Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 18 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 14...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu..
Mtakatifu,Mtakatifu,Mtakatifu Baba wa mbinguni..Mungu wetu na Muumba wetu,Mungu wa Abrahamu , Isaka na Yakobo, Baba yetu,Mlinzi wetu,Kimbilio letu,Yahweh..!Jehovah..!
Tunakushukuru na kukusifu,Asante kwa  ajili ya Ridhiki zako, Asante kwa kutuamsha tena siku hii na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..

Asante kwa wema na Fadhili zako,Asante kwa Baraka zako..
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kukuabudu..

Tunaomba ukatubariki Tuingiapo/tutokapo,vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri,Tuembeapo Baba hatua zetu ziwe nawe...
Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase na Damu ya mwanao Mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti.
Ukatutakase Miili yetu na Akili zetu,Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda, tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa mbinguni tunakuja mbele zako na kuomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..Kwakuwaza,kwakunena/kutenda,kujua/kutojua..

Nasi ukatupe Neema ya kuweza kuwasaheme waliotukosea..
Sarafu iliyopotea
8“Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. 9Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ 10Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”[Luka 15;8-10]

Baba wambingu tunaomba ukawaguse na kuwaponya wote wanaopitia magumu/majaribu,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,waliomagerezani pasipo na hatia Baba haki ikatendeke,waliofungwa na mwovu Baba ukawaponye pia na kuwaweka huru kimwili na kiroho..Waliokataliwa,waliokata tamaa Baba wakapate tumaini la kweli..wenye shida na Tabu..Baba ukaonekane katika shida zao..
Asante kwa ajili ya yote tunayaweka haya mikononi mwako,Tukishukuru na kukusifu,Tukiamini wewe ni Mungu wetu na hakuna kama wewe..
Leo kesho na hata milele..
Amina..!

Taa iliyofunikwa kwa debe
(Marko 4:21-25)
16“Watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga.
17“Chochote kilichofichwa kitafichuliwa, na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani.
18“Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho, kitachukuliwa.”[Luka8;16-18]

Mungu aendelee kuwabariki wote mliopita hapa..
Nawapenda..
 

Waisraeli wanavuka bahari ya Shamu

1Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli warudi nyuma, wapige kambi mbele ya Pi-hahirothi, kati ya mji wa Migdoli na bahari ya Shamu, mbele ya Baal-sefoni. Mtapiga kambi mbele yake karibu na bahari. 3Maana, Farao atafikiri, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga, nalo jangwa limewazuia wasiweze kutoka.’ 4Hapo mimi nitamfanya Farao kuwa mkaidi, naye atawafuatia. Nami nitajipatia utukufu kwa kumwangamiza yeye na jeshi lake. Hapo Wamisri watatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo.
5Farao, mfalme wa Misri, aliposikia kwamba Waisraeli wamekimbia, yeye na maofisa wake walibadili fikira zao, wakasema, “Tumefanya nini kuwaachia Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?” 6Basi, Farao akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake. 7Alichukua magari yake bora ya vita 600 na magari yote mengine ya kivita ya Misri yakiongozwa na maofisa wa kijeshi. 8Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao, mfalme wa Misri, kuwa mkaidi naye akawafuatia Waisraeli ambao walikuwa wameondoka Misri kwa ushupavu.14:8 kwa ushupavu: Au chini ya ulinzi wa Mwenyezi-Mungu. 9Wamisri pamoja na farasi wao wote, magari ya farasi ya vita na wapandafarasi wake waliwafuata Waisraeli, wakawakuta wamepiga kambi kando ya bahari, karibu na Pi-hahirothi, mbele ya Baal-sefoni.
10Waisraeli walipotazama na kumwona Farao akija na jeshi lake dhidi yao, walishikwa na hofu kubwa, wakamlilia Mwenyezi-Mungu. 11Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri? 12Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.”
13Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena. 14Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.”
15Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. 16Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu. 17Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake. 18Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
19Basi, malaika wa Mungu aliyekuwa mbele ya kundi la Waisraeli aliondoka akakaa nyuma yao. Na ule mnara wa wingu pia uliondoka mbele ukasimama nyuma yao, 20ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana14:20 lile wingu … hayakukaribiana: Makala ya Kiebrania si dhahiri na baadhi ya tafsiri ni tofauti. usiku kucha.
21Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu. 22Taz 1Kor 10:1-2 Ebr 11:29 Waisraeli wakapita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa upande wao wa kulia na wa kushoto. 23Wamisri wakawafuata kwa kupitia nchi kavu iliyokuwa katikati ya bahari pamoja na farasi wao, magari yao ya vita na wapandafarasi wao wote. 24Karibu na mapambazuko, Mwenyezi-Mungu aliliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ule mnara wa moto na ule mnara wa wingu, akalitia hofu kubwa. 25Aliyakwamisha magurudumu ya magari yao, yakawa yakienda kwa shida sana. Hapo Wamisri wakasema, “Tuwakimbie Waisraeli; Mwenyezi-Mungu anawapigania Waisraeli dhidi yetu.”
26Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi na kuwafunika Wamisri pamoja na magari yao na wapandafarasi wao.” 27Basi, Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka bahari ikarudia hali yake ilivyokuwa. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji lakini Mwenyezi-Mungu akawasukumizia baharini. 28Maji yakayafunika magari pamoja na wapandafarasi; jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuatia Waisraeli likafa baharini. Hakunusurika Mmisri hata mmoja. 29Lakini Waisraeli walipita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa zimesimama upande wao wa kulia na wa kushoto.
30Siku hiyo Mwenyezi-Mungu aliwaokoa Waisraeli mikononi mwa Wamisri; nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni wamekufa. 31Waisraeli walipoona tendo hilo la ajabu alilofanya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Wamisri, wakamcha, wakawa na imani na Mwenyezi-Mungu na Mose mtumishi wake.

Kutoka14;1-31


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 17 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 13...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu ni mwaminifu sana Tumshukuru katika yote..
Yeye aliyetupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..si kwa Uwezo wetu wala nguvu zetu ni kwa Neema/Rehema zake Mungu..
Tuzidi kumsifu na kuamini,Tumaini la kweli,Faraja ipo kwake,Furaha ina yeye,Mwenye mapenzi ya kweli,Asiyeshindwa na Jambo,Mlinzi mkuu,Muumba wetu,Muumba mbingu na Nchi,Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..Yahweh..!!Jehovah..!!Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega...Hakuna linaloshindikana kwakwe ukiomba na kuamini na kufuata nja zake..
Asante Baba wa Mbinguni kwa  siku hii na kutuamsha salama,Tazama Jana imepita Yahweh..Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine...
Tunakuja mbele zako na tunajinyenyekeza Mfalme wa Amani..Tunaomba ukatubariki na kutulinda,Ukatamalaki na kutuatamia..
Ukabariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..Ukabariki kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka pale msalabani ili sisi tupate kupona..Jehovah..! Ukatakase Akili zetu na Miili yetu tupate kutambua/kujitambua..
Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda na tuwe na kiasi..
Tunakwenda kinyume na Mwovu na kazi zake zote..
Tunajiachilia mikononi mwako Baba..Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe,kwakuwaza/kutenda,kwakujua/kutojua..
Ukatufanye chombo kipya na tukakutumikie sawasawa na mapenzi yako..

Lawi anaitwa kuwa mwanafunzi
(Mat 9:9-13; Marko 2:13-17)

27Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28Naye akaacha yote akamfuata. 29Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. 30Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” 31Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. 32Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.[Luka5:27-32]

Baba tunaomba ukawaponye na kuwaokoa wenye Shida/Tabu,Wagonjwa,Wafiwa ukawe mfariji wao..Tamazama waliovifungoni Baba tunaomba ukawafungue na kuwaponya kimwili na kiroho ..
Tunashukuru na kukusifu Daima,Tunayaweka haya yote mikononi mwako na kuamini wewe ni Mungu wetu Leo kesho na hata milele.
Amina..!
4Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! 5Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. 6Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. 7Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.[wafilipi4;4-7]






Kuwaweka wakfu wazaliwa wa kwanza

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Niwekee wakfu wazaliwa wote wa kwanza wa kiume, maana wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa Waisraeli na kila wazaliwa wa kwanza wa wanyama ni wangu.”
Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu
3Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii mliyotoka nchini Misri ambako mlikuwa watumwa. Hii ndiyo siku Mwenyezi-Mungu alipowatoa humo kwa mkono wake wenye nguvu. Katika siku hii, kamwe msile mkate uliotiwa chachu. 4Siku hii, mwezi wa kwanza wa Abibu, mtaondoka nchini Misri. 5Na wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi ambayo aliwaapia babu zenu kwamba atawapa nyinyi, nchi inayotiririka maziwa na asali, ni lazima muiadhimishe sikukuu hii kila mwaka katika mwezi huu wa kwanza. 6Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, na mnamo siku ya saba mtafanya sikukuu kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. 7Kwa muda huo wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Kusiwepo na mikate iliyotiwa chachu, wala chachu yoyote miongoni mwenu na katika nchi yenu yote. 8Siku hiyo mtawaambia watoto wenu kwamba mnafanya hivyo kwa sababu ya jambo alilowafanyia Mwenyezi-Mungu mlipoondoka nchini Misri. 9Adhimisho hilo litakuwa ukumbusho, kama alama katika mikono yenu au katika paji la nyuso zenu; ili iwakumbushe daima sheria ya Mwenyezi-Mungu. Maana, Mwenyezi-Mungu amewatoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu. 10Kwa hiyo, mtaadhimisha sikukuu hii kwa wakati uliopangwa, kila mwaka.”

Maelezo kuhusu wazaliwa wa kwanza

11Mose akaendelea kuwaambia watu, “Hali kadhalika, wakati Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha katika nchi ya Wakanaani na kuwapeni iwe mali yenu kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu, 12Taz Kut 34:19-20; Luka 2:23 lazima kumwekea Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yenu atakuwa wa Mwenyezi-Mungu. 13Lakini mzaliwa wa kwanza wa kiume wa punda utamkomboa kwa kulipa mwanakondoo, la sivyo, utamuua kwa kumvunja shingo. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa binadamu utamkomboa. 14Kama hapo baadaye mwanao akiuliza maana ya jambo hili, utamwambia, ‘Kwa nguvu ya mkono wake, Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri ambako tulikuwa watumwa. 15Farao kwa ukaidi alikataa kutuachia tuondoke; kwa hiyo Mwenyezi-Mungu alimuua kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri, mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa mnyama. Basi, mimi ninamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yangu, lakini kila mzaliwa wa kwanza wa wanangu namkomboa.’ 16Jambo hili litakuwa kama alama mkononi mwako au utepe katika paji la uso wako, kwamba Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu.”
Mnara wa wingu na wa moto

17Wakati Farao alipowaachia Waisraeli waende zao, Mungu hakuwapitisha katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa ya karibu. Mungu alisema, “Sipendi watu hawa wabadilishe nia na kurudi Misri wakijua itawabidi kupigana vita.” 18Badala yake, Mungu aliwapitisha Waisraeli katika njia ya mzunguko kupitia jangwani, kuelekea bahari ya Shamu.13:18 bahari ya Shamu: Kiebrania neno kwa neno ni “bahari ya mafunjo”. Waisraeli waliondoka nchini Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.
19 Taz Mwa 50:25; Yos 24:32 Mose aliichukua mifupa ya Yosefu kama Yosefu alivyoagiza kabla ya kufa kwake. Alikuwa amewaapisha rasmi Waisraeli akisema, “Mungu atakapowajia kuwatoa nchini humu, ni lazima mwichukue mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.”
20Basi, Waisraeli waliondoka Sukothi, wakapiga kambi huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa. 21Mchana Mwenyezi-Mungu aliwatangulia katika mnara wa wingu kuwaonesha njia, na usiku aliwatangulia katika mnara wa moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana na usiku. 22Taz Hek 10:17-18; 18:3 Mnara wa wingu wakati wa mchana, na mnara wa moto wakati wa usiku, kamwe haikukosekana kuwatangulia Waisraeli.

Kutoka13;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday, 14 April 2017

Nawatakia Ijumaa Kuu Njema na Maandalizi mema ya Pasaka;Burudani-Kwaya Ya Vijana KKKT Mabibo Mateso Ya Bwana Yesu,Azania Front - Kweli ni Huzuni..


Wapendwa/Waungwana nawatakia maandalizi mema ya Pasaka...
Ikawe yenye kheri na Amani,Furaha na Upendo.


         Mpendwa nini umepanga Pasaka hii? Kula na wapendwa Ndugu,Jamaa,Marafiki,Wazee,Wasiojiweza? au Utakuwa wapi?





Mimi baada ya Ibada nitakuwa Kazini ikimpendeza Mungu..!!
Muwe na wakati mwema..
Nawapenda.

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 12...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu na kumsifu Daima..

Mshangilieni Mwenyezi-Mungu, enyi nchi zote! Mwabuduni Mwenyezi-Mungu kwa furaha, nendeni kwake mkiimba kwa shangwe! Jueni kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu. Yeye ndiye aliyetuumba, nasi ni mali yake; sisi ni watu wake, ni kondoo wa malisho yake. Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake. Mwenyezi-Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele, na uaminifu wake katika vizazi vyote.

Tunakushuru eeh Mungu wetu,Baba yetu,Mwamba wetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi..Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Asante kwa yote uliyotutendea/unayoendelea kututendea,Imani na Tumaini tunaweka kwako..

Asante kwa kutuchagua tena kuendelea  na kutupa kibali cha kuiona siku hii Baba wa Mbingu..Neema/Rehema zako zatutosha Mwenyezi-Mungu,Faraja yako inatutosha Baba,Upendo wako wadumu milele,Hakuna wa kufanana nawe Jehovah..!! Hakuna na hatokuwepo Yahweh..!!
Mungu usiye sinzia wala kulala..Mungu unayejibu na kutenda,Mungu unayebariki,Mungu uponyae..wewe watosha Baba wa Mbinguni...wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho Yahweh..!!
Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..Baba ukatubariki tuingiapo/tutokapo,vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..!
Mfalme wa Amani ukabariki Kazi zetu,Bishara zetu,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo..

Baba ukatutakase Miili yetu na Akili zetu..Ukatuokoe na yule Mwovu na kazi zake zote..Ukatufunike na Damu ya mwanao Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..Yeye aliteseka pale msalabani ili sisi tupate kupona..
Yahweh..!! Tazama wenye Shida/Tabu, wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokuwa vifungoni,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao..
Baba tunaomba kwa mkono wako ukawaguse na kuwaponya..wapate kupona kimwili na kiroho,,Baba ukaonekane kwenye  shida zao..
Baba tunakuja mbele zako kwa kujinyenyekeza na tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Jehovah..! kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutokujua..
Baba tunaomba nasi utupe Neema yakuweza kuwasamehe wale waliotukosea..

Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako!

Asante Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako,Tunakusifu na kukushukuru katika yote..Tukiamini ya kwamba wewe ni Mungu wetu na Mwokozi wetu..
Amina..!!

Muwe na wakati mwema  wote 

mliopita hapa na Mungu aendelee kuonekana Maishani mwenu.





Pasaka
(Kumb 16:1-8)

1 Taz Lawi 23:5; Hes 9:1-5; Kumb 16:1-2 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri, 2“Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka. 3Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja. 4Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula. 5Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi. 6Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni. 7Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao. 8Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani. 9Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani. 10Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni. 11Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: Mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.
12“Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. 13Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri. 14Taz Kut 23:15; 34:18; Lawi 23:6-8; Hos 28:17-25; Kumb 16:3-8 Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.”

Sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu

15Mwenyezi-Mungu akasema, “Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtaondoa chachu katika nyumba zenu. Mtu yeyote akila kitu kilichotiwa chachu katika muda huo wa siku saba, ni lazima aondolewe miongoni mwa Waisraeli. 16Siku ya kwanza na siku ya saba mtakuwa na mkutano mtakatifu. Katika siku hizo mbili hamtaruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya lazima ya kutayarisha chakula. 17Mtaadhimisha sikukuu hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ukumbusho wa siku nilipowatoa nyinyi, vikundi vya Israeli, kutoka Misri. Sikukuu hiyo itaadhimishwa na vizazi vyenu vyote vijavyo, kama agizo la milele. 18Basi, mtakula mikate isiyotiwa chachu kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huohuo wa kwanza. 19Katika siku hizo saba, msiwe na chachu yoyote katika nyumba zenu. Mtu yeyote, awe mgeni au mwenyeji, akila kitu kilichotiwa chachu, ataondolewa miongoni mwa jumuiya ya Waisraeli. 20Popote pale mnapoishi, ni mwiko kabisa kula chochote kilichotiwa chachu. Mnapaswa kula mikate isiyotiwa chachu.”

Pasaka ya kwanza

21Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka. 22Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika12:22 na kuyachovya … birika: Au na kuyaweka juu ya kizingiti. na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi. 23Taz Ebr 11:28 Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi12:23 Mwangamizi: Au Malaika wa kifo. kuingia katika nyumba zenu na kuwaua. 24Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele. 25Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza. 26Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’ 27Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
28Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.

Pigo la kumi: Kuuawa kwa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri

29 Taz Kut 4:22-32 Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi-Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri. Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa gerezani. Hata wazaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa. 30Basi Farao, watumishi wake na wakazi wote wa Misri wakaamka usiku. Kukawa na kilio kikubwa nchini kote Misri kwa maana hapakuwa hata nyumba moja ambamo hakufa mtu. 31Hapo Farao akawaita Mose na Aroni, usiku huohuo, akamwambia, “Amkeni! Ondokeni miongoni mwa watu wangu. Nendeni, nyinyi pamoja na hao Waisraeli, mkamtumikie Mwenyezi-Mungu kama mlivyosema. 32Chukueni makundi yenu ya kondoo na ng'ombe, mwondoke; niombeeni na mimi baraka.”
33Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke haraka, wakisema, “Hakika tutakufa sote!” 34Basi, Waisraeli wakauchukua unga wao uliokandwa kabla haujatiwa chachu, na mabakuli yao ya kukandia wakiwa wamezifunga kwa nguo na kubeba mabegani. 35Taz Kut 3:21-22 Waisraeli walikuwa wamekwisha fanya kama Mose alivyowaagiza hapo awali: Waliwaomba Wamisri wawapatie vito vya fedha, dhahabu na mavazi. 36Naye Mwenyezi-Mungu alikwisha wafanya Waisraeli wapendwe na Wamisri, nao Wamisri wakawapa kila kitu walichoomba. Ndivyo Waisraeli walivyowapokonya Wamisri mali yao.

Waisraeli wanaondoka Misri

37Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi, wakasafiri kwa miguu kuelekea Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao 600,000, licha ya wanawake na watoto. 38Kulikuwa pia na kundi la watu wengine walioandamana nao pamoja na mifugo mingi, kondoo na ng'ombe. 39Kwa kuwa walikuwa wameondoka Misri kwa haraka, hawakuweza kutayarisha chakula cha safarini, ila tu ule unga uliokandwa bila kutiwa chachu. Basi, wakaoka mikate isiyotiwa chachu.
40 Taz Mwa 15:13; Gal 3:17 Waisraeli walikuwa wameishi nchini Misri kwa muda wa miaka 430. 41Katika siku ya mwisho ya mwaka wa 430, siku hiyohiyo maalumu ndipo makabila yote ya Mwenyezi-Mungu yaliondoka nchini Misri. 42Usiku huo ambao Mwenyezi-Mungu alikesha ili kuwatoa Waisraeli nchini Misri, unapaswa kuadhimishwa na Waisraeli wote na vizazi vyao vyote, kama usiku wa kukesha kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.

Taratibu za Pasaka

43Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Yafuatayo ni maagizo juu ya adhimisho la Pasaka. Mgeni yeyote hatashiriki chakula cha Pasaka. 44Lakini mtumwa yeyote aliyenunuliwa kwa fedha, baada ya kumtahiri, ataruhusiwa kushiriki. 45Msafiri yeyote, wala kibarua yeyote, hatashiriki chakula hicho. 46Taz Hos 9:12; Yoh 19:36 Mwanakondoo wa Pasaka ataliwa katika nyumba moja. Hamtatoa nyama yoyote nje ya nyumba alimochinjiwa, wala hamtavunja hata mfupa mmoja wa mnyama wa Pasaka. 47Jumuiya yote ya watu wa Israeli itaadhimisha sikukuu hiyo. 48Mgeni yeyote anayeishi miongoni mwenu akipenda kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, ni lazima kwanza wanaume wote wa nyumba yake watahiriwe; hapo atahesabiwa kuwa kama mwenyeji na kuruhusiwa kushiriki. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa asishiriki kamwe. 49Sheria zilezile zitamhusu mzalendo Mwisraeli na wageni watakaoishi miongoni mwenu”. 50Waisraeli wote walitii sheria hiyo na kufanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Mose na Aroni. 51Siku hiyohiyo Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri kwa makundi.

Kutoka12;1-51

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 13 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 11...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Matendo yake makuu kwetu..
Yeye anatujua kuliko tunavyojijua,Yeye ni Mungu wetu na Kimbilio letu,Yeye aliyetupa Kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..Yeye ni Muumba wetu na Muumba wa Mbingu na Nchi..Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Yeye ni Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo, Yeye ni Alfa na Omega..Yeye ni Mlinzi mkuu na Mtawala,Amani,Furaha,Upendo na Fadhili zipo kwake..Yeye akisema ndiyo hakuna wakusema siyo..Yeye atosha Maishani kwetu.ukimuita aitika,ukimuomba anakupa,ukifuata njia zake na kumuabudu yeye hutojuta..



Mungu si mtu, aseme uongo, wala si binadamu, abadili nia yake! Je, ataahidi kitu na asikifanye, au kusema kitu asikitimize?[Hesabu 23:19]
Asante Baba wa mbinguni kwa Neema/Rehema yako uliyotupa..Tazama Jana imepita Baba Leo ni Siku mpya na Kesho ni siku nyingine..
Jehovah..!! tunaomba uibariki siku hii ikawe njema , yenye Amani na kukupendeza wewe..Ukabariki kuingia kwetu na kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Baba..
Tunaomba ukabariki Vilaji/Vinywaji, Kazi zetu,Biashara,Masomo na Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia ukavitakasase kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Baba tunakwenda kinyume na adui mwovu na kazi zake zote..Tunaomba ukatuokoe,kutulinda na kutufunika na Damu ya Mwokozi wetu Bwana Yesu Kristo..
Baba tukuja mbele zako na kujinyeyekeza tunaomba utusamehe pale tulikwenda kinyume nawe..kwakuwaza,kwakunena,kwakujua/kutojua..Mfalme wa Amani tunaomba utupe nasi Neema ya kuweza kuwasamehe wote waliotukosea..
Roho mtakatifu akatuongoze vyema katika yote..
Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Jehovaha..!!!Ukawaguse na kuwaokoa wote wanaopitia magumu/mapito,shida/tabu,Wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,waliokata tamaa,waliokataliwa na wakapate tumaini lako..
ukawaponye kimwili na kiroho pia..

Tunayaweka haya mikononi mwako Yahweh..Sifa na Utukufu ni wako Daima.
Tunashukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu leo na hata milele.


11Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.[Waroma10;11]
Amina..!!
Muwe na wakati mwema..nawapenda.


Tangazo la kuuawa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Bado kuna pigo moja nitakalomletea Farao na nchi ya Misri. Baadaye atawaacheni mwondoke hapa. Tena atakapowaacheni mwondoke, yeye mwenyewe atawafukuza mwondoke kabisa. 2Waambie Waisraeli sasa wasikie vizuri kwamba kila mmoja wao, mwanamume kwa mwanamke, ni lazima amwombe jirani yake vito vya fedha na dhahabu.” 3Mwenyezi-Mungu akawafanya Waisraeli wapendeke mbele ya Wamisri. Tena, Mose mwenyewe akawa mtu mashuhuri sana nchini Misri, na mbele ya maofisa wa Farao na watu wote.
4Mose akamwambia Farao, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Panapo usiku wa manane leo, nitapitia katikati ya nchi ya Misri. 5Nitakapopita, kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri atakufa: Kuanzia mzaliwa wa kwanza wako wewe Farao ambaye ni mrithi wako, hadi mzaliwa wa kwanza wa mjakazi anayesaga nafaka kwa jiwe. Hata wazaliwa wa kwanza wa mifugo nao wote watakufa. 6Kutakuwa na kilio kikubwa kote nchini Misri, kilio ambacho hakijapata kutokea, wala hakitatokea tena. 7Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna mtu, mnyama au mbwa wao atakayepatwa na madhara yoyote, ili upate kutambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu hutofautisha kati ya Waisraeli na Wamisri.’” 8Mose akamalizia kwa kumwambia Farao, “Watumishi wako hawa watanijia na kuinama mbele yangu kwa heshima, wakinisihi niondoke nchini Misri, mimi pamoja na watu wote wanaonifuata. Baada ya hayo, nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa ameghadhabika, akaondoka kwa Farao.
9Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Farao hatakusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka nchini Misri.” 10Basi, Mose na Aroni walifanya maajabu hayo yote mbele ya Farao. Lakini Mwenyezi-Mungu alimfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaruhusu Waisraeli waondoke nchini mwake.

Kutoka11;1-10

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday, 12 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 10...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu yu mwema sana...

Asante Baba wa Mbinguni kwa Neema/Rehema hii uliyotupa Umetupa Kibali cha kuendelea kuiona siku hii Baba...
Sifa na Utukufu ni kwako daima..
Tunajiachilia mikononi mwako na kujinyeyekeza mbele zako Yahweh..!!
Tunaomba Utubariki katika maisha yetu na ukatuongoze katika yote..
Jehovah..!!Ukatuokoe na Mwovu pamoja na kazi zake zikashindwe katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Tukawe barua njema na tukasomeke vyema..

Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine? Nyinyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma. Ni dhahiri kwamba nyinyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu. Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu: Maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uhai.

Ukabariki familia zetu Jehovah..!!!Amani ikawe nasi daima..
Mfalme wa Amani ukatawale, Ukatamalaki na kutuatamia.Ukawe mlinzi mkuu na ukawaguse na kuwaponya wote waliofungwa kimwili na kiroho,Wagonjwa,wenye shida/tabu,wafiwa ukawe mfariji wao..
Mungu wetu, Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa vyote na vyote ni mali yako Baba..
Tunaomba ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo..


Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Yahwehh..kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua...
Nasi ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika safari yetu ya maisha..

6Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana,
mwombeni msaada wakati yupo bado karibu.[Isaya55:6]

Tunayaweka haya mikononi mwako,Tukishukuru na kuamini wewe ndiye Mungu wetu na Muumba wetu..Hakuna linaloshindikana kwako Baba..

Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.[waroma16:20]


Amina..!!!


Pigo la nane: Nzige

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao. Mimi nimemfanya kuwa mkaidi na maofisa wake ili nipate kutenda ishara hizi miongoni mwao, 2ili nyinyi mpate kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu, jinsi nilivyowadhihaki Wamisri kwa kuzifanya ishara hizo miongoni mwao. Hivyo mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
3Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, anasema hivi, ‘Mpaka lini utakataa kujinyenyekesha mbele yangu? Waache watu wangu waondoke ili wapate kunitumikia. 4Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako. 5Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani. 6Nzige hao watajaa katika nyumba zako, nyumba za maofisa wako na za Wamisri wote; watakuwa wengi kiasi ambacho hata wazee wenu hawajapata kuona tangu walipozaliwa, hadi leo.’” Basi, Mose akatoka kwa Farao.
7Viongozi wa Farao wakamwuliza, “Je, mtu huyu atatusumbua mpaka lini? Waache watu hawa waende zao wakamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Je, hujali kwamba nchi ya Misri inaangamia?”
8Hapo, Mose na Aroni wakaitwa warudi kwa Farao, naye akawaambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini, nauliza: Ni kina nani watakaokwenda pamoja nanyi?” 9Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.”
10Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu. 11La hasha! Ni wanaume tu watakaokwenda kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana hilo ndilo mnalotaka.” Hapo Mose na Aroni wakafukuzwa mbele ya Farao.
12Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige watokee ili waingie na kula mimea yote nchini na vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.” 13Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige. 14Taz Ufu 9:2-3 Hao nzige wakaenea kila mahali nchini Misri, wakatua juu ya ardhi yote. Nzige hao walikuwa kundi kubwa kupindukia, kiasi ambacho hakijapata kutokea wala hakitatokea tena. 15Waliifunika nchi yote ya Misri, hata ardhi ikaonekana kuwa giza. Walikula mimea yote na matunda yote yaliyosalia wakati wa ile mvua ya mawe. Hakuna hata jani moja lililosalia nchini. Hakuna jani lolote lililosalia juu ya miti wala mimea popote katika nchi yote ya Misri.
16Hapo Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka, akawaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu. 17Kwa hiyo sasa ninawasihi mnisamehe dhambi yangu, mara hii moja tu, mkaniombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki.”
18Basi, Mose akaondoka kwa Farao, akaenda kumwomba Mwenyezi-Mungu. 19Naye Mwenyezi-Mungu akaleta upepo mkali toka magharibi, ukawainua wale nzige na kuwasukumia kwenye bahari ya Shamu. Hakuna hata nzige mmoja aliyebaki katika nchi nzima ya Misri. 20Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachia Waisraeli waondoke.

Pigo la tisa: Giza

21 Taz Hek 17:1-21 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni ili giza nene litokee nchini Misri, giza nene ambalo mtu ataweza kulipapasa.” 22Taz Zab 105:28; Ufu 16:10 Basi, Mose akanyosha mkono wake juu mbinguni, kukawa na giza nene kote nchini Misri kwa muda wa siku tatu. 23Watu hawakuweza kuonana wala kuondoka mahali walipokuwa kwa muda huo wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga huko Gosheni walimokuwa wanakaa.
24Kisha, Farao akamwita Mose, akamwambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu. Watoto wenu pia wanaweza kwenda pamoja nanyi. Lakini kondoo na mbuzi, na ng'ombe wenu wabaki.” 25Lakini Mose akamwambia, “Ni lazima uturuhusu kuchukua wanyama wa tambiko na sadaka za kuteketezwa ili tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. 26Ngombe wetu ni lazima pia tuwachukue wala hakuna hata ukwato mmoja utakaobaki nyuma, kwa sababu kutoka katika mifugo yetu wenyewe, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala sisi hatujui ni mnyama yupi tutakayemtolea Mwenyezi-Mungu tambiko mpaka tutakapofika huko.”
27Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaachia Waisraeli waondoke. 28Farao akamwambia Mose, “Toka mbele yangu. Jihadhari sana. Usije kuniona tena, maana siku utakapokuja tena mbele yangu, utakufa!” 29Mose naye akamwambia, “Sawa! Kama ulivyosema sitakuja kukuona tena.”

Kutoka10;1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 11 April 2017

Jikoni Leo;MKATE WA AJEMI/BWANA - KISWAHILI,Mpishi da'Fathiya..




Mahitaji:
Mahitaji
Unga wa ngano vicombe 4 - 520 gms
Hamira kijiko 1 kikubwa - 17 gms
Baking soda kijiko cha chai 1 & 1/2 - 10.5 gms
Chumvi kijiko cha chai 1 & 1/2 - 9 gms 
Maziwa ya mtindi kikombe 1 
Maji nusu kikombe ( kwa kuzimua mtindi)
Mafuta vijiko 2 vikubwa 
Yai 1

Shukrani;Aroma of Zanzibar

"Swahili na Waswahili"Pamoja Daima.