Marejeo: Tukumbuke hiki kisa alikuwa akisimulia yule binti niliyekutana naye akiwa kajiinamia kashika shavu, ….akiwa kasimuliwa na mama yake. Huyu binti kwa hali aliyokuwa nayo, alifikia hadi kukusudia hata kujiua.
Binti aliona kabisa , kuwa maisha kwake hayana thamani tena. Na binadamu anapofikia hapo, ujue kweli kuna jambo…nani asiyependa kuishi, hata yule anayekusudia kujiua, muda roho ikitaka kutoka, huwa anajitahidi kuiondoa ile kamba shingoni, lakini anakuwa keshachelewa, siku yake imeshafika, inabidi aonje umauti…na jamani kutoka kwa roho sio kitu cha mchezo.
Katika kisa hiki utagundua kuwa kuna mwanamama hapo ambaye ana jina hilo hilo, …jina ambalo nilisikia akiitwa huyu binti na mama yake mdogo, wakati namuulizia kuhusu maisha yake, kwanini imetokea hivyo, sasa tuendelee na kisa chetu, ………….
*********
‘Mimi sikujua kabisa huyo baba mlevi ninayeishi naye sio baba yangu wa kunizaa, kumbe alikuwa ni baba wa kufikia, hayo niliyajua baadaye, wakati najiandaa na safari ya kuja kuishi huku Dar, mji ambao kila mmoja kule kijijini alitamani kuja kuishi.
Mama yangu aliniambia huyo baba ndiye aliyekuja kumuokoa pale alipoachwa pale porini…..ili wenzake wafike huko wanapohitajika kwa wakati muafaka, na baadaye watarejea kumchukua, au kumtafutia sehemu ya kumuhifadhi.
Wakati kaachwa pale, akiwa kachoka, kwani mwili ulikuwa hauna nguvu, baada ya safari ndefu, baada ya mapigano, na yeye kujitolea kumsaidia huyo jamaa aaliyeficha sura yake kwa kofia ya ngozi ….na haat kujeruhiwa tena…akawa anatamani kulala tu.
‘Wewe pumzika hapa, na utakula nyama hii…mimi nahitaji huko kwetu haraka, leo najua inawezekana ikawa siku ya mwisho, nimeota kuwa nahitaji haraka sana….na kama ulivyoona, hawa watu walikuja kuniua, lakini tumeweza kuokoka…..ngoja nifike huko nyumbani haraka, halafu nitarudi kuhakikisha kuwa upo mikono salama….’akasema.
‘Sawa wewe nenda tu, na nakutakia mafanikio mema, mungu yupo pamoja na wewe, ila ninachokuomba ni kuhusu mtoto wangu…..naomba siku ukija, uje na mtoto wangu, usije bila ya kuwa na mtoto wangu….’akasema huyo mwanamama.
‘Naahidi nitafanya hivyo…na wewe hakikisha unakuwa salama, usiondoke, hapa, …hapa ni salama zaidi’akasema na akambusu kichwani na kuondoka. Huyu mwanamama alikaa pale kwa muda, halafu akaona akatafute maji ya kuoga, maji yaliyokuwepo pale yalikuwa ni machache, ….........
"Swahili NA Waswahili" Pamoja Saaaana.