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; 22ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
23Mungu ndiye shahidi wangu; yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho kwa sababu tu ya kuwahurumieni. 24Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; nyinyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.
2Wakorintho1;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe