Tuesday, 3 January 2012
Sunday, 1 January 2012
Saturday, 31 December 2011
Hotuba ya Mwaka Mpya 2011 ya Rais Jakaya Kikwete!!!!!!
Ahsante Michuzi Blog.
SALAM ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE!!!!!
SALAM ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2011
Ndugu Wananchi;
Leo
tunauaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka 2012. Naungana nanyi
Watanzania wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na
bahati ya kuiona siku ya leo. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi
ambao hawakujaaliwa kuwa nasi kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki.
Tuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema na sisi
tuendelee kumuomba Mola wetu atujaalie rehema na neema tele katika mwaka
ujao.
Mapitio ya Mwaka 2011 na Matarajio kwa Mwaka 2012
Miaka 50 ya Uhuru
Ndugu wananchi;
Mwaka
2011 ulikuwa mwaka wa aina yake na wa kihistoria kwa nchi yetu na wenye
mchanganyiko wa mambo. Kulikuwa na matukio ya furaha na majonzi na
ulikuwa mwaka tuliopata mafanikio mengi na changamoto mbalimbali.
Tumeweza kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa heshima
stahiki kama nilivyoelekeza katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na
kuukaribisha mwaka 2011. Tumezitumia vizuri sherehe hizo kufanya
tathmini ya maendeleo tuliyoyapata tangu Uhuru mpaka hapa tulipo sasa
pamoja na kutambua changamoto zilizo mbele yetu.
Hakika
tumepata mafanikio makubwa sana katika miaka 50 hii ya Uhuru wetu
kuliko yale yaliyopatikana katika miaka 77 ya ukoloni wa Wajerumani
(miaka 34) na Waingereza (miaka 43). Pamoja na mafanikio hayo
tuliyoyapata bado nchi yetu ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani
hivyo bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya mbele yetu. Katika
tathmini iliyofanywa na kila Wizara na Idara za Serikali, mambo
yanayostahili kufanyika miaka ijayo pamoja na mikakati ya kufikia
malengo hayo, yameainishwa vizuri.
Mpango wa Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Bahati
nzuri, mambo yote yaliyoainishwa kufanywa yanakuwa sehemu ya mambo ya
kutekelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 mpaka
2015/2016. Kama mtakavyokumbuka miongoni mwa matukio muhimu katika
mwaka 2011 ni kukamilika kwa kazi ya kufanya tathmini ya kuhuisha Dira
ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na kutengenezwa kwa Mpango wa Kwanza
wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutekeleza Dira hiyo. Tumejipanga
vizuri kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika Bajeti
ijayo. Pia nimeunda Kikundi Kazi kinachoongozwa na Prof. Benno Ndulu
cha kushauri juu ya vipaumbele na kufuatilia utekelezaji wa Mpango huo.
Ndugu Wananchi;
Kwa
mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Watanzania
wenzangu wote kwa jinsi tulivyosherehekea miaka 50 ya kuzaliwa kwa taifa
huru la Tanganyika ambalo sasa ni Tanzania Bara. Tumeikumbuka na
kuitukuza ipasavyo siku hii maalum na adhimu kwa nchi yetu. Nawapongeza
sana wale wote waliofanya kazi kubwa ya maandalizi ya sherehe zile
pamoja na wananchi walioshiriki. Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu
katika ngazi yake na dhamana yake atafanya tathmini ya jinsi mambo
yalivyokuwa katika maeneo yake ili kujua mafunzo gani amepata. Lengo ni
kutambua maeneo ya udhaifu kwa nia ya kurekebisha kasoro zilizopo na
yale waliyofanya vizuri kwa nia ya kuimarisha zaidi.
Mchakato wa Katiba
Ndugu Wananchi;
Tukio
lingine la kihistoria lililotokea mwaka huu tunaoumaliza leo ni kuanza
kwa mchakato wa kupata Katiba mpya ya nchi yetu. Kama mnavyokumbuka,
katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011,
niliahidi kwamba tutaanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi
yetu kwa lengo la kuihuisha, ili hatimaye tuwe na Katiba inayoendana na
taifa lenye umri wa nusu karne. Azma yetu ni kuwa tusherehekee miaka 50
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tukiwa na Katiba mpya
itakayotumika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kama
mnavyofahamu nyote, katika Bunge la Aprili, 2011, Serikali iliwasilisha
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (2011). Tarehe 18 Novemba,
2011 Bunge liliupitisha Mswada huo na mimi nikatia saini na kuwa Sheria
tarehe 29 Novemba, 2011. Sheria hiyo sasa ndiyo inayotoa mwongozo wa
namna mchakato wa kupata Katiba mpya utakavyoendeshwa.
Ndugu Wananchi;
Sheria
hiyo imeainisha utaratibu wa uundwaji wa Tume ya Kukusanya Maoni ya
wananchi wote na jinsi itakavyofanya kazi yake. Aidha, inaelezea
namna ya kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba lenye uwakilishi mpana zaidi
kuliko Bunge la sasa la Jamhuri ya Muungano. Kazi ya Bunge hilo
itakuwa ni kupokea na kujadili Rasimu ya Katiba itakayotayarishwa na
Tume ya Katiba. Baada ya Bunge kujadili Rasimu hiyo na kufanya uamuzi
wake, Rasimu ya Katiba itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa
njia ya kura ya maoni. Sheria, pia, inaelekeza namna kura ya maoni ya
wananchi itakavyoendeshwa na hatimaye kupata Katiba mpya.
Ndugu Wananchi;
Sote
tunafahamu maoni mbalimbali na mjadala mkali uliokuwepo baada ya mimi
kueleza dhamira yangu ya kuanzisha mchakato wa kufanya mabadiliko ya
Katiba yetu wakati Muswada ulipokuwa Bungeni na hata baada ya kupitishwa
na kusainiwa kuwa Sheria. Kwa kutambua wajibu wa kusikiliza maoni ya
wadau, sikusita kukubali maombi ya kukutana na viongozi wa CHADEMA, CUF
na NCCR na Shirikisho la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali. Tulikuwa
na mazungumzo mazuri na viongozi wa CHADEMA, CUF na tulielewana juu ya
namna ya kushughulikia hatua zinazofuata katika mchakato huu.
Nitakutana na viongozi wa NCCR mapema mwezi Januari, 2012.
Napenda
kuwahakikishia Watanzania wenzangu wote kuwa niko tayari kukutana na
kuzungumza na wadau wowote na kupokea mawazo mema ya kuboresha mchakato
wetu huu muhimu. Dhamira yangu na ya wenzangu Serikalini ni kuhakikisha
kuwa tunakuwa na mchakato mzuri ili hatimaye tupate Katiba iliyo nzuri;
Katiba ambayo italilea taifa letu kwa miaka 50 ijayo likiwa na amani,
utulivu, demokrasia na maendeleo makubwa zaidi.
Ndugu Wananchi;
Ni
matarajio yangu kuwa ndani ya robo ya kwanza ya mwaka ujao uundaji wa
Tume ya Katiba utakuwa umekamilika. Katika robo ya pili au ya tatu ya
mwaka 2012, Tume hiyo itaanza kazi yake ya kukusanya maoni. Napenda
kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu wote mjiandae kushiriki
kwa ukamilifu kutoa maoni yenu kwenye Tume ya Katiba. Aidha, niwaombe,
ndugu zangu, tujiepushe na vitendo vya kuzuia watu kutoa maoni yao kwa
uhuru hasa wale wenye maoni tofauti na yetu. Kutoa maoni katika Tume
hiyo ni haki ya kila mwananchi.
Iwe
ni mwiko kwa mtu yoyote au kikundi chochote kumzuia mtu au watu wowote
kutumia haki yao hiyo. Iwe ni mwiko pia kwa mtu, watu au taasisi yoyote
kujaribu kuhodhi mijadala hiyo. Ni vyema tukajua kuwa tunatengeneza
Katiba ya watu wote na kwa maslahi yetu sote. Hatutengenezi Katiba ya
watu fulani wateule au kikundi fulani cha kisiasa au kijamii kwa maslahi
yao. Tuwaache watu watoe maoni yao kwa uhuru ili tupate Katiba ya watu
wote.
Hali ya Usalama Nchini
Uharamia Baharini
Ndugu Wananchi;
Hali
ya usalama wa nchi yetu katika mwaka 2011 ilikuwa ya kuridhisha na
Tanzania iliendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu. Kwa jumla, mipaka
yetu yote ilikuwa salama isipokuwa ule wa majini kwa upande wa Bahari
Kuu ya Hindi ambako kumekuwepo na matukio ya uharamia. Katika mwaka huu
tunaoumaliza leo, kumekuwepo na majaribio tisa ya kuteka meli ndani ya
mipaka yetu katika Bahari Kuu hiyo. Bahati nzuri hakuna hata moja
lililofanikiwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi letu la
Wanamaji. Maharamia saba wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani ambako
kesi zao zinaendelea.
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Jeshi letu la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea
kuifanya ya kupambana na maharamia katika Bahari Kuu ya Hindi. Kutokana
na juhudi zao hizo matukio ya kujaribu utekaji meli yamepungua mwaka
huu ikilinganishwa na mwaka jana ambapo kulikuwa na matukio 30.
Ndugu Wananchi;
Natambua
kuwepo kwa mahitaji kadhaa kwa Jeshi letu na wanajeshi wetu ili
kuimarisha ulinzi katika mipaka yetu ya majini katika Bahari Kuu ya
Hindi na katika maziwa yetu makuu ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.
Tumekwishaanza kuchukua hatua muafaka kwa ajili hiyo na tutaendelea nazo
kwa kasi zaidi katika mwaka 2012 na kuendelea.
Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Juhudi
za kupambana na kudhibiti uhalifu nchini ziliendelea na mafanikio
yameendelea kupatikana. Taarifa za Jeshi la Polisi za kati ya Januari
na Novemba, 2011 zinaonesha kuwa matukio ya makosa makubwa ya jinai
yamepungua ukilinganisha na hali ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka
2010. Makosa hayo yamepungua kutoka 86,150 hadi 69,678 na punguzo kubwa
zaidi limetokana na kupungua sana kwa makosa ya wizi, pamoja na yale ya
kubaka, kunajisi, kutupa watoto, unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma
nyumba, na dawa za kulevya.
Ndugu Wananchi;
Mafanikio
haya ya kutia moyo ni uthibitisho wa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la
Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama. Tutaendeleza juhudi za kuliwezesha Jeshi hilo kwa zana, vifaa,
mafunzo, maslahi na mazingira ya kazi na ya kuishi katika mwaka 2012 na
miaka ijayo ili ufanisi mkubwa zaidi upatikane katika kupambana na
uhalifu nchini.
Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa ajali za barabarani, matukio yamepungua kutoka 22,440 mwaka
2010 hadi 22,000 mwaka 2011. Hata hivyo, ajali zilizosababisha watu
kupoteza maisha ziliongezeka mwaka huu kuliko mwaka wa jana. Mwaka jana
ajali hizo zilikuwa 2,833 ukilinganisha na 3,012 mwaka 2011 na watu
waliopoteza maisha walikuwa 3,332 ukilinganisha na 3,707 mwaka 2011.
Ongezeko
la ajali barabarani linasababishwa na ongezeko kubwa la vyombo vya
usafiri hasa magari na pikipiki. Katika miaka sita iliyopita, magari
514,136 na pikipiki 1,206,679 zimeinginzwa nchini. Sababu nyingine ni
madereva kutokuwa makini katika uendeshaji ama kwa sababu ya ujuzi mdogo
au uzembe na ulevi. Mimi naamini kuwa tatizo hili litapungua sana kama
madereva wataacha uzembe, ulevi na kuheshimu sheria za usalama
barabarani.
Aidha,
nirudie kuwataka ndugu zetu wa Polisi wanaosimamia sheria ya usalama
barabarani, kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo na wale
wote wanaotumia barabara, yaani vyombo vya usafiri na watu.
Ajali ya Mabomu, Meli na Mafuriko
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2011 licha ya ajali barabarani, kulitokea ajali ya kulipuka
mabomu katika kambi ya Jeshi Gongolamboto, ajali ya kuzama kwa meli ya
Spice Islander huko Zanzibar na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam.
Matukio hayo yamesababisha ndugu zetu wengi kupoteza maisha, wengine
kujeruhiwa na mali nyingi kupotea.
Milipuko ya Mabomu
Katika
ajali ya Gongolamboto watu 25 walifariki dunia na 512 walijeruhiwa na
nyumba 1,791 ziliharibiwa kwa viwango mbalimbali. Nimearifiwa kuwa
shilingi 817,740,849 zimelipwa kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa
nyumba zao zilizoharibiwa. Bahati mbaya kwa wale ambao nyumba zao
ziliharibiwa sana na kulazimika kujengwa upya kazi hiyo imechelewa sana
kuanza kwa sababu za urasimu wa kupata viwanja.
Nimemuagiza
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ahakikishe kuwa wahusika katika Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Manispaa ya Ilala wanaacha
urasimu na kuharakisha upatikanaji wa viwanja ili kazi ya ujenzi ianze.
Aidha, nimewaomba viongozi wa Wizara ya Ulinzi, JWTZ na hasa JKT
kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi itakapoanza inakamilika mapema
iwezekanavyo.
MV Spice Islander
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa ajali ya MV Spice Islander iliyotokea Septemba 10, 2011 ndugu
zetu 619 waliokolewa na maiti 203 zilipatikana. Mali iliyokuwa ndani
ya meli hiyo haikuweza kuokolewa hivyo haikuweza kujulikana kama wapo
watu wengine waliokuwa wamezama na meli hiyo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein aliunda Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo. Tume hiyo
imekamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake Serikalini. Hivi sasa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaitafakari taarifa hiyo kwa lengo la
kuchukua hatua muafaka. Subira yavuta heri.
Mafuriko ya Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Kutokana
na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia usiku wa kuamkia tarehe 20 mpaka
tarehe 23 Desemba, 2011, Bonde la Mto Msimbazi na maeneo ya jiji
yalikumbwa na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia
ya jiji la Dar es Salaam. Kutokana na mafuriko hayo ndugu zetu 40
wamepoteza maisha na nyumba na mali nyingi zimeharibiwa. Pia, watu
wapatao 5,029 wamekosa makazi na kupatiwa hifadhi na jamaa zao au katika
maeneo yaliyotengwa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam. Aidha,
Serikali imekuwa ikiwahudumia waathirika hao kwa malazi, chakula na
huduma ya afya. Vile vile, watu na mashirika mbalimbali yamekuwa
yanatoa misaada ya kibinadamu kuwasaidia ndugu zetu hao.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
21 Desemba, 2011, niliwatembelea baadhi ya waathirika na kuona athari
za mafuriko katika jiji la Dar es Salaam. Pia nilipata nafasi ya
kupokea taarifa ya maafa hayo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa. Nilielezwa
shughuli za uokoaji, huduma zinazotolewa kwa walioathirika katika makazi
ya muda na mipango ya baadaye kuhusu watu walioathirika na ujenzi wa
makazi katika Bonde la mto Msimbazi na mabonde mengine katika jiji la
Dar es Salaam.
Niliwapa
pole waathirika na kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam
walivyoongoza juhudi za kuokoa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na janga
hili na jinsi wanavyowahudumia. Niliafiki uamuzi wa Mkoa kwamba ndugu
zetu waliojenga na kuishi katika Bonde la Mto Msimbazi wahame. Aidha,
nilikubaliana na uamuzi wao kuwa wale wote waliojenga katika njia za
asili za kupita maji na kuyalazimisha maji kutafuta njia nyingine na
kusababisha madhara pasipostahili nao pia wabomoe. Maji yaachwe yapite
kwenye njia zake za kawaida ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu kuwa ndugu zetu wa Jangwani na kwingineko hawatakaidi
tena amri halali ya mkoa kama walivyofanya miaka ya nyuma. Baada ya
mafuriko ya mwaka 1998, ambapo baadhi ya watu waliokolewa kwa helikopta
kama safari hii, watu waliamriwa kuhama na kugawiwa viwanja vya kujenga
makazi mbadala. Lakini, walikaidi amri na kudiriki kwenda Mahakamani
kuzuia utekelezaji wa amri hiyo. Bahati nzuri walishindwa.
Wahenga
wamesema “asiyesikia la mkuu huvunjika guu”. Mafuriko yametokea tena
mwaka huu, tena mabaya zaidi. Safari hii helikopta hazikutosha bali
boti na vijana hodari wa kuogelea walitumika kuokoa maisha ya watu.
Pamoja na juhudi hizo safari hii ndugu zetu 40 wamepoteza maisha na mali
nyingi zaidi zimepotea na kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Nimewataka
viongozi wa Serikali na Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam washikilie
msimamo wao huo huo. Watu watakaokaidi wasiachwe kuendelea kuishi
mabondeni. Tukikubali wabaki, sote, yaani watu wenyewe na Serikali,
hatutaeleweka. Tena tutachekwa na kulaumiwa vibaya siku za usoni
mafuriko mengine yatakapotokea na watu kukutwa katika hali kama hii na
Serikali kujikuta inarudia tena kufanya kazi ya kuokoa watu.
Bahati
nzuri maeneo ya kuhamia yametambuliwa na viwanja vimeshaanza kugawiwa.
Kila mwenye nyumba atapewa na naomba hata wapangaji wapewe iwapo
viwanja vitasalia. Hivyo, narudia kuwataka ndugu zetu kuhama kwa hiari
yao na wale watakaokaidi wahamishwe bila ya ajizi kwa mujibu wa taratibu
zilizowekwa.
Uchumi na Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa uchumi, mwaka 2011 ulikuwa na changamoto nyingi. Kulikuwa na
mchanganyiko wa ukame, uhaba mkubwa wa umeme, upungufu wa chakula
kwenye baadhi ya maeneo nchini, kupanda kwa bei za mafuta na vyakula,
kushuka kwa thamani ya shilingi, mfumuko wa bei kupanda na sasa mvua
nyingi na athari zake. Pamoja na changamoto hizo tunatarajia uchumi
wetu utakua kwa asilimia 7 ingawaje wenzetu wa IMF wanakadiria kuwa
utakua kwa asilimia 6.3. Hata kwa kiwango hicho bado nchi yetu inabakia
kuwa miongoni mwa nchi 20 duniani zinazoongoza kwa ukuaji wa uchumi.
Ni dhahiri basi kuwa kama athari hizo zisingekuwepo hali ya uchumi wetu
ingekuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi;
Tulianza
mwaka 2011 kukiwa na ukame mkali uliokumba maeneo mengi nchini.
Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha
mwaka 2011 nililizungumzia suala la uhaba wa mvua na ukame na kutaka
tuombe mvua za masika ziwe nzuri. Mvua hazikuwa nyingi na mtawanyiko
wake haukuwa mzuri. Maeneo mengi mvua zilikuwa chini ya wastani. Kwa
sababu hiyo watu 423,530 katika Halmashauri 36 za mikoa 13 walikumbwa
na upungufu wa chakula na kuilazimisha Serikali kutoa msaada wa chakula.
Aidha,
kwa sababu ya upungufu huo, bei za vyakula zilipanda sana hasa mijini.
Ili kukabiliana na hali hiyo niliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula kuanza utaratibu wa kuuza mahindi kwa wafanyabiashara wa mijini
ili kusaidia kupunguza bei ya chakula. Agizo langu hilo sasa ni sehemu
ya sera ya Taasisi hiyo itakayotekelezwa kila mwaka wakati chakula
kutoka mashambani kitakapopungua katika masoko ya mijini.
Ndugu Wananchi;
Ukame
huo pia ukasababisha kupungua sana kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha
umeme na hivyo kuliingiza taifa katika tatizo kubwa la upungufu wa
umeme. Ili kukabiliana na tatizo hilo TANESCO imelazimika kuingia
mikataba na makampuni ya kuzalisha umeme kwa malipo. Kwa vile gesi
inayozalishwa hivi sasa kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kufulia umeme
iliyopo Ubungo haitoshelezi mahitaji ya taifa, makampuni hayo
yamelazimika kutumia mitambo inayotumia mafuta.
Mitambo
hiyo imepatikana na tayari inazalisha umeme. Ndiyo maana mgao sasa
haupo. Lakini, kwa sababu ya kutumia mafuta, umeme huu ni ghali na
umekuwa mzigo mkubwa wa gharama kwa TANESCO. Kutokana na sababu hizo,
TANESCO wamepeleka maombi EWURA ya kutaka kuongeza bei ya umeme.
Ndugu Wananchi;
Tunamshukuru
sana Mwenyezi Mungu kwamba tunaumaliza mwaka huu na kuuanza mwaka 2012
kukiwa na mvua nzuri karibu nchi nzima. Dua zetu mwaka huu ni kuomba
mvua za kiasi kwani sehemu nyingine mvua zimezidi kipimo. Zimesababisha
mafuriko, vifo vya watu, mali pamoja na miundombinu ya babara
kuharibika. Katika baadhi ya maeneo mazao mashambani hasa mahindi
yanaathirika kwa maji kuzidi. Kwa muelekeo huu wa mvua na hasa kama
mvua za masika nazo zitakuwa nzuri mwaka 2012 kutakuwa na chakula kingi
nchini karibu maeneo yote.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya ukame wa mwaka 2006 na upungufu mkubwa wa umeme wa tangu wakati huo
mpaka mwaka 2008, tulitoa ahadi ya kuchukua hatua za makusudi za
kupunguza utegemezi mkubwa wa kupita kiasi wa umeme wa nguvu ya maji.
Nilisema kuwa tutaanza juhudi za kuendeleza vyanzo vingine vya nishati
hasa gesi asilia na makaa ya mawe mpaka tufikie mahali ambapo hata kama
maji hayatoshi katika mabwawa ya vituo vya umeme, nchi haitakosa umeme.
Tumeendelea
kutekeleza uamuzi ule wa busara. Mpaka sasa Serikali kupitia TANESCO
imeshaongeza MW 245 za umeme unatokana na gesi asilia. Nyongeza hiyo
ingeweza kuwa kubwa zaidi lakini hakuna gesi ya kutosha kutoka Songo
Songo. Bahati mbaya mchakato wa kuongeza gesi umechelewa kwa karibu
miaka miwili, lakini mwelekeo sasa mzuri.
Ndugu Wananchi;
Maombi
yetu kwa Serikali ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la
kusafirisha gesi kutoka Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka
Songo Songo yamekubaliwa. Utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi
18 na gesi itakayoletwa inaweza kuzalisha mpaka Megawati 3,000 za umeme.
Baada ya hapo kasi ya kuongeza umeme itakuwa kubwa zaidi na tatizo la
upungufu wa umeme linaweza kuwa historia.
Bahati
nzuri wawekezaji wa kuzalisha umeme kutumia gesi hiyo wapo,
wanachosubiri ni gesi kufika. Wakati huo huo michakato ya kuzalisha
umeme kutokana na makaa ya mawe ya Ngaka, Kiwira na Mchuchuma imeanza na
ipo katika hatua mbalimbali. Pia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
nguvu ya upepo unaendelea vizuri.
Matatizo ya Bei ya Mafuta
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2011 bei ya mafuta iliendelea kuwa tatizo. Tatizo hilo lilikuwa
na sura ya ndani na ya nje. Bei ya mafuta katika soko la dunia ilipanda
kutoka dola za Marekani 76.1 kwa pipa mwezi Septemba, 2010 hadi dola
100.5 Septemba, 2011 na dola 99.92 jana tarehe 30 Desemba, 2011. Kwa
vile mafuta yanagusa takriban nyanja zote za uchumi na maisha ya
Watanzania nyongeza ya asilimia 45 ya bei za mafuta imesababisha kupanda
kwa gharama ya huduma na bidhaa nyingi hivyo kuongezeka gharama ya
maisha kwa watu.
Ndugu Wananchi;
Hapa
kwetu makali ya ongezeko la bei ya mafuta duniani yaliongezwa na
kushuka thamani ya shilingi na vitendo vya wafanyabiashara ya mafuta.
Thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilishuka kutoka wastani wa
shilingi 1,500 kwa dola ya Kimarekani mwanzoni mwa Januari, 2011 hadi
shilingi 1,815 kwa dola tarehe 27 Oktoba, 2011. Serikali kupitia Benki
Kuu ilichukua hatua mbalimbali zilizoweza kupunguza kasi ya kushuka kwa
thamani ya shilingi hadi wastani wa shilingi 1,595 kwa dola hivi sasa.
Kwa
sababu ya shilingi kupungua thamani, waagizaji wa mafuta walilazimika
kutumia pesa nyingi za Kitanzania kununua dola ambazo kabla ya hapo
walitumia pesa kidogo kuzipata. Hali hiyo ndiyo iliyosababisha athari
za kupanda kwa bei za mafuta duniani kuwa kali zaidi hapa nchini.
Sambamba
na hilo, mwenendo wa wafanyabiashara hasa wa kukataa kutii maamuzi ya
EWURA hasa pale wanapoteremsha bei limekuwa tatizo lingine.
Wafanyabiashara hawako tayari kuona watumiaji wa mafuta wakipata nafuu
hata kidogo. Kila bei zinaposhuka basi watapinga. Ama wataendelea
kuuza kwa bei ya zamani au watasababisha upungufu wa mafuta ili bei
iendelee kuwa juu. Lakini EWURA wanapotangaza kupandisha bei, yote hayo
hayaonekani.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwasihi wafanyabiashara ya mafuta kutoa
ushirikiano kwa EWURA inapotimiza wajibu wake. Ni ukweli ulio wazi kuwa
bei ya mafuta duniani hupanda na kushuka. Kukataa kushusha bei ya
mafuta wakati bei ya dunia inaposhuka ni tamaa ya utajiri iliyovuka
mipaka ya utu. Nawapongeza EWURA kwa msimamo wao na waendelee
kuwawajibisha wanaokaidi. Msirudi nyuma.
Kwa
nia ya kutafuta nafuu ya bei ya mafuta, tumeamua kuanzisha uagizaji wa
pamoja wa mafuta. Lengo ni kupata nafuu ya bei na ya gharama ya
uchukuzi na hivyo kumfanya mtumiaji wa mwisho naye apate nafuu ya bei ya
mafuta. Utaratibu huo utaanza rasmi mwezi Januari, 2012. Tungoje
tuone utakavyopokelewa na wafanyabiashara. Naamini utasaidia, labda
kama utahujumiwa. Naagiza Wizara na Mamlaka husika kuhakikisha kuwa
mpango huu unafanikiwa kama tunavyotarajia.
Kilimo
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kilimo katika mwaka 2011 juhudi za kuleta mageuzi katika
kilimo chetu zinazolenga kuwanufaisha wakulima wadogo zimeendelea
kutekelezwa. Ruzuku ya pembejeo iliendelea kutolewa, maafisa ugani
waliongezwa vijijini na uboreshaji wa masoko na miundombinu vijijini
uliendelea. Juhudi hizo zimeleta matokeo mazuri kwa uzalishaji wa mazao
kuongezeka. Bahati mbaya katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma na
Iringa kumekuwa na usumbufu mkubwa wa ununuzi wa mahindi ya wakulima
katika msimu huu.
Kiini
cha tatizo ni taratibu za kupata fedha za kununulia mahindi
kutokamilika mapema. Nimewaagiza viongozi wa NFRA, Wizara ya Fedha na
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuhakikisha kuwa wakulima ambao
mazao yao yako mikononi mwa NFRA wanalipwa mara moja na usumbufu
uliokuwepo safari hii haujirudii tena mwakani na miaka ijayo. Lazima
taratibu za kupata fedha za kununulia mazao ya wakulima zianze na
kukamilika mapema kabla ya msimu wa ununuzi kuanza. Aidha, nimewataka
wahakikishe kuwa ucheleweshaji wa upatikanaji wa vocha za pembejeo
haujitokezi tena mwakani na miaka ijayo. Kwa sasa njia zitafutwe za
kuhakikisha kuwa wakulima hawakosi pembejeo kwa sababu ya vocha
kuchelewa.
Ndugu Wanananchi;
Vile
vile, nimeelekeza kuwa mwakani uwekwe mfumo mzuri utakaowawezesha
wafanyabiashara binafsi kushiriki mapema katika ununuzi wa mazao ya
wakulima. Pamoja na kuuza sehemu ya mahindi ya NFRA mijini ili kushusha
bei hasa katika kipindi cha upungufu wa mahindi mikononi mwa wakulima,
NFRA itafute namna bora ya kuuza mazao yaliyopo katika maghala yake
mapema kabla ya msimu mpya wa ununuzi haujaanza. Kufanya hivyo kutatoa
nafasi katika maghala ili kutoa nafasi ya kuhifadhi bidhaa za msimu
mpya.
Uwekezaji
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka huu tunaoumaliza leo tulitoa kipaumbele cha juu katika kukuza
uwekezaji nchini na tunakusudia kuendelea kufanya hivyo mwaka ujao.
Tumekuwa tunatangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwashawishi
wawekezaji wa ndani na nje kujitokeza kuja kuwekeza. Pia tumekuwa
tunachukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuifanya
Tanzania kuwa nchi nzuri ya kuwekeza na kufanya biashara.
Tumeainisha
maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji ambayo baadhi yake ni viwanda,
kilimo, madini, utalii, biashara, nishati, uchukuzi na teknohama. Lengo
letu kuu la kuhimiza uwekezaji nchini ni kutaka kuongeza uwezo na kasi
ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kuongeza uzalishaji mali,
kuboresha huduma na kukuza ajira.
Ndugu Wananchi;
Mara
kadhaa unawasikia watu hapa nchini na kwingineko duniani wakiuliza kwa
nini nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo ni maskini wakati rasilimali
zimejaa tele. Moja ya sababu kubwa ni kutokuwepo kwa uwekezaji wa
kutosha wa kuzigeuza rasilimali hizo kuwa bidhaa na huduma za kuuza
katika soko na kuwapatia mapato wamiliki wake watakayoyatumia kuboresha
hali zao za maisha. . Chukua, kwa mfano, mtu mwenye msitu mkubwa na
mzuri anayetaka uwe shamba la kuzalisha mazao yatakayomwezesha kupata
mapato yatakayosaidia kubadili maisha yake. Haitakuwa hivyo mpaka pale
atakapochukua panga na jembe akafyeka na kulima, baadae akachukua mbegu
akapanda, akaweka mbolea, akapalilia, akavuna na kupeleka mazao sokoni
kuuza akapata pesa, atakapozitumia kujipatia mahitaji yake ya maisha.
Kufyeka, kulima, kupanda, kupalilia, kuvuna na kupeleka sokoni ndiyo
uwekezaji.
Ndugu Wananchi;
Ni
kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana sisi katika Serikali
tunahimiza na kuvutia wawekezaji ili nchi itumie fursa zilizopo nchini
kujiletea maendeleo, kupunguza umaskini na kukuza ajira.
Inakadiriwa
kuwa hapa nchini mwaka 2011, kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi
22,152,320 na kati ya watu hao 2,368,672 au sawa na asilimia 10.7 hawana
ajira. Ili watu hao waweze kupata ajira itategemea kwa kiasi gani
tunafanikiwa kukuza uwekezaji katika sekta na shughuli mbalimbali. Bila
ya hivyo kupatikana kwa ajira itakuwa ndoto.
Ndugu Wananchi;
Katika
kuwahamasisha wawekezaji, tunatambua fika umuhimu wa kutoa kipaumbele
kwa wawekezaji wananchi wa Tanzania. Wanahitaji upendeleo maalum na
wanahitaji kuwezeshwa na tumekuwa tunafanya hivyo. Ndiyo maana kuna
maeneo na shughuli zilizotengwa maalum kwa ajili ya wawekezaji wazawa
pekee. Aidha, umewekwa ukomo wa kiwango cha chini cha mtaji ambacho
wawekezaji wageni lazima wawe nacho ili watambuliwe kuwa wawekezaji.
Tusipofanya hivyo uchumi utatawaliwa na wageni.
Lakini
hatukuishia hapo tu, tumelitazama suala la uwezeshaji wa wazawa ili
waweze nao kushiriki katika fursa zilizopo nchini mwao. Tumechukua
hatua za makusudi kufufua Benki ya Rasilimali kwa ajili ya kutoa mikopo
kwa wawekezaji wazawa kwa shughuli za viwanda na biashara. Pia
tunakamilisha mipango ya kuanzisha Benki ya Kilimo kwa ajili ya kutoa
mikopo kwa wakulima wazawa. Benki hizo mbili hazitatoa mikopo kwa
wawekezaji wageni. Aidha, tumeanzisha mpango wa dhamana kwa wauzaji nje
na wenye viwanda vidogo na vya kati, yaani Export Credit Gurantee
Scheme na Small and Medium Enterprises Guarantee Scheme”. Mifuko hiyo
maalum inayosimamiwa na Benki Kuu ipo kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji
wazawa. Mwaka 2011 wananchi wengi walinufaika na Export Credit
Guarantee Scheme kupitia vyama vyao vya ushirika 635 vilivyopatiwa jumla
ya shilingi bilioni 108.67. Aidha, makampuni mengine yalipata jumla ya
shilingi bilioni 24.35. Ni makusudio yetu kuongeza fedha ili makampuni
na na watu wengi wanufaike na fursa hizi.
Uwezeshaji Wajasiriamali Wadogo
Ndugu wananchi;
Tunatambua
kwamba wapo watu wanaopenda kufanya shughuli zao za kujipatia kipato.
Tunatambua pia kwamba si kila mtu atapata nafasi ya kuajiriwa, lakini
wapo wanaoweza kujiajiri kwa maana ya kuwa na shughuli zao za kuwapatia
riziki. Hata hivyo, ili waweze kufanya hivyo wanahitaji kuwa na mtaji,
yaani pesa. Si wengi wanao ndugu au jamaa wa kuwapatia pesa
wanazozihitaji. Pesa za namna hiyo ziko benki ambako kuzipata kwake
kuna masharti magumu, moja likiwa ni dhamana ya kitu kisichoondosheka.
Wengi na hasa vijana hawana dhamana ya namna hiyo.
Ni
kwa nia ya kuwaondoshea kikwazo hicho ili waweza kukopesheka, ndipo
tulipohimiza uanzishaji wa SACCOS na kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi. Ndiyo maana pia kuna Mifuko ya Wanawake na Vijana.
Kwenye Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, tulitenga shilingi
bilioni moja kwa kila Mkoa kwa upande wa Bara na milioni 100 kwa mikoa
ya Zanzibar isipokuwa Mkoa wa Mjini Magharibi uliopata shilingi milioni
200. Pesa hizo zilikopeshwa kupitia Benki za NMB na CRDB kila moja
ikipewa shilingi bilioni 5.5 kwa maelewano kuwa wao watachangia mara
tatu. Pia asasi ndogo za fedha 12 zilipewa jumla ya shilingi bilioni
10.
Ndugu Wananchi;
Tathmini
iliyofanywa na Baraza la Uwezeshaji la Taifa zinaonesha kuwa jumla ya
shilingi bilioni 37.17 zilikopeshwa na benki za NMB na CRDB na jumla ya
shilingi bilioni 12.06 zilikopeshwa na asasi 12 za fedha. Jumla ya
wananchi 72,912 wamenufaika na mikopo hiyo. Kati yao 46,299 ni wanaume
na 36,613 ni wanawake. Mikopo hiyo pia imenufaisha SACCOS 192 na vikundi
vingine 86. Kati ya jumla ya shilingi bilioni 49.23 zilizotolewa kwa
mikopo, shilingi bilioni 39.275 zimesharejeshwa ambazo ni sawa na
asilimia 79.8 ya mikopo iliyotolewa. Kiwango cha urejeshwaji mikopo
kinategemewa kuongezeka kwa vile baadhi ya mikopo iliyotolewa kupitia
asasi ndogo za fedha bado haijaiva.
Ndugu Wananchi;
Tathmini
iliyofanywa inaonyesha pia kwamba yapo mambo mazuri mengi na upungufu
kadhaa. Upungufu uliojitokeza ni pamoja na baadhi ya SACCOS kutoza riba
kubwa kuliko kiwango cha juu kilichowekwa na serikali cha asilimia 12.
Lingine ni kuwa japokuwa vijana ndiyo wanaohitaji uwezeshaji wa
kujiajiri lakini ni asilimia 32.5 tu ya vijana waliokopeshwa. Aidha,
wanawake walikuwa ni asilimia 38.4 tu ya waliokopeshwa.
Baadhi
ya mazuri yaliyojitokeza ni pamoja na: ongezeko la ajira la asilimia
3.8; kuongezeka kwa watu wenye akaunti benki kwani asilimia 33 ya
waliokopeshwa walifungua akaunti kwa mara ya kwanza. Lingine muhimu ni
kupanda hadhi kwa baadhi ya SACCOS, vikundi na watu binafsi
kulikowafanya waweze kupata sifa na nafasi ya kukopeshwa na mabenki.
Urejeshwaji wa mikopo kwa takribani asilimia 80 ni wa kuridhisha japo
ingekuwa bora kiasi chote au hata zaidi ya hapo kitarejeshwa. Hivyo
basi juhudi ziendelee kufanyika katika kurejesha mikopo iliyosalia.
Ndugu Wananchi;
Kwa
ujumla tathmini iliyofanyika inaonesha kuwa mpango huu ni wenye manufaa
na kwamba yafaa tuendelee nao. Pia kwamba tuuongezee uwezo ili
wananchi wengi zaidi wafaidike nao. Serikali inayaafiki mapendekezo hayo
na inayafanyia kazi. Ni makusudio yetu kuwa katika bajeti ijayo
tutatenga fedha zaidi katika Mfuko huu. Tutaendelea kutumia mpango wa
dhamana kwa mabenki ili kuongeza fedha za uwezeshaji. Aidha,
tutauboresha mfuko huu na mingineyo yote ya uwezeshaji kiutendaji na
kifedha ili watu wetu wengi waweze kunufaika nayo. Tutatengeneza mfumo
maalum utakaowawezesha vijana wengi zaidi kunufaika.
Ndugu Wananchi;
Naelewa
kuwa upo utaratibu unaozitaka Halmashauri za Wilaya na Miji kutenga
asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake na
vijana. Utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa ukisuasua. Napenda kutumia
nafasi hii kuzikumbusha Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa
zinatekeleza agizo hilo bila kukosa. Wakuu wa Wilaya wafuatilie
utekelezaji wa agizo hili na watoe taarifa kwa Wakuu wa Mikoa kila miezi
minne ambao nao watatoa taarifa kwa Waziri Mkuu.
Malimbikizo ya Madai ya Watumishi Serikalini
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2011 kero ya malimbikizo ya madai ya stahili mbalimbali za
watumishi wa umma wakiwemo walimu imejirudia tena. Tatizo hili
nililikuta wakati naanza kazi hii na tukafanya jitihada kubwa na kulipa
madeni yote. Baada ya kubaini kuwa limekuwa linajirudiarudia kila baada
ya kipindi kifupi, nilitoa maelekezo kwa Halmashauri za Wilaya na Miji
na Wizara za Serikali kuhakikisha kuwa tatizo hilo linakoma.
Kuhusu
uhamisho nilielekeza kwamba kama Halmashauri au taasisi yoyote ya
Serikali haina pesa za uhamisho, isiwahamishe watumishi wake. Niliagiza
kuwa mtindo wa kuhamisha watumishi bila ya kuwa na fedha za uhamisho
ukomeshwe mara moja. Nilitaka kiongozi au mhusika yeyote atakayekiuka
agizo hili alipishwe yeye gharama za kumhamisha mtumishi huyo. Kuhusu
madai ya likizo nilielekeza kutengwe fedha za kutosha za likizo kwani
mapumziko ni haki na muhimu kwa wafanyakazi. Hata hivyo kama fedha
hakuna si busara kulimbikiza madeni. Uzuri wa likizo ni kuwa hazipotei.
Wakati wa kustaafu siku za likizo ambazo mtumishi hakuchukua hulipwa.
Ndugu Wananchi;
Nilisema
pia kwamba suala la kuwapandisha watumishi vyeo bila kuwarekebishia
mishahara yao kwa wakati ni upungufu wa kiutendaji ambao ni lazima
ukomeshwe mara moja. Kupandishwa watumishi vyeo ni mpango unaoeleweka
na siyo jambo la dharura wala ajali. Kwa mujibu wa utaratibu wa
Serikali, mtumishi hupandishwa cheo kwa misingi miwili. Kwanza,
kutimiza masharti ya muundo wake wa utumishi, na pili, kuwepo kwa fedha
kwenye bajeti ya Wizara au Idara husika kwa madhumuni hayo. Hivyo iweje
leo mtu apandishwe madaraja bila kulipwa mshahara stahiki? Hili
halieleweki na wala halikubaliki.
Ndugu Wananchi;
Niliagiza
viongozi wa Wizara zote na Halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi wote
wanapandishwa vyeo wakati wao ukiwadia na wanalipwa stahili zao kwa
wakati. Hali kadhalika, madeni ya malimbikizo ya mafunzo hayawezi kuwepo
kama utaratibu wa serikali wa mafunzo ungefuatwa. Chini ya utaratibu
huo mambo matatu hupaswa kuzingatiwa. Kwanza, mpango wa mafunzo wa
Wizara, Idara au Taasisi. Pili, watumishi wanaohitaji mafunzo kuingizwa
kwenye mpango wa mafunzo wa taasisi husika. Tatu, kutenga fedha za
kugharamia mafunzo hayo. Kama fedha haikutengwa, mtumishi hawezi kwenda
kusoma. Mtumishi anayejiendeleza nje ya mpango huo atafanya hivyo kwa
gharama zake mwenyewe.
Sasa
madeni hayo ya mafunzo yanatoka wapi? Kama wako watendaji wanaowaruhusu
watumishi walio chini yao kwenda kusoma bila kutengewa fedha kwenye
bajeti wawajibishwe ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya hotuba yangu ya Februari, 2009 na Serikali kulipa takriban shilingi
bilioni 64 kwa madai ya walimu mwaka huo, bado Serikali ililipa tena
shilingi bilioni 29.8 kati ya Julai 2010 na Oktoba 2011. Hivi sasa
nimeambiwa tena kuna madai mapya yaliyofikia shilingi bilioni 52.7. Sina
tatizo na madai yanayostahili kulipwa na najua kwamba shilingi bilioni
22.5 zimetolewa na kati ya hizo shilingi bilioni 19.2 zimekwishapelekwa
kwenye Halmashauri husika na shilingi bilioni 3.3 ni kwa ajili ya
waajiriwa wa Wizara. Zilizobakia zitalipwa kwenye mishahara yao.
Bado
ningependa kujua imekuwaje tena kuwe na malimbikizo makubwa kiasi hiki.
Mambo haya tulikwishaelewana kuhusu namna ya kuepuka malimbikizo.
Kulikoni? Je lini tabia hii ya kulimbikiza madeni itakoma? Nataka
majibu toka kwa wahusika.
Ndugu Wananchi;
Hivi
karibuni tumelijadili suala la ajira na huduma kwa walimu. Tumegundua
kuwa zipo mamlaka kadhaa zinazohusika na ajira na masuala ya walimu na
kwamba huenda inachangia kasoro hizi zinazojitokeza. Tumeelewana kuhusu
kulitafutia ufumbuzi wa kudum wa suala hilo mapema iwezekanavyo. Labda
itasaidia. Naamini baada ya muda si mrefu tutakuwa tumepata jawabu
litakaloturidhisha sote. Serikali na walimu ili tuondokane na misuguano
isiyokuwa ya lazima.
Mahusiano ya Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika
medani ya Kimataifa mwaka 2011, Serikali iliendelea kutetea na
kuendeleza maslahi ya Tanzania nje ya nchi. Mahusiano yetu na mataifa
na mashirika ya kikanda na kimataifa yamezidi kuimarika. Ahadi yetu
katika mwaka 2012 ni kuendeleza juhudi hizo maradufu kwani nchi yetu
inanufaika sana kwa ajili hiyo.
Washirika
wetu wa maendeleo wameendelea kutuunga mkono, kututia moyo na
kutusaidia katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Tunawashukuru
sana kwa ushirikiano mzuri na misaada yao na tunawaahidi kuitumia vizuri
misaada hiyo.
Sensa
Ndugu Wananchi;
Katika
kumalizia hotuba yangu nataka kuzungumzia mambo mawili. Jambo la
kwanza ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Jumapili ya tarehe 26
Agosti, 2012. Hapa nchini tumekuwa na utaratibu wa kufanya sensa kila
baada ya miaka 10, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2002.
Kufanya
Sensa ya Watu na Makazi ni jambo lenye umuhimu wa kipekee kwa taifa.
Takwimu na taarifa zitakazokusanywa husaidia taifa katika kupanga
mikakati na mipango yake ya maendeleo. Aidha, husaidia Serikali kupima
mafanikio ya programu zake mbalimbali za Maendeleo. Husaidia pia
kujipanga vizuri katika kufanya mambo yake.
Ndugu Wananchi;
Maandalizi
ya kufanyika kwa sensa hiyo yanaendelea vizuri. Maelekezo yanatolewa na
yataendelea kutolewa kuhusu namna itakavyofanyika na wajibu wa kila
mmoja wetu. Ninawaomba Watanzania wenzangu msikilize maelezo na
maelekezo hayo. Pia naomba nyote muhifadhi na kuikumbuka tarehe hiyo
ili siku hiyo mtu asikose kuhesabiwa. Mwisho, naomba kila mmoja wetu
awepo kuhesabiwa siku hiyo.
Vitambulisho vya UTaifa
Ndugu Wananchi,
Jambo
la pili ni vitambulisho vya uraia. Hatimaye azma ya tangu Uhuru ya
kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha uraia tumeweza kuanza kuitimiza.
Mwezi Desemba mwaka 2011, mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya uraia
umeanza. Mchakato huu ambao ni wa miaka mitatu umegawanyika katika
awamu nne kila moja ikihusisha makundi mbalimbali.
Awamu
ya kwanza imeanza na watumishi wa Dar-es-Salaam na Zanzibar na
vitambulisho vyao vitatolewa wakati wa sherehe za Muungano mwezi Aprili
2012. Baada ya hapo zitafuta awamu nyingine. Nawasihi wananchi
wenzangu mjiandae kwa kutayarisha nyaraka muhimu zitakazohitajika kwa
ajili ya kufanikisha zoezi hilo. Aidha, naomba kutoa tahadhari kwamba
watumishi watakaohusika na zoezi hili wawe waadilifu. Sitapenda kuona
au kusikia vitambulisho vinatolewa kwa watu ambao hawastahili kuvipata.
Ni wajibu wao kujiridhisha na nyaraka zinazowasilishwa na wananchi na
kama watakuwa na mashaka ni vyema kuwasiliana na taasisi husika kwa
uthibitisho zaidi.
Hitimisho
Ndugu Wananchi; Watanzania Wenzangu;
Wakati
tunapojiandaa kuanza mwaka mpya hapo kesho, napenda kuwahakikishia kuwa
mimi na wenzangu Serikalini tumedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa moyo
wetu wote na kwa nguvu zetu zote. Tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu
na vipaji alivyotujaalia Mwenyezi Mungu kushirikiana nanyi katika
kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazolikabili taifa letu na
watu wake. Naamini kwa pamoja na ushirikiano tutaweza, kila mtu atimize
wajibu wake.
Baada ya kusema hayo, nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya 2012. Sote tusherehekee kwa amani na utulivu.
Mungu Ibariki Afrika;
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Subscribe to:
Posts (Atom)