Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "3Yahane" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Yuda" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao. Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana. Waebrania 11:1-3 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
Kwa imani Abeli alimtolea Mungu tambiko iliyokuwa bora kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa alikufa, bado ananena. Waebrania 11:4 Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu. Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta. Waebrania 11:5-6 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
|
|
|
1Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo, nawaandikia nyinyi mlioitwa na Mungu na ambao mnapendwa naye Mungu Baba, na kuwekwa salama kwa ajili ya Yesu Kristo.
2Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
Waalimu wa uongo
3Ndugu wapenzi, nilikuwa na mpango wa kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, lakini nimeona lazima ya kuwaandikieni nikiwahimizeni mwendelee na juhudi kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote. 4Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake Kiongozi na Bwana wetu. Lakini, Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu zamani hukumu inayowangojea watu hao.
5Sasa nataka kuwakumbusheni mambo fulani, ingawaje haya mlikwisha fahamishwa kikamilifu mara moja: Kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe siku ile kuu. 7Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote.
8Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. 9Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.” 10Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili. 11Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. 12Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo. Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa. 13Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu.
14Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu 15kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.
Maonyo na maagizo
17Lakini nyinyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo. 18Waliwaambieni: “Siku za mwisho, watatokea watu watakaowadhihaki nyinyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.” 19Hao ndio wanaosababisha mafarakano, watu wa fikira za kidunia, wasio na Roho wa Mungu. 20Lakini nyinyi, wapenzi wangu, jijengeni wenyewe juu ya imani yenu takatifu kabisa. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, 21na kudumu katika upendo wa Mungu, mkimngojea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye, kwa huruma yake, atawajalieni uhai wa milele.
22Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka; 23waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni. Lakini kwa wengine muwe na huruma pamoja na tahadhari, mkichukia hata mavazi yao yenye madoa ya tamaa zao mbaya.
Sala ya sifa
24Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, 25kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.
Yuda1;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe