Friday, 25 October 2019
Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 41....
Mungu anaahidi kuisaidia Israeli
1Mungu asema hivi:
“Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize!
Enyi mataifa jipeni nguvu;
jitokezeni mkatoe hoja zenu,
na tuje pamoja kwa hukumu.
2“Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki,
mtu ambaye hupata ushindi popote aendako?
Mimi huyatia mataifa makuchani mwake,
naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake!
Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi,
kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi.
3Yeye huwafuatia na kupita salama;
huenda kasi kana kwamba hagusi chini.
4Nani aliyefanya yote haya yatendeke?
Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio?
Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo,
mimi nitakuwapo hata milele.
5“Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa;
dunia yote inatetemeka kwa hofu.
Watu wote wamekusanyika, wakaja.
6Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema,
‘Haya! Jipe moyo!’
7Fundi anamhimiza mfua dhahabu,
naye alainishaye sanamu kwa nyundo,
anamhimiza anayeiunga kwa misumari.
Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’
Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike.
8Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu,
wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua,
wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu;
9wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia,
wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu;
mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’
10Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe.
Usifadhaike, mimi ni Mungu wako.
Nitakuimarisha na kukusaidia;
nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
11“Naam! Wote waliokuwakia hasira,
wataaibishwa na kupata fedheha.
Wote wanaopingana nawe,
watakuwa si kitu na kuangamia.
12Utawatafuta hao wanaopingana nawe,
lakini watakuwa wameangamia.
13Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
ndimi ninayetegemeza mkono wako.
Mimi ndimi ninayekuambia:
‘Usiogope, nitakusaidia.’”
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu,
enyi Waisraeli, msiogope!
Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia.
Mimi ni Mkombozi wenu,
Mtakatifu wa Israeli.
15Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria,
chenye meno mapya na makali.
Mtaipura milima na kuipondaponda;
vilima mtavisagasaga kama makapi.
16Mtaipepeta milima hiyo,
nao upepo utaipeperushia mbali,
naam, dhoruba itaitawanya huko na huko.
Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu;
mtaona fahari kwa sababu yangu
Mungu Mtakatifu wa Israeli.
17“Maskini na fukara wakitafuta maji wasipate,
wakiwa wamekauka koo kwa kiu,
mimi Mwenyezi-Mungu nitawajibu;
mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha.
18Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu,
na chemchemi katika mabonde.
Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji,
na nchi kame kuwa chemchemi za maji.
19Nitapanda miti huko nyikani:
Mierezi, mikakaya, mijohoro, na mizeituni;
nitaweka huko jangwani:
Miberoshi, mivinje na misonobari.
20Watu wataona jambo hilo,
nao watatambua na kuelewa kwamba
mimi Mwenyezi-Mungu nimetenda hayo,
mimi Mtakatifu wa Israeli nimefanya jambo hilo.”
Mwenyezi-Mungu aipuuza miungu ya uongo
21Mwenyezi-Mungu, Mfalme wa Yakobo, asema:
“Enyi miungu ya mataifa,
njoni mtoe hoja zenu!
22Leteni hoja zenu, mtuambie yatakayotukia.
Tuambieni matukio ya kwanza yalikuwa yapi
nasi tutayatafakari moyoni.
Au tutangazieni yajayo,
tujue yatakayokuja.
23Tuambieni yatakayotokea baadaye,
nasi tujue basi kama nyinyi ni miungu.
Fanyeni kitu chochote, chema au kibaya,
ili tutishike na kuogopa.
24Hakika, nyinyi si kitu kabisa.
hamwezi kufanya chochote kile.
Anayechagua kuwaabudu nyinyi ni chukizo.
25“Nimechochea mtu toka kaskazini,
naye amekuja;
naam, nimemchagua mtu toka mashariki,
naye atalitamka jina langu.
Yeye atawakanyaga wafalme kama tope,
kama vile mfinyanzi apondavyo udongo wake.
26Nani aliyebashiri haya tangu mwanzo,
hata sisi tupate kuyatambua?
Nani aliyetangulia kuyatangaza,
ili sasa tuseme, alisema ukweli?
Hakuna hata mmoja wenu aliyeyataja,
wala hakuna aliyesikia maneno yenu.
27Mimi ni yule wa kwanza, niliyetangaza kwa Siyoni,
nikapeleka Yerusalemu mjumbe wa habari njema.
28Nimeangalia kwa makini sana,
lakini simwoni yeyote yule;
hamna yeyote kati ya hao miungu awezaye kushauri;
nikiuliza hakuna awezaye kunijibu.
29La! Miungu hiyo yote ni udanganyifu,
haiwezi kufanya chochote;
sanamu zao za kusubu ni upuuzi.
Isaya41;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Thursday, 24 October 2019
Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 40....
Tumaini la kuponywa katika Yerusalemu
1Mungu wenu asema:
“Wafarijini watu wangu,
nendeni mkawafariji.
2Semeni na wenyeji wa Yerusalemu kwa upole,
waambieni kwamba utumwa wao umekwisha,
wamesamehewa uovu wao.
Mwenyezi-Mungu amewaadhibu maradufu
kwa sababu ya dhambi zao zote.”
3Sauti ya mtu anaita jangwani:
“Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia,
nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu.
4Kila bonde litasawazishwa,
kila mlima na kilima vitashushwa;
ardhi isiyo sawa itafanywa sawa,
mahali pa kuparuza patalainishwa.
5Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu utafunuliwa,
na watu wote pamoja watauona.
Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hayo.”
6Sikiliza! Kuna sauti inasema, “Tangaza!”
Nami nikauliza, “Nitangaze nini?”
Naye: “Tangaza: Binadamu wote ni kama majani;
uthabiti wao ni kama ua la shambani.
7Majani hunyauka na ua hufifia,
Mwenyezi-Mungu avumishapo upepo juu yake.
Hakika binadamu ni kama majani.
8Majani hunyauka na ua hufifia,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9Nenda juu ya mlima mrefu,
ewe Siyoni, ukatangaze habari njema.
Paza sauti yako kwa nguvu,
ewe Yerusalemu, ukatangaze habari njema.
paza sauti yako bila kuogopa.
Iambie miji ya Yuda:
“Mungu wenu anakuja.”
10Bwana Mungu anakuja na nguvu,
kwa mkono wake anatawala.
Zawadi yake iko pamoja naye,
na tuzo lake analo.
11Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
atawakusanya wanakondoo mikononi mwake,
atawabeba kifuani pake,
na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole.
Mungu wa Israeli hana kifani
12Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake,
kuzipima mbingu kwa mikono yake?
Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni;
kuipima milima kwa mizani
au vilima kwa kipimo cha uzani?
13 Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu,
au kuwa mshauri wake na kumfunza?
14Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri,
ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi?
Nani aliyemfunza njia za haki?
Nani aliyemfundisha maarifa,
na kumwonesha namna ya kuwa na akili?
15Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo,
ni kama vumbi juu ya mizani.
Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini.
16Kuni zote za Lebanoni
na wanyama wake wote
havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake.
17Mataifa yote si kitu mbele yake;
kwake ni vitu duni kabisa na batili.
18Mtamlinganisha Mungu na nini basi,
au ni kitu gani cha kumfananisha naye?
19Je, anafanana na kinyago?
Hicho, fundi hukichonga,
mfua dhahabu akakipaka dhahabu,
na kukitengenezea minyororo ya fedha!
20Au ni sanamu ya mti mgumu?
Hiyo ni ukuni mtu anaochagua,
akamtafuta fundi stadi,
naye akamchongea sanamu imara!
21Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Je, hamkuambiwa tangu mwanzo?
Je, hamjafahamu mwanzo wa dunia?
22Dunia iliumbwa na huyo aketiye juu ya mbingu;
kutoka huko wakazi wa dunia ni kama panzi!
Yeye amezitandaza mbingu kama pazia,
na kuzikunjua kama hema la kuishi.
23Yeye huwaporomosha wakuu wenye nguvu,
watawala wa dunia huwafanya kuwa si kitu.
24Mara tu wanaposimikwa na kuanza kuota,
hata kabla hawajatoa mizizi kama miti udongoni,
Mwenyezi-Mungu akiwapulizia hunyauka,
kimbunga huwapeperusha kama makapi!
25Mungu Mtakatifu auliza hivi:
“Nani basi, mtakayemlinganisha nami?
Je, kuna mtu aliye kama mimi?”
26Inueni macho yenu juu mbinguni!
Je, ni nani aliyeziumba nyota hizo?
Ni yule aziongozaye kama jeshi lake,
anayeijua idadi yake yote,
aziitaye kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi,
hakuna hata moja inayokosekana.
27Enyi watu wa Israeli wazawa wa Yakobo,
kwa nini mnalalamika na kusema:
“Mwenyezi-Mungu hatujali sisi!
Mungu wetu hajali haki yetu!”
28Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu wa milele;
yeye ndiye Muumba wa kila kitu duniani.
Yeye hafifii kamwe wala kuishiwa nguvu.
Maarifa yake hayachunguziki.
29Yeye huwapa uwezo walio hafifu,
wanyonge huwapa nguvu.
30Hata vijana watafifia na kulegea;
naam, wataanguka kwa uchovu.
31Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu,
watapata nguvu mpya.
Watapanda juu kwa mabawa kama tai;
watakimbia bila kuchoka;
watatembea bila kulegea.
Isaya40;1-31
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Wednesday, 23 October 2019
Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 39....
Wajumbe kutoka Babuloni
(2Fal 20:12-19)
1Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani, mfalme wa Babuloni, aliposikia kwamba Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, alimtumia ujumbe pamoja na zawadi. 2Basi, Hezekia aliwakaribisha na kuwaonesha nyumba ya hazina: Fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani, vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakuna chochote katika ikulu yake au katika nchi yake ambacho hakuwaonesha.
3Ndipo nabii Isaya alipokwenda kwa mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu “Wamenijia kutoka nchi ya mbali, huko Babuloni.” 4Halafu Isaya akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”
5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi: 6Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya wazee wako hadi leo, vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. 7Tena baadhi ya watoto wako mwenyewe wa kiume watapelekwa mateka nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.” 8Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu ulilosema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kutakuwa na amani na usalama muda wote niishipo.”
Isaya39;1-8
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Tuesday, 22 October 2019
Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 38....
Mfalme Hezekia anaugua
(2Fal 20:1-11; 2Nya 32:24-26)
1Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.”
2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu, 3akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.
4Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya: 5“Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. 6Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.”
21Basi, Isaya akasema, “Chukueni andazi la tini mkaliweke kwenye jipu lake, apate kupona.”38:21-22 aya ya 21-22 zimehamishiwa hapa kuleta maana yake kamili katika simulizi hilo. 22Hezekia akauliza, “Ni ishara gani itakayonijulisha kwamba mimi nitakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?” 7Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi. 8Nitafanya kivuli kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi, kirudi nyuma hatua kumi.” Nacho kivuli kikarudi nyuma hatua kumi.38:8 ngazi … hatua kumi … hatua kumi: Au Kwenye saa ya jua … hatua kumi … hatua kumi.
9Kisha mfalme Hezekia alipopona, akatunga wimbo huu wa shukrani:
10“Nilisema: Nikiwa mbichi kabisa,
inanibidi niage dunia.
Mimi nimepangiwa kwenda kuzimu
siku zote zilizonibakia.
11Nilisema sitamwona tena Mwenyezi-Mungu,
katika nchi ya walio hai;
wala sitamwona mtu yeyote tena,
miongoni mwa wakazi wa ulimwengu.
12Makao yangu yamengolewa kwangu,
kama hema la mchungaji;
kama, mfumanguo nimefungasha maisha yangu;
Mungu amenikatilia mbali;
kabla hata mwisho wa siku amenikomesha.38:12 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
13Usiku kucha nililia kuomba msaada;
kama simba, anavunjavunja mifupa yangu;
mchana na usiku ananikomesha.38:13 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
14“Ninalia kama mbayuwayu,
nasononeka kama njiwa.
Macho yangu yamefifia kwa kuangalia juu.
Ee Bwana, nateseka;
uwe wewe usalama wangu!
15Lakini niseme nini:
Yeye mwenyewe aliniambia,
naye mwenyewe ametenda hayo.
Usingizi wangu wote umenitoroka
kwa sababu ya uchungu moyoni mwangu.
16“Ee Bwana, Sisi twaishi kutokana na yote uliyotenda,
kwa hayo yote mimi binafsi pia ninaishi.38:16 aya hii maana ya Kiebrania si dhahiri.
Nirudishie afya, uniwezeshe kuishi.
17Nilipata mateso makali kwa faida yangu;
lakini umeyaokoa maisha yangu
kutoka shimo la uharibifu,
maana umezitupa dhambi zangu nyuma yako.
18Huko kuzimu mtu hawezi kukushukuru wewe;
waliokufa hawawezi kukushukuru wewe.
Wala washukao huko shimoni
hawawezi tena kutumainia uaminifu wako.
19Walio hai ndio wanaokushukuru,
kama na mimi ninavyofanya leo.
Kina baba huwajulisha watoto wao uaminifu wako.
20“Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
Nasi tutamsifu kwa nyimbo za vinubi
siku zote za maisha yetu,
nyumbani kwake Mwenyezi-Mungu.”
Isaya38;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
Subscribe to:
Posts (Atom)