Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluya Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu Muumba wetu
Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote vilivyomo
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye huruma
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo
Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Uzima
Mwenyezi-Mungu wetu Mungu wa walio hai
Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega..!!
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Baba wa Mbinguni...!!
1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salamu!
Imani na hekima
2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. 4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. 5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. 7,8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
Yakobo 1:1-8
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Jehovah utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote
Mungu wetu ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa
Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake. Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda. Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya
Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahweh tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio
ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah ukatupe neema ya kiufuata njia zako
Mungu wetu tunakasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Mungu wetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu
nasi tukatunmike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....
Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.
Yahweh tunawaweka mikononi mwako wote wenye shida/tabu,
wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitajio yake
Baba wa Mbinguni wewe unajua haja zao na mahitaji yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
nazo zikawaweke huru
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Ukawape macho ya rohoni Mungu wetu na masikio ya kusikia sauti yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina.....!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba ukae nanyi
daima....
Nawapenda.
|