|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu katika yote....
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo... Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...
Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’ “Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Matendo 4:26-27 |
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Matendo 4:28-29 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga. Matendo 4:30-31 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Unyenyekevu na ukuu wa Kristo
1Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi? 2Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. 3Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. 4Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake. 5Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu:
6Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu;
lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu
ni kitu cha kungangania kwa nguvu.
7Bali, kwa hiari yake mwenyewe,
aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi,
akawa sawa na wanadamu,
akaonekana kama wanadamu.
8Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa,
hata kufa msalabani.
9Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa,
akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.
10Ili kwa heshima ya jina la Yesu,
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,
vipige magoti mbele yake,
11na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
Mwanga kwa ulimwengu
12Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu, 13kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
14Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi, 15ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga, 16mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure.
17Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo. 18Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu.
Timotheo na Epafrodito
19Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu. 20Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo. 21Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo. 22Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili. 23Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea. 24Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni.
25Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu. 26Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa. 27Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi. 28Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke. 29Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye, 30kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe.
Wafilipi2;1-30
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe